Shahidi wa pili Ronald Manongi (49), katika kesi ya wizi wa mabilioni ya fedha za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), inayowakabili watuhumiwa Farjala Hussein na Rajab Maranda amedai kuwa BoT ilimwondoa shaka juu ya akaunti iliyofunguliwa na washitakiwa.
Manongi ambaye alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Utendaji na Huduma za Benki katika Benki ya Umoja wa Afrika (UBA), alidai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana, kuwa wakati akiwa ofisa katika benki hiyo, wakurugenzi wa Kiloloma and Brothers, walifungua akaunti Agosti 31, 2005 namba 0101305008 na aliitilia shaka baada ya kuona imeingiziwa na BoT fedha ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 1.8.
Mbele ya jopo la mahakimu wakazi chini ya Crypiana William ambaye ni Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Kazi, shahidi huyo alidai kuwa baada ya kuona akaunti hiyo imepata kiasi hicho cha fedha, alimwandikia Naibu Gavana wa BoT, barua iliyoelezea shaka yake kuhusu akaunti hiyo na kuituma kwa Kurugenzi ya Usimamizi wa Mabenki katika ofisi za BoT.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, BoT ilimwandikia barua ya kumjibu ikiwa imeandikwa na Naibu Gavana Juma Reli, ambaye akimtaka aondoe shaka juu ya kampuni hiyo, kwa sababu BoT imeridhia akaunti hiyo kupata fedha hizo.
Baada ya kuandikiwa barua hiyo na BoT, shahidi huyo alidai kuwa aliwaandikia barua wamiliki wa akaunti hiyo, ambao ni washitakiwa katika kesi hiyo, akiwataka wamweleze zaidi kuhusu akaunti hiyo na kudai kuwa Septemba 26, 2005 alipokea barua kutoka kwa mmoja wa wamiliki wa akaunti hiyo, Maranda, aliyemweleza kwamba wana kibali cha kulipwa deni na BoT kwa niaba ya kampuni ya B.C. Cars Export na kwamba kazi ya kukusanya madeni kwa niaba ya kampuni za nje ni biashara yao mpya. Aliongeza kuwa Maranda alimwandikia kwamba kampuni yao ya Kiloloma and Brothers, ina kibali maalumu cha kutumia kiasi cha fedha ambazo zimelipwa na BoT kupitia akaunti yao na kwamba hayo ni moja ya makubaliano yao na B.C. Cars Export.
Manongi alidai kuwa baada ya kupata barua hizo kutoka BoT na kwa wamiliki wa akaunti ya Kiloloma and Brothers, aliiruhusu akaunti hiyo kuendelea na alimwandikia mkuu wake wa kazi, akimweleza kuwa amepata maelezo ya kutosha BoT na kwa wamiliki wa akaunti hiyo.
Akieleza jinsi fedha hizo zilivyoanza kutolewa katika akaunti hiyo, shahidi alidai kuwa baada ya akaunti kuingiziwa fedha, wamiliki hao walianza kuzitoa kwa nyakati tofauti na kwa mara ya kwanza walitoa Sh milioni 30. Shahidi alidai kuwa Septemba 5, 2005 wamiliki hao walichukua tena Sh milioni 150 na Septemba 13, mwaka huo walitoa Sh milioni 100 wakitumia hundi namba 062352.
Alidai kuwa Septemba 15, mwaka huo walitoa Sh milioni 300 kwa hundi namba 062354. Na kwa hundi namba 062355 walitoa Sh milioni 100. Alidai kuwa walitoa fedha tena Oktoba 7, 2005 kwa hundi namba 062356 zikiwa Sh milioni 20. Manongi alidai kuwa kwa mara ya kwanza kupitia akaunti hiyo Oktoba 19, mwaka huo walihamisha Sh milioni 100 kwenda nje ya nchi katika akaunti ya B. C.
Cars Export Uingereza. Pamoja na kutuma fedha hizo walichukua Sh milioni 100 kwa hundi namba 062357. Oktoba 21, mwaka huo, shahidi alidai kuwa walichukua Sh milioni 45 kwa hundi namba 062358 na baada ya kuchukua fedha hizo, Oktoba 24 walihamishia Sh milioni 308.7 katika akaunti ya B. C. Cars Export.
Baada ya kuhamisha fedha hizo wamiliki hao siku hiyohiyo walinunua dola 10,000 za Marekani kwa Sh milioni 11.5 kutoka UBA, wakiwa na lengo la kubadili fedha hizo kutoka kwenye shilingi kwenda dola. Alidai kuwa Novemba 6, mwaka huo kwa kutumia hundi namba 062360 walichukua Sh milioni 5.2. Shahidi aliiambia Mahakama kuwa baada ya hapo wamiliki hao hawakufanya malipo tena bali Novemba 8, 2006 walihamisha Sh 41,000 kwenda katika akaunti yao ya dola namba 0101305019.
Aliongeza kuwa tangu BoT ilipoingiza fedha katika akaunti hiyo, hakuna fedha yoyote iliyoingia zaidi ya kutolewa na kwamba mpaka sasa akaunti hiyo imebakiwa na Sh 115,000. Shahidi alidai kuwa fedha zilizolipwa nje ni Sh milioni 714.7. Baada ya kumaliza kutoa ushahidi upande wa utetezi uliokuwa na Wakili Majura Magafu uliomba upewe muda wa kupitia hundi zote zilizotumika mahakamani ili uweze kuuliza maswali kwa shahidi. Kesi hiyo ya wizi wa zaidi ya Sh bilioni moja iliahirishwa hadi leo itakapoendelea kusikilizwa.