Emmanuel Marangakis as Attorney of Anastasios Anagnostou Vs The Administrator General, Civil Case No. 1 of 2011

Apr 26, 2022
64
100
Kesi ambayo Mahakama Kuu ya Tanzania iliamua kwamba Raia wa Kigeni wanaweza kumiliki ardhi kwa njia ya kurithi (where High Court of Tanzania ruled that non-citizen heirs could own land by way of inheritance).

Imeandaliwa na Kuletwa kwako nami, Zakaria - Advocate candidate.

Utangulizi: Hii kesi inahusu nini? Hoja kuu kwenye hii kesi ilikuwa ni, “Je, ni sahihi kisheria kurithisha haki ya kumiliki ardhi kwenda kwa mrithi ambaye sio Mtanzania?” Ukizingatia kuwa sheria ya wakati huo, ilikuwa inakataza mtu asiye mzawa kumiliki ardhi nchini Tanzania.

{i} Je, Mahakama iliamuaje?
{ii} Na kwa sasa utaratibu ukoje? Je, bado uamuzi huu unasimama kama ulivyo au sheria imebadilishwa? Twende pamoja!

MATERIAL FACTS (STORY)

-Tarehe 07-05-2006, binti wa Kitanzania (Diana Artemis Ranger) mwenye asili ya Ugiriki, alifariki bila kuacha wosia, katika hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam.

-Marehemu aliacha mali ikiwemo nyumba maeneo ya Upanga, Dar es Salaam.

-Marehemu aliacha warithi watatu. Kaka yake (Anastasios Anagnostou), mpwa (niece) wake (Iranis Anagnostou), mpwa (nephew) wake wa kiume (Georgious Anagnostou) ambao wote watatu hawakuwa Watanzania. (Mfano kaka alikuwa raia wa Ugiriki).

-Kaka wa marehemu, Anastasios Anagnostou, akamchagua na kumpa mamlaka kisheria (power of attorney) Emmanuel Marangakis ili awe mwakilishi wake kwenye hii kesi na kufanya kila kitu kwa niaba yake.

-Emmanuel Marangakis akaenda Mahakamani kuomba barua za usimamizi wa mirathi (letters of administration).

-Akawekewa pingamizi na wapwa wa marehemu, Iranis Anagnostou (niece) na Georgious Anagnostou (nephew).

-Tarehe 07/05/2007, Mahakama ikatoa uamuzi mdogo (ruling) na kumteua mpwa (nephew) wa marehemu Georgious Anagnostou kuwa wasimamizi wa Mirathi.

-Emmanuel Marangakis hakuridhika.
-Akakata rufaa Mahakama ya Rufani.

-Mahakama ya Rufani ikamuondoa mpwa wa marehemu Georgious Anagnostou, kwenye usimamizi wa mirathi na badala yake ikamteua Kabidhi Wasihi Mkuu (Administrator General) yule wa RITA.

-Wakati Rufaa ikiwa bado inaendelea (pending), Georgious Anagnostou aliyekuwa msimamizi wa mirathi mwanzo, akauza nyumba ya pili iliyokuwa Masaki, Dar es Salaam.

-Kupitia makubaliano yao wenyewe (Anastasios Anagnostou, Iranis Anagnostou na Georgious Anagnostou), Mahakama ikaamua kwamba, mali zilizobaki (nyumba ya Upanga Dar es Salaam) iende kwa Anastasios Anagnostou (kaka wa marehemu).

-Kupitia barua ya Georgious Anagnostou ya tarehe 04/05/2010, warithi pia walikubaliana kama ifuatavyo:

1. Georgiuos Anagnostou distributes the assets from the sale of the house in Masaki (belonging to the estate) and other minor assets already in his hands, together with bank balance in Tanzania, to all the heirs except Anastasios Anagnostou.

2. Anastasios Anagnostou atapata gari na nyumba iliyo Upanga na Emmanuel Marangakis ameondolewa kulipa kodi kwa matumizi ya nyumba na gari miaka minne iliyopita.

(Anastasios Anagnostou gets the house at Upanga (the suit property) and the car and Emmanuel Marangakis is relieved of having to pay rent for the use of the house and the car over the past four years.)

-Hata hivyo Kabidhi Wasii Mkuu akaona kwamba hawezi kumgawia nyumba Anastasios Anagnostou, kwa sababu Anastasios Anagnostou sio Mtanzania (non citizen), kwa hiyo hana haki ya kumiliki ardhi nchini Tanzania kwa mujibu wa Sheria ya Adhi ya Tanzania.

-Anastasios Anagnostou akawa anadai haki yake ya kurithi kama mnufaika wa mali ya dada yake na kulingana na makubaliano ya warithi wote.

