Faida za Muswada wa Bima ya Afya kwa Wananchi wa kawaida na masikini

Mathayo Fungo

JF-Expert Member
Nov 13, 2018
319
510
Naikumbuka vizuri sana siku ya tarehe 06/04/2021 ambapo Rais wangu mpendwa Mama Samia akiwaapisha viongozi mbalimbali pale Ikulu yetu, alisema kuna suala la Bima ya Afya kwa Wote, wataalam kaeni mlimalize hili, tuleteeni Serikalini tulijadili ili tuone kama linatekelezeka kwa kiwango gani.

Agizo hili lilinifanya nione kuwa Rais wetu anatamani kuona kila mwananchi anakuwa na Bima ya Afya ili kuwa na uhakika wa kupata huduma za matibabu wakati wowote.

Hili pekee linanifanya nami niungane na wananchi wazalendo ambao wamekuwa wazi kusema kuwa Mama anaupiga mwingi sana katika masuala yanayolenga ustawi wa mwananchi mmoja mmoja. Nasema haya kutokana na umuhimu wa suala la matibabu kwa wananchi ambalo limekuwa likiumiza wananchi wengi na wengine kujikuta wako kwenye umasikini mkubwa ili tu waweze kugharamia huduma hizo kwa mwanafamilia anayepatwa na maradhi.

Katika pita pita zangu, nilibahatika kuwa sehemu ya wadau walioshirikishwa kutoa maoni kuhusu muswada unaopendekezwa na kwa uwelewa wangu Bunge linasubiriwa kuupitisha Muswada huu.

Naandika haya sio kwa kutaka kusifia kundi la watu fulani kwani huduma za matibabu ni haki ya kila mwananchi kwani ugonjwa hauna tajiri wala maskini hivyo hakuna sababu ya propaganda katika suala nyeti kama hili ambalo Mama yetu mpendwa aliliona na kuagiza lifanyiwe kazi kwa haraka.

Nimepata msukumo wa kuandika haya kutokana na hoja dhaifu za baadhi ya watu ambao naweza kusema hawawatakii mema watanzania ambao kazi yao imekuwa ni kupinga Muswada huu kwa kuleta hoja za kudhoofisha na katika hili niseme hatutakubali hata kidogo.

Naamini kila mmoja anayesoma hapa atakubaliana nami kuwa suala la huduma za matibabu ni suala kubwa na nyeti na ni hitaji la msingi kwa kila mmoja, kila kukicha tunaona matangazo ya kuchangishana fedha za matibabu, watu wengi wanapoteza uhai na familia nyingi zinaingia kwenye umasikini mkubwa.

Ili kuondokana na haya hatuna budi kukubaliana na Muswada wa Bima ya Afya kwa wote ambao umekuja na majibu ya changamoto hizo. Kupitia muswada huu kwanza tutakuwa na usawa katika kupata huduma za matibabu lakini gharama za kuchangia ni ndogo mno ikilinganishwa na gharama zilizopo za huduma za matibabu kwa sasa.

Nilipopata fursa ya kutoa maoni, nilielezwa kuwa mchango pendekezwa kwa Kaya ya watu sita ni Shilingi 340,000 ambayo ukiigawa kwa mtu mmoja mmoja ni sawa na Shilingi 4,700 kwa mwezi ama kwa hesabu rahisi ni Shilingi 157 kwa siku.

Sasa hapa turudi kwenye hoja hasa za wale wanaopinga wakisema gharama ni kubwa, Je hii shilingi 157 kwa siku kuna Mwananchi yoyote anayeshindwa kuwa nayo? Mbona kwenye harusi ambayo inafanyika siku moja tunachangia fedha nyingi ambazo zinaweza kutuhudumia kwa mwaka mzima? Je wale wenzangu tunaokutana kwenye Viti virefu bia moja tu huoni kama gharama yake inaweza ikakusaidia kwa kiasi kikubwa kama kweli umedhamiria kuweka fedha kidogo kidogo ili ufanikishe kuwa na Bima ya afya?

Hapa unaweza ukaona ni kwa namna gani suala la afya hatujalipa kipaumbele sisi wananchi. Ni kweli wakati umefika tuache kudanganyana katika hoja au masuala ya msingi kama haya ni lazima tuseme ukweli na kuhamasishana kwenye masuala ya msingi. Hoja ya kutanguliza umasikini wa Watanzania haina mashiko na umaskini sio sifa hivyo ni wazi kuwa wananchi wanaweza kugharamia mchango pendekezwa.

Lakini pia tukumbuke kuwa Serikali bado ina mzigo mkubwa wa kuhakikisha inaongeza fedha katika eneo hilo ili kuwezesha upatikanaji wa huduma bora, lakini Serikali imekwenda mbali zaidi kwa kuweka utaratibu maalum kwa wenzetu ambao hawana uwezo wa kuchangia bima ya afya kwa wote ambao watapewa kadi za bima ya afya zitakazo gharamiwa na Serikali ili kuwawezesha kupata huduma za afya. Mnyonge mnyongeni lakini hakiyake mpeni, nani kama Mama Samia.

Naamini kila mwananchi atakapokuwa kwenye bima ya afya, hakika tutakuwa na Taifa la wananchi wenye afya njema na wanaoweza kushiriki vyema shughuli za kimaendeleo. Msisitizo wangu hapa ni tuache upotoshaji kwenye suala hili la msingi na linalolenga kuwakomboa wananchi wa hali zote.

Nimalize kwa kumpongeza Rais wangu na viongozi wote ambao mnafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha hali za Watanzania zinakuwa bora zaidi.

Mtanzania huru
 
Back
Top Bottom