Mimi naomba kuunga mkono hoja iliyotolewa kuhusu hizo kampuni za kina Kinje, kuanzia hiyo iliyopewa tenda ya Ubungo Bus Terminal, na hiyo ya kuegesha magari mjini, Tanzania Parking Services, kama ifuatavyo:
1) Ubungo Bus Terminal ni vurugu tupu. Kuanzia nje hadi ndani, hakuna kinachoeleweka. Hakuna mpango hakika wa huduma kwa wanaotoa huduma na wanaopokea huduma. Hakuna usalama wa uhakika. Nje ya hiyo terminal kumejaa wezi, vibaka na matapeli. Unaweza kurubuniwa - kama wewe si 'mtoto wa mjini' (hehe, mimi hawanipati) - na kuambiwa kuna basi linaondoka 'fasta fasta'. Wewe na haraka zako, ukawafuata wale watu mpaka ndani. Kumbe wameshakula njama na mtu ambaye atakuwa na kitambulisho bandia, kuonesha kwamba yeye ni mkataji tiketi wa hilo basi; tena amevaa sare za kampuni hiyo ili kukupa matumaini na uhakika kwamba 'huingizwi mjini'. Wale ambao ni wafanyakazi halali wa kampuni ya hilo basi, kwa wakati huo, wako kimya, wakikutazama, kwani wanajua kwamba kwenye hizo pesa utakazokatishwa tiketi bandia kuna mgao wao! Unakata tiketi, unakaa kwenye kiti 'chako' ndani ya basi tayari kusubiri safari kuanza. Mara basi linaanza safari yake, anaingia kondakta wa basi na mkaguzi wa tiketi. Anapofika kwako unampa tiketi uliyokatishwa, hapo ndipo kizaa-zaa kinapoanza. Unaambiwa "Tiketi hii si yetu. Tunaomba utulipe fedha zetu au ushuke nje." Nadhani mnajua kinachoendelea baada ya hapo.
Kampuni ya kina Kinje mbona haiweki watu wa kuhakikisha kwamba wanaokata tiketi wanatambuliwa rasmi, kwa mfumo mzuri zaidi wa utambulisho? Mbona haiwajibiki kuweka matangazo kuwatahadharisha wateja kwamba, kwa hali yoyote ile, wasikate tiketi NDANI ya eneo la terminal, ila, wakate tiketi zao kwenye ofisi maalum zilizo kwenye uzio wa terminal hiyo?
2) Tukienda kwenye hawa wanaotoza wenye magari ada ya maegesho ya magari, kule ni tabu tupu. Si tu kwamba haieleweki nani mwenye wajibu wa kutoa huduma za ulinzi wa magari yanayoegeshwa, bali pia, inasadikika kwamba baadhi ya watoza kodi hao hushirikiana na vibaka wanaoiba vifaa kwenye magari, kama vile side mirrors, radio, etc. Hii inatokana na ukweli kwamba watoza kodi hao HAWAAJIRIWI kama wafanyakazi, ila wanaajiriwa kama vibarua, yaani, CASUAL LABOURERS! Pia, wanawekewa viwango maalum (quota) vya makusanyo ya ada za maegesho kwa kila siku na kila wiki. Wasipovifikia (viwango ambavyo, kutokana na hali halisi si rahisi kuvifikia), huachishwa kazi na kufukuzwa kama mbwa. Wapo vijana wengi tu ambao 'wamepitia' ajira za 'wiki moja' kama watoza kodi ya maegesho ya magari jijini Dar, na watakuambia yaliyowasibu! Kiwango kikubwa cha Shs. 30,000/= kwa wiki kufikiwa si rahisi. Kwa wasichana, wengi wao wanalazimika 'kutembea' na mabosi wa kampuni hiyo ili wasifukuzwe kazi, kwani ukweli ni kwamba hali mbaya ya uchumi inawafanya vijana kufanya kazi aina yoyote ile, hata kama kazi hiyo itahatarisha afya zao. Kwa akina dada, wengi wao hulazimishwa kufanya ngono bila kinga, jambo ambalo linachangia kueneza kasi ya maambukizi ya UKIMWI!
Nyie mnaosema hoja hii isijadiliwe hapa mnakosea, kwani kina Kinje na wenzake wanarithishwa na kuendeleza ufisadi! Ufisadi, kwa hali yoyote ile, lazima ujadiliwe, na lazima upingwe!
Wewe unayekataa tusijadili hili suala, basi, mimi binafsi nina mashaka nawe, kwani wewe pia, kwa kukataa hoja hii, moja kwa moja nawe ni FISADI!
Siogopi kusema! Nitasema tu! Mtake msitake! Kwani, kama hujajua bado, Ibara ya 18 (1) na (2) inanipa uhuru wa kutoa maoni yangu. Kwa maoni yangu, mkataa pema pabaya panamwita... unaitwa FISADI kwa kuwa unakataa tusijadili ufisadi huu!
Bora niende kaburini nikitetea haki, kwani walio wengi, wanyonge, wamepokwa haki yao, kuliko kukaa kimya na kuwa mwoga, nikisema, naogopa kufa, au si kazi yangu kusema!
./Mwana wa Haki!