Faida Za Kimwili (Afya) Na Kiroho (Imani) Za Kufunga

Makirita Amani

JF-Expert Member
Jun 6, 2012
1,915
3,407
Kufunga ni utaratibu ambao umekuwa unafanywa na watu mbalimbali kwa kuamua wao wenyewe au kutokana na taratibu za dini zao. Katika kipindi hiki cha kufunga, mtu anajinyima chakula kwa kipindi maalumu. Watu wengi ambao wamekuwa wanafunga wamekuwa wakifanya hivyo kwa sababu ndiyo utaratibu wa dini zao, ila hawajui kwa undani ni yapi hasa manufaa ya wao kufunga.
Kufunga kuna faida nyingi sana kwa mtu kimwili yaani afya yake na pia kiroho yaani imani yake. Kufunga ni utaratibu ambao unampa mtu faida nyingi kwa yeye kuchagua kujinyima chakula japo unaweza kukipata kama unavyotaka mwenyewe. Leo kwenye makala hii tutajadili faida hizi za kufunga, kama ulikuwa hujui uweze kujua na kama ulikuwa hujawahi kufunga basi uchague kufanya hivyo japo mara moja moja.

Faida za kimwili za kufunga.
Kufunga kuna faida nyingi sana za kiafya. Tafiti nyingi zimefanyika na zimeonesha manufaa makubwa sana ka afya za wale ambao wanafunga kwa kipindi fulani. Zifuatazo ni baadhi ya faida hizo.

1. Kuongeza uwezo wa mwili wa kujiponya wenyewe na kuongeza kinga ya mwili.
Wote tunajua ya kwamba unapokula chakula unaongeza nguvu mwilini, hiyo ni kweli, lakini ni upande mmoja. Kwa upande mwingine kula chakula kunatumia nguvu kubwa ya mwili wako. Unapokula chakula kinatakiwa kumeng’enywa na mfumo wa chakula wa mwili wako. Hili ni zoezi ambalo linahitaji nguvu kubwa kutoka kwenye mwili wako.
Pia vyakula tunavyokula huwa vinakuwa na sumu mbalimbali ambazo mwili inahitaji kuzivunja ili zisilete madhara kwenye mwili wako. Hii nayo inatumia nguvu ya mwili wako katika kuhakikisha sumu hizo zinaondolewa kwenye mwili.
Kwa mzigo huu mkubwa ambao mwili wako unakuwa nao, unakosa nguvu ya kuweza kupambana na vimelea vya magonjwa au kuweza kujitimu kwa majeraha mbalimbali yanayotokea ndani ya mwili. Kama mwili wakati wote una mzigo wa chakula ambao unahitaji kumeng’enywa au kuondolewa sumu hiki ndiyo kinakuwa kipaumbele cha kwanza na vingine vinasubiri.
Unapofunga hata mara chache unausaidia mwili kupeleka nguvu ambazo zinatumika kwenye kumeng’enya chakula kwenye kazi nyingine muhimu za mwili kama kuponyesha majeraha na kuongeza kinga ya kupambana na magonjwa.

2. Kufunga kunakuwezesha kupunguza uzito wa mwili.
Hapa ndipo wengi wanapopenda kusikia kwa sababu uzito wa mwili uliozidi ndiyo janga kubwa katika zama hizi. Hii ni hatari kubwa sana kwa sababu inakaribisha magonjwa sugu na hatari kama kisukari, shinikizo la juu la damu na hata kansa.
Uzito wa mwili uliozidi unatokana na mwili kupata chakula kingi hasa cha wanga kuliko unavyohitaji. Kwa sababu chakula ni kingi kuliko mahitaji, mwili unaamua kutunza chakula hiki kwa matumizi ya baadaye. Hivyo wanga unabadilishwa kuwa mafuta na kuhifadhiwa chini ya ngozi, huku ndio kunaleta kunenepa.
Unapofunga unaulazimisha mwili kutumia akina ya chakula ambayo imehifadhiwa kama mafuta chini ya ngozi ya mwili wako. Kwa njia hii mwili unapunguza uzito kwa sababu kile ambacho kilihifadhiwa sasa kinatumika.
Kufunga ni moja ya njia za kupunguza uzito kama kutafanywa sawasawa.

3. Kuwa na nguvu za ziada za ubunifu na kupunguza usingizi.
Kama tulivyoona kwenye pointi ya kwanza, unapokula nguvu kubwa ya mwili wako inapelekwa kwenye kumeng’enya chakula pamoja na kuondoa sumu. Na unapofunga maana yake nguvu ile inakuwepo kwenye mwili na inaweza kutumika kwa shughuli nyingine za mwili.
Unapofunga unaupa mwili wako nguvu ya kuweza kufanya shughuli mbalimbali. Na pia unaipa akili yako uwezo mkubwa wa ubunifu kwa sababu hakuna mahitaji makubwa ya virutubisho vya chakula kwenye shughuli nyingine za mwili. Akili yako inatumia sehemu kubwa ya virutubisho vya chakula vinachukuliwa na mwili baada ya chakula kumeng’enywa.
Pia kufunga kunapunguza uhitaji wa usingizi, nina uhakika umewahi kuona hili kwamba pale unapokula na kushiba ndiyo unasinzia, hata kama ni mchana. Hii inatokana na nguvu kubwa kutumika kwenye chakula ulichokula. Unapofunga nguvu hii haipelekwi tumboni bali inabaki kwenye mwili wako hasa ubongo na hivyo kuwa vizuri.
Kufunga kunaongeza ubunifu kwa wale wanaofanya kazi zinazotumia akili kama uandishi, usanii, na kazi nyingine za kitaalamu.

