Eti ni kweli nchi iko kwenye ‘auto pilot’? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Eti ni kweli nchi iko kwenye ‘auto pilot’?

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by mchakachuaji192, Feb 27, 2011.

 1. mchakachuaji192

  mchakachuaji192 JF-Expert Member

  #1
  Feb 27, 2011
  Joined: Oct 19, 2010
  Messages: 353
  Likes Received: 26
  Trophy Points: 45
  KATIKA siku za hivi karibuni kuna msemo umeshika kasi baina ya watu wa kada ya kati. Huo msemo ni kwamba nchi iko kwenye ‘auto pilot’.

  Huu ni msemo uliobuniwa na mwandishi nguli wa makala wa gazeti litokalo kila juma. Mwandishi huyu alimaanisha kwamba nchi inakwenda kama vile haina mtu anayeidhibiti huko inakoelekea.

  Kimsingi hoja ya mwandishi huyu ni swali la msingi ikiwa tuna visheni (maono) kama taifa hasa kama hakuna kiongozi anayetupeleka kufikia hayo maono ya kitaifa.

  Ukiangalia kwa makini matukio yanayotokeza, utajiuliza kama ina maono kuna juhudi za kweli zinafanyika kutufikisha katika maono hayo?

  Hivi ni kiongozi gani anayeiongoza nchi kwa sasa? Huyo au hao wanaoingoza wanaidhibiti kwa kiwango gani tunachoweza kusema nchi haikuwa kwenye auto pilot? Tutafakari ili kujua nini cha kufanya ili kama taifa tufike pale tunapopahitaji.

  Ni kweli kwamba moja ya malengo ya vyama vya siasa ni kukamata dola. Inawezekana ikawa hili ni lengo la kwanza la kila chama cha siasa. Lakini kukamata dola haipaswi kuwa ndio mwisho na mwanzo wa malengo ya kisiasa.

  Tunakamata dola ili iweje? Hapa ndiyo inawezekana CCM inaelekea wametufikisha mwisho. Na lengo lao lilikuwa ni kushinda walikokuwa wakiita kuwa kwa kishindo huku malengo mengine yakiwa yamepotea.

  Hiyo inadhihirisha kuwa kazi yao kubwa ndani ya chama imekuwa ni kupanga mikakati ya kushinda. Nilibahatika kumsikia mwandishi mkongwe, Jenerali Ulimwengu akisema, maono ya watu sasa yamekuwa finyu ni kuangalia uchaguzi mkuu. CCM baada ya uchaguzi mkuu, wanaangalia uchaguzi wa ndani ya chama. Hivyo wakati wote kila mmoja anaangalia uchaguzi unaofuata. Malengo na dira imekuwa ni kuangalia namna ya kuwabwaga wapinzani wa ndani na nje ya chama katika uchaguzi unaofuata.

  Bahati mbaya sana ni kwamba chaguzi zetu zimetawaliwa na fedha.

  Nimesikia kwamba hata hao walioko ndani ya chama wanaopinga malipo ya Dowans, hawafanyi hivyo kwa moyo mkunjufu kwamba wanalilia taifa na watu wao.

  Habari zinasema kwamba vigogo wa chama hicho wanaopinga malipo ya Dowans wanalia kwa hofu kwamba fedha za malipo hayo zinaweza kutumika katika kuamua rais wa 2015. Tumefika hapo.

  Mawazo yetu na mwelekeo wetu ni tufanye nini kushinda uchaguzi unaofuata. Fikiria fedha zilizotumika kuipa CCM ushindi. Sina hesabu ya fedha zilizotumika lakini kwa akili ya kawaida unajua si haba. Tumeona mabango, vipeperushi, misafara na hata takrima.

  Hivi vyote ni gharama. Fedha zile zingewekezwa kwenye maendeleo tungekuwa tumeboresha maisha ya watu wangapi? Kuna mtu aliniambia nitazame yale mabango mengi yaliyotapakaa kila kona. Akaniambia kuna jambo moja la msingi.

  Kwamba katika mabango yale yaliyokuwa na picha za Rais Jakaya Kikwete msisitizo ulikuwa kuchagua Kikwete na kuichagua CCM. Hayakuwa na ahadi au hayakutupa dira. Hatuna malengo thabiti.

  Hata ukiangalia yale mabango yaliyokuwa yameandikwa hari zaidi, nguzu zaidi na kasi zaidi hayakujitosheleza wala hayakubeba ahadi yenye mashiko. Hari zaidi ya kufanya nini? Nguvu zaidi za kufanya nini? Kasi zaidi kuelekea wapi?

  Kama ni kuongezeka kwa gharama za maisha kweli tumekwenda kwa kasi zaidi. Kama ni kufeli kwa wanafunzi wa kidato cha nne kweli tumeporomoka kwa ari zaidi na kama ni kupambana na mabomu kweli tumeona nguvu zaidi. Dira yetu, mwelekeo wetu na maono yetu ni yapi?

  Tumekuwa watu tulioamua kwamba tutavuka mto tukishaufikia. Tumekataa kuona kwamba mbele yetu kuna mto hivyo tutembee tukitafakari namna tutakavyouvuka pindi tukiufikia. Tumeamua kuwa taifa la dharura.

  Angalia mahangaiko ambayo sisi kama taifa tunayapitia. Tatizo la umeme ni kituko. Hata niliposikia Kamati ya bunge ya Nishati na Madini ikizungumzia mbinu za muda mfupi za kumaliza tatizo la umeme nilijisikia kucheka.