-Anasema sio kazi ya Kabidhi Wasii Mkuu kama msimamizi wa mirathi kuchagua amgawie kipi na kipi asigawe.

-Yeye mwenyewe (Anastasios Anagnostou) ameshagawa nyumba kwa Emmanuel Marangakis, mwakilishi (attorney) wake kwenye hii kesi. Mwakilishi ana uhuru wa kuamua anavyoona inafaa. Haelewi kwa nini, Kabidhi Wasii Mkuu hataki kufata matakwa yake.

-Mgogoro ukaenda Mahakama Kuu.

-Ikafunguliwa Kesi Maalum kwa ajili ya kuiomba Mahakama Kuu itoe ufafanuzi na kujibu hoja zifuatazo:

1: Je, Kabidhi Wasii Mkuu anaweza kisheria kurithisha nyumba ya Upanga, Ilala, Dar es Salaam kwa Anastasios Anagnostou ambaye ni Raia wa Ugiriki na mrithi wa Marehemu dada yake (Diana Artemis Ranger)?

2: Je, Anastasios Anagnostou, anaweza kuuza mali zake kama alivyofanya, kwenda kwa Emmanuel Marangakis Mtanzania ambaye pia ni mwakikishi wake kwenye hii Kesi.

3: Je, njia (solution) pekee iliyopo ni kuuza mali na kugawa kilichopatikana kwa warithi?

UAMUZI WA MAHAKAMA KUU

-Kesi ilisikilizwa na kuamuliwa na mheshimwa Jaji, Dr. Fauz Twaib (ambaye amestaafu kwa sasa).

-Mahakama ikaanza kuchambua Sheria ya Ardhi.

-Kifungu cha 20 cha Sheria ya Ardhi (Land Act), kinakataza mtu asiye mzawa (non citizen) kumiliki Ardhi isipokuwa kwa lengo la uwekezaji tu (for investment purpose).

Nanukuu, “For avoidance of doubt, a non-citizen shall not be allocated or granted land unless it is for investment purposes under the Tanzania Investment Act”

-Kifungu hiki kinakataza “ugawaji (allocation)” na “uruhusu (granting)” wa ardhi kwa mtu asiye mzawa (non citizen). Hii maana yake ni nini?

-Kujua maana yake, tuangalie kwanza maana ya “ugawaji (allocation)” na “uruhusu (grant)” wa ardhi.

-Ukisoma sheria, kifungu cha ufafanuzi (definition section) kinatoa ufafanuzi ufuatao.

Neno “Transfer (uhamisho)” inamaanisha “passing (kuuza au kuhamisha) haki ya kumiliki ardhi, pango au rehani kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine, KWA KITENDO CHA WAHUSIKA WENYEWE NA SIO KWA KUPITIA SHERIA KUCHUKUA MKONDO WAKE, na inahusisha nyaraka ambayo kwayo uhamisho huo umefanyika.”

Kwa kiingereza “Transfer” means “the passing of a right of occupancy, a lease or a mortgage from one party to another BY ACT OF THE PARTIES AND NOT BY OPERATION OF LAW and includes the instrument by which such passing is effected.”

Kwa hiyo, kwenye Sheria ya Ardhi, kurithi wakati wa kifo SIO UHAMISHO, kwa sababu sheria haisemi ni kupitisha haki ya kumiliki ardhi, kwa kitendo cha mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine. (So, under the Land Act, a bequest upon death is not a transfer, because it is not a “passing of a right of occupancy by an act of one party to another.”)

Badala yake ni UPITISHO au UHAMISHO (TRANSMISSION), neno ambalo kifungu cha pili cha Sheria ya Ardhi kinalifafanua kuwa, UPITISHO (TRANSMISSION) ni kuhamisha (passing) haki ya kumiliki ardhi, pango au rehani KUTOKA KWA MTU MMOJA KWENDA KWA MWINGINE KUPITIA SHERIA KUCHUKUA MKONDO WAKE WAKATI WA KIFO au ufilisi au vinginevyo”

Nanukuu kwa kiingereza, “Rather, it is a transmission, a word which section 2 of the Land Act defines as “the passing of a right of occupancy, a lease or a mortgage FROM ONE PERSON TO ANOTHER BY OPERATION OF LAW ON DEATH or insolvency or otherwise” [emphasis mine].

ZINGATIA: Nimeamua kunukuu na kiingereza ili ukishindwa kuelewa kiswahili usome kwa kiingereza kama unakielewa. Maana baadhi ya maneno ni magumu sana kwa kiswahili, mathalani neno TRANSMISSION kwa kiswahili, ungelitafsri vipi hapa? Utasema MAAMBUKIZI? Mimi nimetumia upitisho au uhamisho kwa madhumuni ya hii kesi (as far as this case is concerned)

-Sasa, Turudi kwenye hoja ya msingi (central issue).