Faida za kiroho za kufunga.
Kufunga siyo tu kuna manufaa kwenye afya yako, bali pia kuna manufaa makubwa kwenye imani yako. Kufunga ni zoezi moja ambalo linaweza kuimarisha imani yako kwa kiasi kikubwa sana. Kwa kufunga unaweza kuona ni jinsi gani unakua kiimani na kuweza kukabiliana na changamoto zako za kimaisha. Zifuatazo ni faida za kiimani za kufunga.

1. Kujijengea nidhamu binafsi na kudhibiti tamaa.
Hakuna kitu ambacho ni hatari kwa ukuaji wetu wa kiimani kama tamaa. Tamaa imekuwa na madhara makubwa kwenye maisha ya watu wengi. Unapofunga unajijengea uwezo wa kudhibiti tamaa yako hasa ya mwili. Kumbuka unapofunga unachagua kutokula chakula japo unaweza kukipata. Hii ni tofauti kabisa na yule ambaye anakosa kabisa chakula na kukaa na njaa. Ila wewe chakula unacho lakini unaamua kukaa na njaa. Hii inakusaidia kujidhibiti wewe mwenyewe na hivyo kuacha kufanya mambo kwa sababu tu unayaona au unatamani kufanya.
Kwa mfano unapofunga utatamani chakula, lakini kwa kuwa unajua umefunga hutakula chakula. Hii inakujengea nidhamu binafsi. nidhamu hii binafsi unaweza kuihamishia kwenye shughuli nyingine na ukaweza kupata matokeo makubwa. unapofanya kitu chochote cha tofauti kuna sauti zitakuambia uache kufanya hasa unapokutana na changamoto. Kwa kuwa na nidhamu binafsi utaweza kuendelea kufanya licha ya changamoto unazokutana nazo.

2. Kufunga kunatuwezesha kuthamini kile tulichonacho, hata kama ni kidogo.
Moja ya tabia za binadamu ni kutokutosheka. Mchukue mtu ambaye hajawahi kula mkate na ataufurahia sana mkate siku za mwanzoni, baada ya hapo anauzoea mkate na ataanza kukuambia hawezi kula mkate bila siagi. Mpe siagi na atafurahia sana mwanzoni, baada ya muda atakuambia mkate bila siagi na yai siyo mtamu.
Tuna tabia ya kuzoea kile ambacho tunacho kwa sasa na kutaka zaidi na zaidi. Ubaya wa tamaa za binadamu ni kwamba hazina kikomo. Lakini unapofunga unajidhibiti wewe mwenyewe. Unapokaa siku nzima bila ya kula, pale unapopata chakula hutachagua kama chakula hiki nakipenda au sikipendi, bali kipaumbele kinakuwa ni kupata chakula. Katika hali ya kawaida ni vigumu mtu kula viazi na kuvifurahia, kila siku. Lakini unapofunga viazi vinakuwa ni moja ya chakula utakachokifurahia sana.
Kufunga kunatuwezesha kuthamini kila kitu ambacho tayari tunacho kwenye maisha yetu. Na pia kunatufanya tuelewe kwamba kuna watu ambao wanakosa kile ambacho sisi tumezoea na kuona ni cha kawaida sana. Hii inatuimarisha zaidi kiimani.

3. Kufunga kunaimarisha maombi au tahajudi.
Kwa wale ambao wana utaratibu wa kufanya maombi kufunga kunawawezesha kutulia kwenye maombi na kuweka mawazo yao kwenye kile hasa wanachotaka kukamilisha kwenye maombi yao. Kama tulivyoona kwamba kushiba kunapoteza nguvu ya mwili, kufunga kunakufanya uwe na nguvu ya kuweza kufanya maombi muhimu kwako.
Pia wale ambao wanafanya tahajudi (meditation) kufunga kunawawezesha kudhibiti mawazo yao wakati wana tahajudi. Kwa sababu mwili hauna mzigo mwingine unaofanyia kazi ni rahisi kudhibiti mawazo yako na kuweza kufikiri kwa kina kile ambacho unataka kufikiri.
Kufunga pia kunakufanya uwe na shukrani, kitu ambacho ni muhimu kwenye ukuaji wa kiroho. Unapoweza kushukuru kwa kidogo unachopata unajiweka kwenye nafasi ya kupata kikubwa zaidi.

Hatua ya wewe kuchukua.
Jenga utaratibu wa kufunga kwenye maisha yako. siyo lazima ufunge kwa siku nyingi bali unaweza kuchagua angalau siku moja kwa wiki na ukafunga au kwa utaratibu mwingine ambao utaendana na maisha yako na mazingira yako pia. Muhimu ni wewe uwe na kipindi ambacho unachagua kutokula huku ukiendelea na shughuli zako za maisha kama kawaida ili uweze kupata faida za kiafya na kiimani.
Nakutakia kila la kheri katika mifungo yako utakayojijengea, uwe na afya bora na ukue zaidi kiimani.
TUPO PAMOJA.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
MUHIMU; Kila siku huwa naandika makala nzuri za kukuwezesha kuwa na maisha bora, yenye furaha na mafanikio makubwa. kuweza kusoma makala hizi za kila siku jiunge na KISIMA CHA MAARIFA . Tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz na utapata maelekezo ya kujiunga na kupata makala hizi. Karibu sana rafiki yangu.
 
Mungu akujaalie na akusimamie.
Umeeleza vizuri sana,na hata wana Science wakubwa Duniani wanaafiki hivyo.
Mungu atupe wepesi
 
Back
Top Bottom