Fikra za Nyerere zitumike kuchagua viongozi bora | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Fikra za Nyerere zitumike kuchagua viongozi bora

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by MziziMkavu, Oct 15, 2010.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Oct 15, 2010
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,615
  Trophy Points: 280
  Miaka 11 tangu Baba wa Taifa, Mwalimu Julias Nyerere alipofariki dunia, ni muhimu taifa kukumbuka juhudi zake za kumkomboa Mtanzania kutoka katika ujinga, maradhi na umaskini ambavyo hata hivyo bado vimekithiri miongoni mwa wananchi.
  Wakati tukiadhimisha miaka 11 ya kuondokewa na Mwalimu Nyerere, taifa linashiriki  Uchaguzi Mkuu wa nne tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, 1992.
  Zipo hotuba nyingi alizozitoa Mwalimu Nyerere, zikiwa katika mfumo wa maneno na nyingine kwenye maandishi. Watanzania na jamii nyingine duniani, tunaendelea kuzitumia kama nukuu zenye kuielimisha jamii pana.


  Wakati tunaadhimisha miaka 11 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, ni vizuri kuijadili moja ya hotuba hizo aliyoitoa kupitia kitabu chake cha Mei 1962, alipokuwa Rais wa Tanganyika African National Union (TANU), kikaitwa “ Tujisahihishe’.
  Maudhui ya kitabu hicho yanaweza kuongeza maarifa na nguvu za Watanzania katika  kuwachagua viongozi bora katika uchaguzi wa mwaka huu.
  Itakumbukwa kwamba wakati wa uhai wake, Mwalimu Nyerere alipinga mambo mengi yanayorudisha nyuma maendeleo ya nchi na watu wake. Miongoni mwa hayo ikiwa ni unafsi (ubinafsi), fitina, rushwa, uongo, uhujumu wa mali za umma (ufisadi) na uvivu wa kufikiri.


  Mwalimu Nyerere hakuyapenda hayo kwa hofu kuwa, Tanganyika (wakati huo), ingeweza kuangukia kwenye matatizo makubwa ya kiuongozi, kama ilivyo sasa kwa viongozi wetu.
  Katika pitio la kitabu hicho, suala la ubinafsi alilichukulia kama donda ndugu, yaani likimpata mtu yeyote haliwezi kupona, na hapo aliandika, “matatizo mengi hutokana na unafsi, unafsi ni wa aina nyingi, swali ambalo twalisikia mara kwa mara, ni hali yetu ya baadaye itakuaje?”


  “Ni swali ambalo sina shaka kuwa kuna watu wanaoliuliza kwa nia safi kabisa, lakini mara nyingi linatokana na unafsi.”
  Anaendelea kuandika kwamba mtu anayeuliza na anafikiri kuwa TANU (kwa sasa CCM) iliundwa kwa faida yake binafsi, na kwamba chama kiliundwa ilimradi kuwa ikiwa atakubali kuwa mwanachama au kiongozi, basi chama hicho kitamfanyia jambo fulani kama tuzo,  huku anasahau kabisa kuwa lengo ni kujishughulisha na haja za wananchi kwa ujumla.
  Akaandika: “lakini kwa mtu wa aina hiyo, hata kama TANU inatimiza madhumuni yake ya jumuiya, ataona kuwa ni umoja ambao hauna maana kwa sababu hautimizi haja zote za nafsi yake, huu ni unafsi.”


  Akasema katika kitabu hicho kuwa kama wanachama wa TANU na hasa viongozi, hawatakihukumu chama hicho kwa mahitaji ya jumuiya, bali kwa mahitaji ya nafsi zao, kamwe hakitadumu kwa vile uanachama wa namna hiyo ni ugonjwa katika chama.
  Ni dhahiri kwamba Baba wa Taifa alishayaona hayo zaidi ya miaka 49 iliyopita. Kinachojitokeza hivi sasa katika chama tawala kilichotokana na TANU ni sehemu ya maono hayo.


  Kuna dalili na ishara za wazi kwamba viongozi na wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi hivi sasa, wamemiliki maslahi yaliyo ya umma, tena kwa kutumia njia zisizokuwa halali.
  Katika kitabu hicho, Mwalimu Nyerere anazungumzia dalili nyingine ya unafsi kuwa ni fitina. Kanuni mojawapo ya TANU ikasema hivi: “nitasema kweli daima fitina kwangu ni mwiko.”


