Bilionea Asigwa
JF-Expert Member
- Sep 21, 2011
- 16,515
- 28,487
KIASI cha Sh. bilioni 2.8 zilizokuwa zitumike kwa ajili ya semina elekezi kwa mawaziri, zitatumika kununua vifaa vya kuangalia mwenendo wa afya za mgonjwa na uchunguzi, ikiwemo mashine za CT-scan katika hospitali za rufaa za mikoa nchini.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Kemirembe Lwota, aliyetaka kujua serikali itapeleka lini mashine ya X-ray na CT-scan kwenye Hospitali ya Mkoa wa Mwanza ya Sekouture.
Jafo alisema mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano baina ya serikali ya Tanzania na Uholanzi na utakapokamilika hospitali nyingi za rufaa za mikoa zitakuwa na vifaa muhimu kwa ajili ya huduma za afya.
Alisema Hospitali ya Sekoture ina mashine mbili za X-ray ambazo zilinunuliwa na serikali 2002 na zinafanya kazi pamoja na kuwapo kwa matengenezo ya kuharibika mara kwa mara kutokana na uchakavu wake.
"Hospitali hiyo haina mashine ya CT-scan na huduma hiyo kwa sasa inapatikana katika Kospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando,"alisema Jafo.
Katika swali la nyongeza, Mbunge huyo alihoji ni lini serikali itanunua mashine hizo kwa ajili ya hospitali hiyo kutokana na wananchi wa Mwanza wanapata shida ya kupata vipimo hivyo na kulazimika kwenda kwenye hospitali za binafsi ambazo zinagharama kubwa.
Akijibu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema mbali na mradi huo, pia zimepatikana fedha ambazo zilikuwa zitumike kwenye semina elekezi ya mawaziri Sh. bilioni 2.8 ambazo zitatumika kununulia vifaa hivyo.
"Fedha imeshatolewa, hivyo muda wowote vifaa vitasimikwa katika hospitali zote za rufaa za Tanzania, suala hili litafanyika kabla ya mwaka wa fedha 2015/16 kumalizika," alisema Mwalimu.
Source: Nipashe