Faru John wajanja walishamnywa kitambo, pembe zilizoonyeshwa ni za faru "Hadija"

Return Of Undertaker

JF-Expert Member
Jun 12, 2012
4,572
26,885
Source Jamuhuri
IMG_20161227_051156.jpg


Faru John wamemnywa
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, amekalia kuti kavu baada ya taarifa kuanza kuvuja na kuonesha kuwa aliwasilisha pembe za faru ‘feki’ kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Taarifa za uhalisia wa pembe alizowasilisha zinaacha maswali mengi baada ya JAMHURI kuhojiana na watu zaidi ya 50 wakiwamo wahifadhi.

Baadhi ya waongoza watalii wanasema Faru John ‘wamemnywa’ kwa maana kuwa wamemuua makusudi na kuuza pembe zake, lakini hali ilivyobadilika kutoka na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuagiza uchunguzi wa kina, sasa wanahaha kuhalalisha taarifa za uongo walizompa.

“Faru John wamemnywa. Yeye alikuwa na pembe zilizochongoka kiajabu. Pembe zake zilikuwa na ukubwa usiotofautiana. Hizi pembe butu walizomkabidhi Waziri Mkuu ni za Faru Hadija. Hata uzito wa kilo mbili walizosema siyo kweli,” anasema mmoja wa waongoza watalii.

Wakati mtoa taarifa huyo akisema hivyo, wahifadhi katika Mbuga ya Ngorongoro na Pori la Akiba la Grumeti wanasema hajawahi kuwapo faru mwenye jina la Hadija na Waziri, Prof. Jumanne Magembe, anasema pembe za Faru John ziliishakatwa kuondoa ncha.

“Pembe za Faru John zilikuwa na uzito wa kilo saba. Waziri Mkuu amepewa zenye uzito wa kilo mbili. Hii ni aibu. Wabanwe na waziri awajibishwe kwa kushiriki uongo huu. Hata kaburi la Faru John halipo, na hapa Grumeti hakuna mbwa mwitu na fisi wa kula mzoga wa faru kama John na kuumaliza. Waseme pembe halisi zimekwenda wapi,” amesema mmoja wa walinzi.

Waziri Maghembe na timu yake wamewasilisha pembe mbili kwa Waziri Mkuu Majaliwa wakidai ndizo za Faru John, lakini baada ya kuwataka wawasilishe vipimo vyenye kujumuisha vinasaba, ghafla wamegeuka na kusema kuwa faru huyo hakuzikwa bali aliachwa akaliwa na wanyama.

Waziri Mkuu Majaliwa akiwa ziarani wilayani Ngorongoro, Arusha Desemba 5, 2016 amewataja kwa majina baadhi ya wahifadhi na kusema waliahidiwa Sh milioni 200, na wakapewa fungu la awali la Sh milioni 100 kumhamisha Faru John na kutimiza matakwa yao ya kumuua.

Hali halisi

Ni dhahiri kwamba Faru John amekufa, ila kitendawili ni juu ya taratibu na nia ya uhamishwaji wake kutoka makazi yake ya asili ambayo aliishi kwa miaka 37 na kupelekwa Grumeti Singita, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.

Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kwamba awali taarifa ya wataalamu, iliyohusisha Idara ya Wanyamapori, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Wakala wa Wanyamapori ilipendekeza apelekwe katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, lakini kinyume chake akapelekwa Grumeti Singita.

Taarifa ya wataalamu hao, ambayo JAMHURI imeiona, ilizingatia mambo mengi kuhakiisha faru huyo haathiriwi na mazingira, badala yake kwa matakwa na maslahi yasiyofahamika akapelekwa Grumeti Singita, sehemu ambayo wanyama wanaishi ndani ya uzio.

“Tulikubaliana timu ya wataalamu kwamba lazima Faru John apelekwe Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi… mamlaka yetu sisi yaliishia kwenye kushauri kitaalamu, lakini hayo mambo mengine yaliyofanyika yanatakiwa kujibiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro,” anasema mmoja wa wataalamu walioshiriki kuandaa taarifa ya kumhamisha Faru John.

