EPA kimyaa! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

EPA kimyaa!

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by BAK, Nov 1, 2008.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Nov 1, 2008
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,609
  Likes Received: 82,182
  Trophy Points: 280
  Imetolewa mara ya mwisho: 01.11.2008 0010 EAT

  • EPA kimyaa!

  *Hakuna kesi ya mafisadi iliyofunguliwa
  *Mwanyika, Feleshi 'wazima' mawasiliano
  *Wasomi, wananchi waonesha kukunja nyuso

  Na Waandishi Wetu
  Majira

  SIKU moja baada ya Balozi wa Marekani nchini, Bw. Mark Green, kufanya mahojiano maalumu na gazeti hili na kumshauri Rais Jakaya Kikwete akunje uso katika kupambana na mafisadi, leo Arobaini ya waliokwapua fedha kutoka akaunti ya EPA imefika, huku uchunguzi wa gazeti hili ukibaini kuwa hakuna dalili za kuwapo kesi yoyote iliyokwishafunguliwa.

  Juhudi za Majira kuwapata wahusika hadi jana jioni ziligonga ukuta baada ya simu za viongozi wote wakuu wenye dhamana na suala hilo kutokuwa hewani.

  Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa Kamati iliyoundwa na Rais, Bw. Johnson Mwanyika hakupatikana bungeni Dodoma ambako Bunge linaendelea na hata alipotafutwa kupitia simu yake ya kiganjani iliendelea kutokuwa hewani kwa siku kadhaa hata jana.

  Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Bw. Eliezer Feleshi ambaye kisheria ndiye ana wajibu wa kuyapitia majalada ya kesi kubwa za jinai kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Mashitaka ya Jinai (CPA) na pia Sheria ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (PCCA) naye simu zake zote mbili vivyo hivyo hazikuwa hewani.

  Ukimya wa watendaji hao wakuu umeongeza wasiwasi na hata kulifanya agizo la Rais alilolitoa bungeni Dodoma alipohutubia Bunge Agosti 21 mwaka huu, kukwama.

  Akihutubia Bunge, Rais alitoa agizo kwamba "...Tumekubaliana kwamba itakapofika tarehe 31 Oktoba, 2008 mwisho, ambaye hakulipa mpaka tarehe mosi Novemba, 2008 awe amefikishwa mahakamani ili mahakama itusaidie kupata fedha za watu.

  "...Hatuwezi kutumia fedha nyingine kwa ajili hiyo. Kwa hiyo, kuanzia tarehe 1 Novemba, 2008 mshike mshike. Tumewapa fursa ya kutosha, ambaye hakuitumia fursa hiyo basi."

  Kauli hiyo ya Rais ilidhamiria kuwa kufikia leo, waliokuwa hadi jana hawajarejesha fedha walizokwapua BoT wawe wamerejesha, lakini uchunguzi katika mahakama kadhaa uliofanywa na gazeti hili ulionesha kuwa si waendesha mashitaka wala mawakili wa Serikali, waliokuwa na taarifa za kufunguliwa kesi mpya dhidi ya mtuhumiwa yeyote wa EPA.

  Baadhi ya waendesha mashitaka kwenye Mahakama ya Kisutu waligusia hamu waliyonayo juu ya kesi dhidi ya mafisadi hao na kuahidi iwapo zitafikishwa hapo, watatumia ujuzi wao wote kwa maslahi ya Taifa kuhakikisha haki inatendeka na Watanzania wanaujua ukweli wote kuhusu EPA.

  Kutokana na ukimya huo wa wakuu wa taasisi hizo muhimu, wasomi na wananchi mbalimbali nao wameendelea kushikwa na jakamoyo wakishinikiza kuona hatua hizo zinachukuliwa.

  Kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mwandishi Wetu Peter Masangwa, anaripoti kuwa wasomi waandamizi wa chuo hicho walionya kuwa hata kama watuhumiwa walioshindwa kulipa fedha hizo watafikishwa mahakamani, waliolipa pia wachukuliwe hatua kama hizo, kwa sababu nao walitenda kosa la jinai la wizi.

  Profesa Mwesiga Baregu wa Kitivo cha Sanaa alionya: "Sioni mantiki kwamba warudishe hela kisha mambo yaishe. Hata waliorudisha nao wachukuliwe hatua kwa sababu kilichofanyika ni jinai. Watakaobainika wafilisiwe na wafungwe."

  Mhadhiri mwingine, Dkt. Benson Bana, hakutaka kulizungumzia sakata hilo kwa kina, hata hivyo alishauri kuwa hatua za kisheria zifuate mkondo wake na anasubiri uamuzi ili atoe maoni yake.

  Naye Hillary Komba anaripoti kuwa wananchi mbalimbali wamemtaka Rais Jakaya Kikwete kuwabana wahusika waliochota fedha hizo.

  Bw. Steven Kivume mkazi wa Tabata, alisema kuwaonea huruma ni kuwaingiza Watanzania katika matatizo makubwa kwa kuwa nchi ni masikini na haina fedha za kutosha, lakini watu wachache wanachota fedha bila kuogopa.

  Alishangaa kuona hadi jana hakukuwa na taarifa zozote za kurejeshwa fedha hizo wala kufikishwa mahakamani.

  Kwa upande wake, Bibi Bahati Makusanya, mkazi wa Mtoni kwa Azizi Ali, alisema uchotaji wa fedha zinazotakiwa kutumika katika matumizi ya nchi unasababisha nchi kushindwa kufikia malengo ya kuboresha uchumi wa nchi.

  "Fedha hizo zilizochotwa zimetangazwa kuwa zikirudishwa zitaelekezwa katika kutoa ruzuku kwa wakulima, hivyo Serikali lazima ihakikishe kuwa zote zimerudishwa na ambao hawakurudisha hadi siku ya mwisho ya kurejesha wachukuliwe hatua kali," alisema.

  Msomaji mwingine wa gazeti hili, Bw. Hassan Juma, wa Manzese, alionya kuwa wananchi wamechoka kufanyiwa usanii, kuna nafasi ya kurudisha imani kwa Serikali, iwapo itahakikisha kwamba haipindishi jambo hilo kwa lengo la kulindana katika uongozi.

  Alisema fedha zote zitangazwe kama zimerudishwa na waliokataa watangazwe hadharani, ili kutoa fundisho kwa wengine wasidiriki kutumia mafasi zao vibaya.
   
Loading...