-Je, ni sahihi kisheria kurithisha haki ya kumiliki ardhi iliyopo kwenye mali ya marehemu kwenda kwa mrithi ambaye sio Mtanzania?

-Hii hoja inaibua maswali mengine ya msingi, kama vile, Je! Kijana au binti asiye Mtanzania aliyezaliwa na mtu (Mtanzania) ambaye anamiliki ardhi Tanzania, anaweza kurithi haki ya kumiliki ardhi ya mzazi wake, kwa jinsi zuio lilivyowekwa na kifungu cha 20(1) cha Sheria ya Ardhi?

“Whether a non-Tanzanian son or daughter of an owner of land in Tanzania can succeed his/her parent in the ownership of landed property in view of the restriction imposed by section 20 (1) of the Land Act.”

-Mahakama ikasema, mali za marehemu ni haki zinazoweza na zinatakiwa kurithiwa na warithi wa marehemu. Sasa je, ni sahihi kusema kwamba, haki hizi zinakoma baada ya mwenye nazo kufariki, kwa sababu tu kwamba warithi wake sio Watanzania?

-Sidhani kama itakuwa ni madhumuni ya kifungu hiki cha sheria (spirit of this provision), kusema kwamba mrithi hawezi kurithi ardhi isipokuwa kama ni Mtanzania.

-Kisheria, kama nilivyokwisha kufafanua (Jaji anasema), ni wazi, na naamua hivyo, kwamba kurithi mali ya marehemu baada ya kifo chake, sio ruhusa (grant) wala ugawaji (allocation) wa haki ya kumiliki ardhi.

-Hivyo basi, inawezekana urithi kufanyika kwa upande wa mtu asiye mzawa (non citizen)

-Pia, msimamo huu unaimarishwa na vifungu vya 68, 71 na 140 vya Sheria ya Usajili wa Ardhi (Land Registration Act), kuhusu kile kinachoitwa “Uhamisho wakati wa Kifo (Transmission on Death)”

-Hivi vifungu ndio huwa vinatumika wakati ardhi inapohamia kwa mrithi. (These are the applicable provisions where landed property devolves to an heir).

-Ukisoma kifungu cha 140 kinasema:

“Mmiliki wa mali au maslahi yoyote akifa, mwakilishi wake binafsi kisheria, kupitia maombi kwenda kwa msajili kwenye fomu maalum na kwa kumpelekea msajili nakala ya barua ya uthibitisho au uteuzi wa kusimamia mirathi ya mmiliki (marehemu), au ya kuteuliwa kwake chini ya sehemu ya nane ya Sheria ya Uthibitisho wa Wosia na Usimamizi wa Mirathi au chini ya Jedwali la nne la Sheria ya Mahakama za Mahakimu, (huyo mwakilishi - akifanya hivyo) atastahili kusajiliwa kama mmiliki kwenye ile nafasi ya marehemu.”

Kwa kiingereza, kifungu hiki kinasomeka hivi:

“On the death of the owner of any estate or interest, his legal personal representative, on application to the Registrar in the prescribed form and on delivering to him an office copy of the probate of the will or letters of administration to the estate of the owner, or of his appointment under Part VIII of the Probate and Administration of Estates Act or the Fourth Schedule to the Magistrates’ Courts Act shall be entitled to be registered as owner in the place of the deceased.”

-Uhamisho huo unatakiwa kuwekwa kumbukumbu (recorded) chini ya kifungu cha 71.

-Na hakuna popote kwenye Sheria ya Usajili wa Ardhi panapozuia uhamisho kisheria kwenda kwa mtu asiye Mtanzania (nowhere in the Land Registration Act, is there a restriction against a transmission by operation of law in terms of section 68 of the said Act, against a non-Tanzanian).

Mahakama Kuu ikasema, “the process of acquiring title by inheritance is not a grant or allocation of land. It cannot, therefore, be said to be restricted under section 20 (1) of the Land Act. It was plainly not the legislature’s intention to place any such restrictions.”

Kwamba, kitendo cha kupata umiliki wa ardhi kwa njia ya kurithi sio kuruhusiwa au kugawiwa ardhi. Hivyo haiwezekani kusema eti hicho kitu kimezuiwa chini ya kifungu cha 20(1) cha sheria ya Ardhi. Ni wazi kabisa haikuwa dhumuni la bunge kuweka zuio kama hilo.

Kuhitimisha, Mahakama ikatoa majibu yafuatayo kwa hoja zilizopelekwa mahakamani kuomba ufafanuzi;

1: Kwamba, Kabidhi Wasii Mkuu (Administrator General) anaweza kisheria kugawa nyumba iliyopo Upanga, Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam kwa Anastasios Anagnostou, ambaye ni raia wa Ugiriki na mrithi wa mirathi ya marehemu Diana Artemis Ranger, dada yake.

2: Kwamba, Anastasios Anagnostou (raia wa Ugiriki) anaweza kuuza haki zake kwenda kwa Emmanuel Marangakis (Mtanzania na mwakilishi wake halali kwenye hii kesi).

3: Sio sahihi kisheria kusema kwamba, solution (suluhu au njia) pekee iliyopo ni kuuza mali na kugawa kilichopatikana kwa warithi.

-Mahakama ikaagiza kwamba, Kabidhi Wasihi Mkuu amrithishe nyumba Anastasios Anagnostou raia wa Ugiriki kwa kufata taratibu zilizoainishwa na vifungu vya 68, 72 na 140 vya Sheria ya Usajili wa Ardhi.

-Hiyo ilikuwa tarehe 13/05/2011.

HIYO KESI IMEISHA.

Sasa swali linalofuata ni je, utaratibu bado uko vile vile au sheria imebadilishwa?

-Mwaka 2019 Serikali iliandaa muswada ikipendekeza kufanya marekebisho ya sheria, kuzuia wasimamizi wa mirathi wasigawe mirathi inayohusu ardhi kwa warithi ambao sio raia wa Tanzania.

-Kwa mujibu wa muswada huo, raia wa kigeni wangeweza tu kupewa kile kilichopatikana baada ya msimamizi wa mirathi kuuza ardhi.

-Muswada ulipoenda Bungeni na kujadiliwa, Serikali ikaghairi kufanya marekebisho ya sheria.

-Kwa hiyo warithi ambao sio Watanzania wanaruhusiwa kuendelea kurithi ardhi, sio lazima msimamizi wa mirathi aiuze na kugawa kilichopatikana.

-Mpaka leo napoandika makala hii, kifungu cha 20 cha Sheria ya Ardhi ya Tanzania kinakataza mtu asiye Mtanzania (foreigner) kumiliki ardhi nchini Tanzania isipokuwa tu kama ni kwa dhumuni la uwekezaji.

-Sheria ya Uwekezaji ya Tanzania (Tanzania Investment Act), inasema kwamba watu wasio wazawa (non citizens) wanaruhusiwa tu kumilimiki ardhi kama ni kwa ajili ya uwekezaji.

-Tofauti na hapo raia wa kigeni (non citizens) hawaruhusiwi kumiliki ardhi nchini Tanzania.

TARATIBU ZA MGENI KUMILIKI ARDHI NCHINI TANZANIA:

Je, ni utaratibu gani mtu ambaye sio raia wa Tanzania anatakiwa kuufata ili aweze kumiliki ardhi nchini? (Usikose makala itakayofuata)

-----MWISHO----

Angalizo: Position au maelezo haya ni kwa mujibu wa kesi na sheria zilizokuwa zinatumika mpaka siku ya kupost hili andiko. Hivyo unaposoma leo haya maelezo, soma kesi na sheria zilizopo sasa hivi, ili ujue utaratibu bado ni ule ule au la! Sheria zinarekebishwa na mpya zinatungwa kila siku.

Pia natoa angalizo, wale wazee wa kukopi machapisho ya watu na kuweka majina yenu. Ni kosa kisheria. Hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayejimilikisha andiko hili. Unaruhusiwa tu kushare lakini usibadili yaliyomo. Ni heri uanze kuandika ya kwako mpya.

Makala hii imeandaliwa na kuletwa kwako nami Zakaria (0754575246 WhatsApp).
 
-Muswada ulipoenda Bungeni na kujadiliwa, Serikali ikaghairi kufanya marekebisho ya sheria.
Naomba ushahidi wa hili. Naomba link ya taarifa rasmi ya kusema kwamba serikali ilighairi kuidhinisha mabadiliko yaliyokuwa yameandikwa kwenye Muswada wa Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali na. 8 wa 2019, ambamo kuna sheria ya kukataza mrithi asiye raia wa Tanzania kurithishwa ardhi ya Tanzania.

Maana kwenye tovuti ya Bunge wameandika kuwa muswada huo ulipitishwa na Bunge tarehe 28/01/2020 (screenshot nimeambatanisha).

WLMAA 8 of 2019 Passed in Parliament, ila kuna mtu JF anasema serikali ilighairi (k. 45 Probate).jpg
 
Back
Top Bottom