Akieleza sababu zilizowafanya wataalamu kufikia hatua ya kumhamisha Faru John, mtoa habari wetu amesema faru huyo alikuwa na tabia ambazo hazikuwa za kawaida akiwa ndani ya ‘kreta’ ya Ngorongoro, kwani alifikia hatu ya kufanya mapenzi mpaka na faru watoto, hali ambayo ilianza kusababisha usumbufu kwa faru wengine katika ‘kreta’ hiyo.

Faru John amekufa?

Kwa mujibu wa chanzo chetu ndani ya Grumeti Singita, kifo cha Faru John kinaonesha ambavyo mamlaka hazikumjali hata baada ya kupewa taarifa za kifo hicho.

“Baada ya Faru John kufa, mamlaka hapa zilitoa taarifa kwenye Idara ya Wanyamapori. Lakini kaka huwezi kuamini hawakuja kuchukua nyara (pembe) hizo mpaka pale Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipoonekana kuchachamaa akimhitaji Faru John akiwa mzima ama amekufa.

“Taarifa pengine zilikuwa zikipuuzwa tu, na inawezekana hilo pia ndilo linalomfanya Waziri Mkuu ahisi kuna kitu hapo. Maana kama walikuwa wanaambiwa waje kuchukua nyara na majibu yao yalikuwa ni kwamba wanasubiri kupata ndege ndipo waje, lakini baada ya suala hili kuwa mada moto, wamekuja haraka na kuchukua nyara hizo, hii inatia shaka,” kinasema chanzo chetu.

Taarifa zaidi zinasema kuwa Faru John alianza kudhoofu mara baada ya kufikishwa hapo Grumeti Singita. Timu ya madaktari wawili mmoja kutoka Ngorongoro na mwingine kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) wamekuwa wanakwenda kumtazama bila kutoa matibabu.

“Wamekuwa wanakuja hapa madaktari wawili baada ya kuwa wanapewa taarifa za afya ya Faru John… Wamekuwa wakija hapa kumwangalia, lakini sikuwahi kuona akipatiwa matibabu yoyote, badala yake wakawa wanasema akidhoofu zaidi wapatiwe taarifa. Nadhani hapo kinachogomba ni posho. Wamekuwa wakila posho tu bila kujali afya ya Faru John,” anasema mmoja wa askari ambaye alikuwa akimlinda faru huyo.

Madaktari waliku wanalipwa Sh 500,000 kwa siku na Grumeti na inaelezwa kuwa walikuwa hawampi matibabu yoyote zaidi ya kufurahia kuendelea kupata posho, hali iliyosaidia kumdhoofisha hadi kifo chake na wao wakatekeleza mpango wao haramu.

Serengeti wakataliwa

Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti waliomba kumchukua Faru John alipotajwa kuwa na vurugu, lakini maombi yao hayakujibiwa. Kwa mshangao walisikia na kuona Grumeti Singita, ambayo ni kampuni binafsi inaomba na kupewa haraka haraka faru huyo. Kikao cha kupitisha maombi ya Grumeti kilipitishwa haraka haraka kwa ushirikiano na Ikorongo Game Reserve.

Faru John amekuwa akilindwa na askari 9, huku kila mmoja akilipwa Sh 25,000 kwa siku na amelindwa kwa miezi minane kabla ya kufa kwake. Faru John amekuwa analindwa kwa Shilingi 225,000/- kwa siku. Katika kipindi cha miezi 8 aliyokaa katika eneo hilo, zimetumika zaidi ya Sh milioni 54, kumlinda.

Faru huyo alikuwa akilindwa na askari wa taasisi nne tofauti. Askari Wanyamapori wa Ikorongo, Kikosi Maalumu cha Kupambana na Ujangili (KDU), askari wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na Grumeti Singita.

Kaimu wa Meneja wa Pori la Akiba la Ikorongo, lililoko wilayani Serengeti, Dickson Mrema, alimwekea masharti magumu mwandishi wa habari hizi, huku akitaka apatiwe barua iliyosainiwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mali Asili na Utalii.

