Fikra zangu

omiry1

Member
Oct 3, 2015
6
45
Kiongozi ni kama mwendesha farasi, akiwa bora atamwendesha farasi katika mwelekeo maalumu lakini akiwa hajui kumweka sawa farasi atayumbishwa, ni lazima ajue kumshika vizuri farasi na kumwelekeza sehemu ya kwenda. Kiongozi mbovu husababisha farasi kukosa mwelekeo.

Wananchi wanapokosa viongozi wazuri hukosa mwelekeo kama taifa. Nchi hukosa utaratibu na mpangilio. Matumaini ya waliowengi hupotea.
Ni lazima siasa zetu ziendane na mantiki pamoja na dhamira ya dhati ya kulisongesha taifa letu mbele na sio porojo. Ni lazima wanasiasa wetu wawe wazalendo na kuamua yale yaliyo bora kwa manufaa ya taifa.

Pale tu siasa zetu zitakapokuwa na mantiki watu wetu wengi watarudisha hisia za uzalendo kwa taifa lao na watakuwa tayari kwa kulitumikia.

Ni lazima tujue siasa ni chombo pekee ambacho kitatusaidia kuharakisha maendeleo yetu.
Pale siasa inapokuwa nzuri katika nchi, maendeleo ni lazima yaje. Ni siasa pekee inayowaunganisha watu katika malengo mamoja ya utaifa na kuleta mwelekeo. Inapokuwa nzuri huwa na tija kwa wananchi wote. Lakini inapokuwa mbaya huleta fujo na mgawanyiko.


Kwahiyo kujitambua kwa wanasiasa ni muhimu sana. Kujitambua kwao kunajenga na kudhibiti kauli zitakazoleta mgawanyiko ndani ya jamii zetu. Kuna nguvu kubwa katika maneno ya wanasiasa ni muhimu wote kutambua hilo.

Kwahiyo kiongozi mzuri ni yule anayechagua maneno yenye faida na yanayojenga taifa, anayejua kuelekeza katika njia iliyo sahihi, anayeongea masuala ambayo yataonekana dhahiri ni yenye mantiki katika macho ya raia.

Mwelekeo wa taifa hautapatikana kama viongozi wetu hawatokuwa na mwelekeo na kujua ni nini wanajenga na kwa wakati gani.Mkondo wa mawazo ya viongozi mara nyingi huwa mkondo wa wananchi. Wananchi hukosa dira pale viongozi wanapokosa dira.

Mawazo ya wananchi ni lazima yaelekezwe katika mwelekeo fulani, kazi ya kuelekeza mawazo haya ni kazi ya viongozi, bila raia kuelekezwa katika mkondo fulani wa mawazo hakika hatutaweza kupata mafanikio, ikiwa mawazo ya wananchi wetu yakiwa yametawanyika na bila kuwa na mwelekeo fulani. Ni muhimu kutambua hili taifa ni lazima liwe na malengo.

Malengo haya ni lazima yapandikizwe katika kila moyo na akili za mwananchi. Wajenzi wa taifa hili ni wananchi, viongozi wasifikiri wataleta maendeleo kwa wananchi bila wananchi kushiriki katika ujenzi wa taifa lao wenyewe.

Ni lazima wakumbuke wao viongozi ni waratibu tu lakini kazi kubwa ya ujenzi wa taifa hufanywa na raia wenyewe. Na ulinzi wa maliasili na wa taasisi zao ni jukumu lao. Ni lazima wajengewe wajibu huu kwa taifa lao.Ni lazima wahisi hili ni taifa ni lao. Na jukumu la kulipeleka taifa hili mbele ni la kila mmoja wetu. Wananchi wakishajengewa wajibu huu na kufahamu vizuri na kisha kuelewa kwanini tuko kama taifa na kwa faida gani, wana wajibu gani kwa taifa na kwa jamii, itakuwa rahisi kwao kulinda mali za umma na kuzipenda taasisi zao zinazo wahudumia.