  Tatizo la umeme si tatizo la dharura. Matatizo hayo yalianza tangu miaka ya tisini nilishuhudia matatizo makubwa ya umeme. Kwa wale wenye umri mkubwa kuliko mimi huenda walishuhudia tatizo la umeme miaka mingi zaidi.

  Hili halipaswi kuwa tatizo linaloshughulikiwa kwa dharura miaka zaidi ya ishirini! Tulilifahamu tatizo hili , tulikuwa na fursa ya kuingia mikataba inayoeleweka na wawekezaji lakini tukapoteza fursa hiyo.

  Hatuna cha kujivunia ingawa tumekuwa na gesi ya songosongo. Umeme wa maji tuliambiwa unategemea mvua. Huu wa gesi tunasema nini? Tuna hazina ya makaa ya mawe. Pamoja na uwezo wa kuwalipa wawekezaji waliowekeza kwenye umeme lakini hatuna uwezo wa kuwekeza kwenye shirika letu la umeme.

  Tunafanya vituko na viroja. Tunalenga nini? Sarakasi zote tunazoziona sasa ni vita ambayo sina hakika kama ni ya kumpigania mwananchi. Tunashuhudia kamati za bunge zikijaribu kujigeuza serikali badala ya kudhibiti serikali zinajaribu kuwa watekelezaji.

  Yote haya ni ushahidi wa ombwe katika mfumo wetu wa uongozi na ndio maana watu sasa wanauliza; nchi iko kwenye auto pilot?

  Hata maafa ya Gongo la Mboto nayo yanatuonyesha namna ambavyo hatuna mbinu na mikakati ya kujihami wakati wa maafa. Usiku ule wa maafa nakumbuka nilikuwa nikiangalia luninga ili kujua kama tutajulishwa chochote.

  Nakumbuka niliona tangazo kwamba wananchi wameambiwa wakae sehemu za mabondeni! Hakuna maelezo yoyote na wala hakukuwepo msaada wa kuwapeleka huko “Mabondeni”. Hata hospitali zetu hazikuandaliwa kujua namna ya kupokea wagonjwa wakati wa maafa.

  Nimeelezwa na mwanaume mmoja aliyempeleka mke wake hospitali habari ya kusikitisha. Mke wake amekatika mkono, damu zinavuja. Mhudumu wa mapokezi anasisitiza lazima walipie kwanza fedha pale ya cheti ndipo huduma ziendelee.

  Baba yule kwa bahati alikuwa na shilingi elfu mbili mfukoni kwake. Simlaumu sana yule mhudumu. Hii ndio namna tulivyowaandaa watu wetu. Hawajui tofauti ya heri na shari. Kama taifa hatujawapa maono ya kujua wafanye nini pindi ikitokea katika hali fulani.

  Kwa mara nyingine tena tumepoteza uhai wa watu wasio na hatia kwa mlipuko wa mabomu na kuwapatia baadhi ya watu wetu vilema vya kudumu na wengine vilema vya muda. Tumeingia gharama kubwa ya mali. Lakini hakuna anayewajibika.

  Hii nayo inaweza kushindilia hoja ya wanaohoji ikiwa nchi ipo kwenye auto pilot? Mamlaka ya nchi yalichukua tahadhari gani baada ya milipuko ya awali? Nani anawajibika katika kuhakikisha usalama wetu? Kama yupo mwenye dhamana ya kulinda usalama wetu, alitekeleza wajibu wake?

  Nani anawajibika kwa matokeo mabovu ya kidato cha nne? Nani anawajibika kwa ukosefu wa umeme? Nani anawajibika matatizo ya elimu ya juu? Je, ni kweli tumepoteza mwelekeo?
  Source: Tanzania Daima
   
 2. BONGOLALA

  BONGOLALA JF-Expert Member

  #2
  Feb 27, 2011
  Joined: Sep 14, 2009
  Messages: 13,784
  Likes Received: 2,392
  Trophy Points: 280
  kufikiria 86% ya watanzania wataunganishiwaje umeme walau huu wa kubahatisha hilo halipo vichwani mwao kabisa!mtu ninayemuona walau ana malengo fulani ya utawala wake ni dk magufuli wengine wanatafuna kodi zetu tuu!
   
 3. The Analyst

  The Analyst JF-Expert Member

  #3
  Feb 27, 2011
  Joined: Feb 26, 2011
  Messages: 464
  Likes Received: 92
  Trophy Points: 45
  Auto-pilot inasaidia ndege au meli kwenda pasipo rubani katika mazingira fulani. Hili si jambo baya wala la hatari endapo linafanyika kwa kufuata taratibu muhimu za kurusha ndege au kuendesha meli kwa usalama. Nchi yetu ipo katika hali tofauti.
  Sisi rubani wetu ni Kimeo. Hana taaluma wala utashi wa kuendesha ndege vizuri isipokuwa anapenda au amelazimishwa kukalia kiti cha rubani. Kwa hapa nchini mambo yanaweza kuwa tofauti sana kama tutapata rubani mwingine mwenye uwezo na nia ya dhati ya kuendesha ndege kwa usalama. JK na wapambe wake wanachukulia vitu kirahisi tu na kuona kuwaudhi mafisadi wawili au watatu ni hatari zaidi kuliko kuwafanyia mema watanzania 45 milioni.
   
Loading...