Mrema aliomba kupatiwa vitambulisho na mwandishi, lakini hata baada ya kupatiwa vitambulisho aling’aka na kusema hawezi kuruhusu chochote kufanyika.

“Siwezi kukuruhusu… Haya ni maelekezo. Hata kama ukimpigia simu Waziri au Katibu Mkuu, siwezi kukuruhusu kupita hapa kuingia huko Grumeti Singita, ila kama ukiwasiliana na Katibu Mkuu, Meja Generali Gaudence Millanzi, akakupatia barua na siyo kutuma barua pepe nitakuruhusu,” amesema Mrema huku akibonyeza bonyeza simu yake ya mkononi.

Kuingia ndani ya eneo la Grumeti Singita, lazima upate kibali kutoka Ofisi ya Meneja wa Pori la Akiba la Ikorongo. Hata hao maafisa wa Grumeti hawakuwa tayari kumpokea mwandishi bila kupata kibali kutoka ofisi ya meneja huyo.

Hata baada ya kuombwa, kwamba mwandishi hakuwa anahitaji mahojiano isipokuwa kupata baadhi ya picha ndani ya eneo alimokuwa Faru John, bado aliendelea kushikilia msimamo wake, kwamba kwa mujibu wa maelekezo hawezi kuruhusu. Haikufahamika mara moja kama maelekezo aliyonayo bila kutaja ni kutoka ngazi ipi ya uongozi, hakuna mwandishi anayeruhusiwa kuingia Grumeti kwa sasa.

Baba yake Faru John

Uzao wa Faru John unaonekana kama una laana. Baba yake Faru John alipotea katika mazingira ya kutatanisha mwaka 1992. Haikuwahi kuripotiwa kama alikufa, miaka 23 baadaye sasa. Madhila kama hayo yanakikuta kizazi chake, mpaka imefikia hatua ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kudai kaburi, vipimo vya vinasaba na mambo mengine mengi kumhusu Faru John.

Akizungumza na JAMHURI, mmoja wa watumishi katika eneo hilo, ambaye hakupenda kutajwa jina lake, anasema Faru John alipelekwa katika eneo hilo Desemba mwaka jana chini ya ulinzi mkali wa maofisa 54 na msafara wa magari 15.

Grumeti-Singita wazungumza

Akizungumza na JAMHURI, Mkurugenzi wa Grumeti Singita, Graham Ledger, amesema angeweza kuzungumzia suala hilo, lakini akatoa maelekezo msemaji wa kampuni hiyo azungumze.

JAMHURI ilimtafuta Msemaji wa kampuni hiyo, Doris Parsons, kama ilivyoelekezwa na Mkurugenzi Mtendaji. Parsons amesema kampuni ya Grumeti Singita inaendelea kusubiri kusikia matokeo ya jopo la uchunguzi wa sakata la Faru John, litakapomaliza kazi yake.

“Sisi hapa hatuna jambo ambalo tunaweza kusema, maana tukisema chochote tunaweza kuathiri uchuguzi unaoendelea…tunasubiri uchunguzi ukamilike na ripoti iwe wazi,” amesema Parsons.

Profesa Maghembe azungumza

Akizungumza na JAMHURI, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe, amesema kumekuwa na mazingira ambayo yanazunguka suala la Faru John, na kwamba watu wote wenye chuki zao na Wizara ya Maliasili na Utalii wameona hapa kwenye suala la faru ndiyo sehemu ya kupumulia.

Prof. Maghembe amesema Faru John alizaliwa 1978 na ilipofika 1990, akawa ndiye ‘mtemi’ pale Ngorongoro Kreta, japo walikuwapo faru wengine ambao walikuwa wanagombania majike na Faru John. Jinsi walivyokuwa wakipambana kupata majike, amekuwa akipambana na faru wengine na kuwaua.

Anasema ilifikia hatua mpaka akamuua faru mdogo mwenye miaka 4. Hata baada ya kusababisha hivyo vifo viwili bado aliendelea kuwa mbabe tu.

“Hata kama angepelekwa Mkomazi, bado tatizo la ubabe lingeendelea tu… hata pembe zake ambazo tulizikabidhi, utaona pembe yake kubwa ilikuwa imekatwa juu na kuwa butu walau kupuguza madhara kwa faru wengine,” amesema Prof. Maghembe.