Wakijitambua itakuwa rahisi sana kushinikiza sheria ili kulinda utaratibu. Hisia hii ya raia kwa taasisi zao ni muhimu, hisia ya mapenzi na kujitolea ili kuona taasisi zinazohudumia raia zikiendelea.

Wajibu huu wa mtu kwa jamii yake na taifa lake ni muhimu sana. Wakielewa taasisi hizi ni mali yao na zipo kwa faida yao na kwa vizazi vijavyo nafikiri mtazamo wao utabadilika.

Ni lazima wajue taasisi zote sio mali ya serikali ni mali yao. Wana wajibu wa kuzilinda na kuziendeleza.
Ni lazima tujenge wajibu huu katika jamii yetu. Binadamu ni lazima awajibike kwa jamii yake. Kutoweka kwa nidhamu hii ndio chanzo cha mambo mengi. Na taifa letu limekosa pia utaratibu sababu ya nidhamu hii kutoweka.

Haya ni mambo ambayo ni lazima tufanye ili taifa letu lirudi katika mstari. Ni kwa kuwajibika huku kwa jamii ndipo tutakapojenga jamii iliyobora. Kukikosekana kuwajibika huku hatutafika mbali kama taifa.

Kukiwepo na kuwajibika huku hakuna mtu atakayemuuzia mwenzake bidhaa bandia mfano au kutokuchukulia maanani majukumu aliyopewa na jamii katika nyanja mbali mbali.

Iwe mwalimu, daktari au mhandisi. Tukiisha wajengea wajibu huu watu wetu. Itakuwa rahisi sana kushinikiza sheria kufanya kazi yake kwa watu wenye uelewa wa kutosha kuhusu wajibu wao kwa jamii. Pasipo elimu hii, raia wetu watakuwa waoga tu wa sheria lakini wakipata nafasi ya kufanya uhalifu watafanya.

Ni lazima tufahamu ujenzi wa taifa ni wajibu wa raia wote, taifa huimarika pale raia wote waposhiriki katika ujenzi wa taifa, uendelezaji wake na ulinzi wake.

Taifa hili litaendelea kuwepo ikiwa watu wote watashiriki katika ujenzi wake kwa kujitambua.
Watu wenye mawazo bora ni lazima washiriki katika kufanya taifa hili liwe bora zaidi na la kuvutia. Ni kwa mawazo chanya pekee ndipo tutakapo lijenga taifa hili.

Ni kwa watu ambao wanaojadili njia za kutatua matatizo yaliyopo sasa hivi ili kuleta maendeleo ndio watakao linyanyua taifa hili sio watu wanaojadili kila wakati matatizo ya taifa.

Ili tulijenge taifa hili kwa ustadi ni lazima tulipende. Upendo huu kwa taifa ndio utakaotufanya tuwe na juhudi zaidi na ubunifu zaidi kusudi lipendeze.

Ni lazima tusahau yaliyopita na tuangalie ya mbele sasa hivi, tujenge taifa zuri zaidi kwa kuwa na mawazo mazuri zaidi na chanya juu ya taifa letu.

Ni lazima tusahau mgawanyiko wetu na kuleta umoja katika malengo.Ni lazima tukusanye mawazo yetu na tuyaekeze katika mkondo uliobora zaidi wa kufanya taifa hili liwe zuri.

Tunaweza kufanya hivi kwasababu mawazo yetu ndio yanayojenga. Ubora wa mawazo yetu ndio ubora wa taifa.

Ni muhimu kufahamu kama taifa letu lina magugu ni kutokana na fikra na mawazo yetu mabaya.
Fikra na mawazo mazuri hutengeneza taifa zuri. Tunachohitajika sasa hivi ni kubadilisha fikra na mawazo yetu ili tujenge taifa imara na lililobora.

Taifa ambalo mtu atafikiria jamii kwanza kabla hajafanya kitu chochote. Tukifika huko tutakuwa tumekomaa kiakili na tutajenga taifa imara la watu wanaoshirikiana kuleta maendeleo yao wenyewe.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom