Eti bado kuna ndoto ya maisha bora? | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Eti bado kuna ndoto ya maisha bora?

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Mzito Kabwela, Dec 14, 2009.

 1. Mzito Kabwela

  Mzito Kabwela JF-Expert Member

  #1
  Dec 14, 2009
  Joined: Nov 28, 2009
  Messages: 17,520
  Likes Received: 1,691
  Trophy Points: 280
  MNANIFANYA nitoe kicheko cha uchungu! Inawezekanaje mnaambiwa mnaletewa maisha bora wakati haya ya kawaida tu yanawashinda?

  Mnataka kukimbia kabla ya kutembea? Bongo ni vituko juu ya vituko na kero juu ya kero. Inawezekanaje haya yanatokea, lakini hakuna wa kushangaa mwanakwetu?

  Labda hao wenye posho mbili-mbili ndio wanaofaidi maisha bora. Maisha bora kwa baba yangu mwalimu mstaafu anayelipwa pensheni isiyotosha hata nauli?

  Kabla ya kutoa ahadi ya maisha bora si mhakikishe kwanza walau tuna hayo maisha ya kawaida? Kabla ya kusema kwamba mtaweka luninga kwenye mahospitali si walau mtuhakikishie kwanza kwamba tuna vidonge vya kutuliza maumivu? Bado mnashangaa ninachokishangaa?

  Enyi wana, nasikia siku hizi mnataka eti kubadili kaulimbiu! Mnasema maisha bora hayaji kama mvua. Toba! Mlipokuwa mnaimba beti na tungo anuwai kutuambia tukichagua chama nambari wahedi tutapata maisha bora kwani hamkujua haya?

  Maisha bora yatoke wapi na huu ufisadi uliotuzunguka kila kona? Mizaha itakuwa ipi zaidi ya hii ya kutukejeli kwamba maisha bora hayaji kama mvua?

  Kwani walimu wanaowadai mafao yao miaka nenda miaka rudi wanapaswa kufanya nini zaidi kuliko kushika chaki? Huko simo ila tunawakumbusha ahadi yenu ya maisha bora kwa kila mwanakaya. Mtajiju siku ya kampeni.

  Maisha bora wakati kuna kipindupindu tena jijini Dar es Salaam? Ikiwa hapo ilipo Ikulu watu wanaugua magonjwa hayo ya aibu itakuwaje kwenye mikoa ya pembezoni?

  Mnajidai hamfahamu ninalowaambia? Kwa taarifa yenu Dar es Salaam kuna kipindupindu. Kuna asiyejua kwamba ugonjwa huu ni ugonjwa wa kumeza kinyesi?

  Nazungumzia kinyesi cha mwanadamu, si kinyesi cha pusi au fisi. Mnashangaa nini hapo? Mbona tunataka maisha ya kawaida kabisa ya kunywa maji safi kabla ya kutuletea hayo maisha bora ya kunywa maji yaliyopoozwa kwenye jokofu? Mtashangaa sana, lakini huo ndo’ ukweli wenywe mwanakwetu.

  Hamna habari kwamba kuna watu hawana hakika ya kupata mlo kila siku? Huyu ukimpa ahadi ya chakula bora, utakuwa unamtusi mwanakwetu.
  Yeye unadhani anahitaji hicho kinachoitwa balansi dayati? Anahitaji chochote cha kufanya tumbo lisikutane na mgongo! Ubora ni maigizo na kejeli kwake. Huko simo ila ujumbe wa kweli ndo’ huo mwanakwetu.


  Si mmeona yale yaliyowakuta ndugu zetu wa pale Upareni? Mvua imeweza kuondoa vibanda vyao na uhai wao. Unadhani wangekuwa na haya maisha ya wastani wangekuwa wameonja mauti wakati huu?

  Hamkawii kusema eti ni kazi ya Mungu! Kama wataalam wapo ilikuwaje siku zote isijulikane kwamba maporomoko yanaweza kutokea maeneo yale? Unadhani wakazi wa maeneo hayo wanahitaji mahekalu kama ya kwenu huko Masaki, Mikocheni, Oysterbay na maeneo mengine ya Uzunguni?
  Wao wanahitaji tu vibanda salama ambavyo vitawakinga na jua, joto na baridi. Ukiwaletea hao habari za kuwaletea maisha bora ya kukaa kwenye nyumba za kisasa unawakejeli hawa. Msichokielewa ni kipi hapa enyi ndugu?

  Pamoja na hoja yenu kwamba maisha bora hayaji kama mvua, mbona kuna mengine yako ndani ya uwezo wenu? Sikiliza hawa jamaa wa Tandale kwa Tumbo wanavyolia.
  Wanasema kuanzia kituo cha basi hadi maeneo ya chama nambari wahedi hapo Tandale ukitembea, unatembea umeweka rehani roho yako!

  Wanasema wakabaji wanakwapua bila kujali muda, iwe mchana, iwe usiku hawana tabu. Hayo si maneno yangu, ni kilio cha wakazi wa maeneo hayo yote.

  Mnaonaje mkarekebisha maslahi ya askari wetu ili waweze kutulinda kwa ufasaha zaidi? Nazungumzia askari polisi, sizungumzii hawa askari wa kampuni binafsi maana kuna kampuni zimeajiri walinzi hadi unajiuliza kama wanaweza kulinda chochote. Askari anavaa ndala bado abakie askari? Hiyo si mada ya leo.

  Ila kabla ya hiyo ahadi ya maisha bora mnaonaje mkituhakikishia usalama wetu na mali zetu? Tunalielewa hili la ulinzi shirikishi, lakini mnaonaje mkapiga panga bajeti za kutumbua mkamwongezea kaka yangu Lau Masha senti kwenye bajeti yake ili askari wetu wawe na vifaa vya kutosha?

  Jambazi akimzidi polisi vifaa, mwadhani kuna atakayepona? Mimi simo ila fungueni macho muone. Ikibidi wale waliopokea posho mbili warudishe ili tupanue wigo wa bajeti ya vijana wa Said Mwema.

  Nasema tena simo katika haya yote. Najitoa mzima mzima miye. Haya ya wafugaji kupoteza mifugo yao na makazi yao bado hamyaoni?
  Mzee wa Loliondo anayetimuliwa kwenye makazi yake kwa kisingizio cha kulinda mazingira ana hamu ya kusikia santuri yenu ya maisha bora kwa kila Mtanzania?

  Nimesikia waziri anasema eti walikuwa Wakenya wale waliokuwa wanaishi mbugani! Labda hatujui historia na jiografia kwa pamoja. Mbona maelezo mengine yamefanana na utani?

  Wazee walioamua kuja hadi Dar es Salaam kwa malalamiko unaweza kuwatuliza kwa kuwaambia kuna maisha bora mbele ya safari? Labda kama unataka wakutandike kofi la kelbu!

  Wanasema hakuna msiba usio na mwenzake. Wakati wafugaji wakitimuliwa huko kwenye mapori ili wasifanye uharibifu kwa mahayawani, tunaambiwa ukame nao umekodolea macho hawa wafugaji wenzetu.

  Hawa ukiwasimulia habari ya maisha bora wakati wanauza ng’ombe mzima kwa bei ya kuku hapa jijini, si unawatania? Acheni mizaha enyi watu, tuwe rialistiki.

  Kampeni zijazo hatutaki mtujengee ghorofa hewani. Msituambie maisha bora wakati yale ya kawaida tu ni ndoto. Au mwadhani ikiwa ninyi mwala, kunywa na kusaza ndiyo wote wako hivyo?

  Mwadhani watu wote wana uwezo wa kunywa mvinyo kama ninyi? Mnazungumzia kujenga zahanati kila kata wakati waganga na wakunga hawapo?

  Kwani hamjui hata hizi zahanati zilizopo hazina dawa? Tuongeze majengo au tuimarishe zilizopo ili kweli mtu akienda awe amekwenda kutibiwa si kusubiri msiba?

  Mtashangaa sana, lakini ukweli ndiyo huo. Unapomwambia mama anayepelekwa kujifungua akiwa amebebwa kwenye chekecheke kwamba unamletea maisha bora, unataka kumpa wazo gani?
  Natafakari hadi nashindwa mtu wangu.
   
Loading...