Anasema suala la Faru John kupelekwa Grumeti Singita, limekuwa ni suala la mchakato.

“Maombi ya Grumeti yaliletwa Mei, mchakato ukaendelea mpaka Desemba 8, mwaka jana”, anasema Prof. Maghembe anayeongeza kuwa wakati hayo yanafanyika hakuwa ameteuliwa kushika wadhifa wa Waziri wa Maliasili na Utalii.

“Mimi nimeteuliwa kuwa Waziri Desemba 23, mwaka jana… nikaapishwa Desemba 28, na ndiyo siku nilianza kazi rasmi. Nilifika wizarani mambo yote yakiwa yamekamilika… lakini utasikia watu wanasema Maghembe amekaa pale na majizi na wamemuuza Faru John,” amesema Prof. Maghembe.

Waziri Maghembe anakwenda mbali zaidi na kuwatuhumu baadhi ya wadau wa sekta utalii, kwamba wanawahonga waandishi ili kuhakikisha anachafuliwa aondoke. Amewataja baadhi ya washiriki wa mkakati huo kuwa ni Shirikisho la Utalii Tanzania na Chama cha Wenye Hoteli za Kitalii.

Uchunguzi kifo cha Faru John

Baada ya taarifa za kifo cha Faru John, iliagizwa uchunguzi wa kitabibu ufanyike, sampuli zilizochukuliwa na wataalamu kwa ajili ya uchunguzi ni maini, moyo, figo, utumbo, damu. Lakini matokeo ya uchunguzi huo waligundua kwamba minofu ya Faru John ilikuwa imekufa, lakini pia alikuwa na maambukizi mengi sana tumboni pamoja na minyoo.

“Huyu mnyama alikuwa na wanawake wengi kule Ngorongoro, lakini pale alipohamishiwa alikuwa na jike moja… Grumeti wanaye jike mmoja tu anaitwa Laikipia, baada ya dume liloitwa Limpopo kufa kutokana na kuchomwa pembe na tembo. Faru John hakupelekwa Grumeti kama anauzwa, isipokuwa ni mpango wa kuongeza idadi ya faru,” anasema Maghembe.

Hata hivyo, katika hali ya kushangaza wakati Faru John aliondolewa Ngorongoro kwa tuhuma za kuwa na nguvu nyingi na kuua faru wengine ndani ya hifadhi, Prof. Maghembe anasema Faru John alipofika Grumeti yakamfika. “Faru John [alipofika Grumeti) alikuwa anapigwa sana na Laikipia [faru jike aliyemkuta]. Amekuwa akipata kipigo kwa mwaka mzima,” amesema Prof. Maghembe.

Kaburi la Faru John

Alipoulizwa lilipo kaburi la Faru John, Prof. Maghembe amesema mnyama kama faru akifa anakuwa chakula cha fisi, mbwa mwitu.

“Ninaomba wakubwa wetu wajue kwamba, taratibu zote zilifuatwa na hata baada ya faru huyo kufa, tulifanya uchunguzi na nyara zote zilikusanywa kwa mujibu wa taratibu na sheria,” amesema Prof. Maghembe.

Wakati Prof. Magembe akisema hayo, maafisa eneo la Grumeti wanasema Faru John alifariki mwezi Agosti na pembe zake hazikuchuliwa hadi Desemba wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alivyocharuka.

“Sheria inataka pembe au kitaalamu tunaomba nyara kuchukuliwa ndani ya siku saba. Hata hivyo, nyara hizo hazikuchukuliwa hadi Desemba Mheshimiwa Majaliwa alipocharuka. Wanatafuta kila mbinu kujinasua, ila hili wanalo,” anasema mmoja wa watoa taarifa.

Hadi sasa kuna wingu zito juu ya uhalisia, na Waziri Mkuu Majaliwa ameunda Tume inayochunguza kupata ukweli juu ya pembe alizokabidhiwa alizozishtukia kuwa si za Faru John.
 
Back
Top Bottom