  Lakini hivi sasa viongozi na wanaogombea uongozi hasa kupitia CCM, wanaitekeleza vipi dhana hiyo? Kimsingi ni sawa na kusema ahadi hiyo hivi sasa haina mtekelezaji na kama wapo ni wachache wa kuhesabu.
  Hili linadhihirishwa na viongozi wetu wanaotafuta fursa mbalimbali za kisiasa kwa lengo la  kujinufaisha, huku wakitumia fitina na uongo uliokubuhu, kutoa ahadi zisizoweza kutekelezeka.
  Lakini wakati tunaadhimisha miaka 11 ya kifo cha Mwalimu Nyerere, na takribani miaka 49 ya uhuru, ni muhimu tutafakari dhamira za viongozi waliopo na wanaotaka uongozi, kwani idadi ya viongozi na wanachama wafitini ambao kimsingi ni wasaliti wa Mwalimu, imeongezeka.


  Ifahamike kwamba kosa linatokana na unafsi, linafanyika kila siku na wakati mwingine, linafanywa na viongozi kwa makusudi, hivyo jamii inapaswa kuwa makini hasa kipindi hiki cha kampeni na hatimaye Uchaguzi Mkuu.
  Inaaminika kwamba viongozi wa umma wanastahili kutokana na umma pasipo hila, vitisho, rushwa au ujanja wa aina yoyote.


  Lakini mara nyingine wananchi wanafanya makosa kwa kuwachagua viongozi wasiozingatia maadili ya uongozi, hili ni jambo la hatari kwa demokrasia na taifa.
  Hivyo, kila mwananchi aliyetimiza masharti ya upigaji wa kura mwaka huu, anapaswa kuwachagua viongozi bora, wasiotoa rushwa na wenye kufuata maadili stahiki ya uongozi.


  Haifai hata kidogo kumchagua kiongozi anayetoa rushwa na kuhonga vitu kama kofia, fulana, kanga, pipi, biskuti, wali, pilau, pombe au kitu chochote chenye kutoa ushawishi ili achaguliwe.
  Pia haifai kumchagua kiongozi kwa sababu ya kutoa fursa zenye maslahi ya kiuchumi, kama kupewa nafasi ya kuimba kwaya wakati wa kampeni ama kutokana na kufanya kazi  ya kubandika mabango ya kujinadi kwa wapiga kura na kupata posho kwa siku kadhaa.**
  Haifai kumchagua mtu kuwa kiongozi kwa sababu ya undugu, mathalani kuamini kwamba mtu mwenye uhusiano wa karibu kama mjomba, shangazi, shemeji, binamu ama wifi, anafaa kuwa kiongozi wa umma.


  Kiuhalisia mambo aliyozungumzia Mwalimu Nyerere yapo na yanatuzunguka katika maisha yetu ya kila siku, huku yakiathiri kwa kiwango kikubwa maendeleo ya jamii na taifa kwa jumla.


  Wapo wagombea wanaobezwa kutokana na kuwa na kiwango kidogo cha elimu. Hoja ambayo kwa Mwalimu Nyerere haikuwa na nguvu kiasi hicho.
  Tafsiri ya elimu kwa Mwalimu Nyerere, iligusia ufanisi katika kutafuta ukweli wa mambo na kwamba kupata elimu katika mfumo rasmi kama shule, kunasaidia kuufikia ukweli huo kirahisi.


  Lakini japo kwa sasa kuna walioshindwa kupata elimu ya juu, jamii inaweza kujifunza jambo moja, kwa mfano jimbo la uchaguzi linakabiliwa na ukosefu wa maji. Baada ya kujua sababu zake lazima fursa ya kujielimisha ifikiwe kwa kutafuta njia zinazoweza kulipatia maji jimbo husika.


  Jambo la maana ni kuzipa akili uhuru kamili na kutafuta elimu bila kutia kiini macho na utashi wa nafsi, hasa wakati huu wa uchaguzi ambapo elimu ya mpiga kura inahitajika sana, ili kuwapata viongozi bora wenye utashi kamili wa kuwatumikia watu.
  Mawazo haya stahiki ya Mwalimu Nyerere ni muhimu kutiliwa mkazo wakati wa  kuadhimisha miaka 11 ya kifo chake na miaka 49 ya uhuru wa Tanzania.
  Muda umefika wa kuacha kulalamika kutokana na umaskini uliokithiri katika jamii zetu, kwani kipindi hiki cha uchaguzi ni fursa muhimu ya kuchukua hatua ya kuchagua viongozi bora watakaoleta maendeleo stahiki.


  Gideon Mwakanosya analiandikia NIPASHE kutoka mjini Songea. Anapatikana katika simu namba 0754 928752 au 0715 928752. Pia kwa barua pepe: gideonmwakanosya@yahoo.com"  CHANZO: NIPASHE
   
Loading...