Elimu ya Afya ya Uzazi itasaidia kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi

Maguguma

Member
Mar 13, 2023
13
6
Prof. Andrea Barnabas Pembe ambaye ni Profesa wa Magonjwa ya Kina mama na Uzazi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) anaelezea madhara ya utoaji mimba usio salama.

Anasema hali hiyo ni pindi ujauzito unapotolewa katika njia zisizo salama na zisizo zingatia afya na utaalam wa mchakato wa zoezi hilo.

Madhara ya kiafya
Utoaji mimba unaweza kukusababishia hali mbaya kiafya kama vile kiwewe (trauma), kuwa mgumba, kuharibu Shingo ya Kizazi, Msongo wa Mawazo na hata kifo.

Pamoja na hivyo utoaji mimba kuna wakati unaweza kuwa na athari kulingana na historia ambayo inaweza kuendana na mila na imani ya watu au jamii husika.

Msongo wa mawazo hasa kwa wanawake huwa una athiri Wanawake wengi baada ya kutoa mimba.

Mwanamke anaweza kupoteza damu nyingi, kupata maambukizi makali ya bakteria yanayoweza kuathiri mwili ukashindwa kufanya kazi na hata kupoteza uhai wake.

Madhara mengine ni uwezekano wa kushindwa kupata mtoto kabisa kwa kuathiri mirija ya mfuko wa kizazi kuziba, pia aina ya utoaji mimba inaweza kuchangia ukuta wa mbele na nyuma wa mfuko wa kizazi kugandamana pamoja.

Hali ilivyokuwa miaka ya nyuma
Prof. Andrea Barnabas Pembe anaeleza miaka ya 1990 wapo waliokuwa wakijaribu kutoa mimba kwa kutumia spoku za baiskeli, vijiti vya miti, vipande vya mizizi n.k kwa kuingiza vifaa hivyo kwenye nyumba za mimba wakiamini itatoka, walipata madhara mengi.

Wengine walienda kwa wahudumu wa afya ambao hawakuwa na utaalam wa kutoa mimba wakaishia kupata madhara makubwa. Wengine walitumia chai yenye majani mengi, kemikali kama vile Jiki, dawa kama kolokwini.

Zamani pia kuna walioamini mjamzito akifanya mazoezi makali au kazi ngumu au kukimbia basi mimba itatoka na wapo ambao waliamini kupigwa sehemu ya tumbo basi mimba itatoka, hiyo ilikuwa ni kutokana na uelewa mdogo waliokuwa nao.

Elimu ya uzazi itolewe mapema
Profesa anasema ni vizuri elimu ikaanza kutolewa mapema zaidi kwa kuwa vijana wengi wanafanya vitendo vya kujamiiana wakiwa na umri mdogo, hata mabinti wanaovunja ungo zamani ilikuwa wanatokewa na hali hiyo wanapokuwa na umri wa miaka 15 na kuendelea lakini kwa sasa hadi miaka 11 hadi 12.

Wanatakiwa kupata elimu hiyo mapema ili kuwaanda kujua ambacho wanaweza kukutana nacho, kwa kuwa wanavunja ungo mapema wanatakiwa kufundishwa namna ya kudhibiti mihemko yao.

KAULI YA TAWLA
Mkurugenzi Mtendaji wa TAWLA, Tike Mwambipile anasema TAWLA inaunga mkono suala la elimu ya afya ya uzazi kwa jamii kwani itasaidia kupunguza mimba zizotarajiwa na hata magonjwa.

Anasema kuwa elimu ya afya ya uzazi na uwekezaji wake ni muhimu kwa jamii na hasa katika kuchagiza maendeleo.

"Elimu ya afya ya uzazi itasaidia kupunguza idadi ya watu wanaopata mimba zisizotarajiwa na kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na uzazi," anasema.

Maoni ya Wadau
Gazeti la JAMHURI, limemnukuu Mkurugenzi wa Miradi wa Shirika la Haki Zetu Tanzania lililopo Wilayani Ilemela Mkoani Mwanza, Gervas Evodius, akisema suala elimu sahihi ya afya uzazi ndani ya familia limekuwa ni changamoto kutokana na mila na tamaduni.

"Bado ni changamoto katika utoaji wa elimu ya afya uzazi jambo ambalo linachangia mimba zisizotarajiwa na kuchangia vifo vitokanavyo na uzazi," anasema.

Evodius anasema,kitu kinachosababisha wasichana wengi wasipewe elimu ni masuala ya mila zenye mtazamo hasi ambazo zimekuwepo awali katika jamii zetu kuhusiana na afya ya elimu ya uzazi.

Mimba za utotoni huchangia kuongezeka kwa changamoto za uzazi ikiwemo vifo
Mdau wa Afya ya Uzazi, Peter Mwaihola katika maoni aliyoyaandika anashauri kuwa Serikali ifanye maboresho ya Sheria ya Ndoa.

Anasema “Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa kwenye mjadala wa namna ya kudhibiti ndoa za utotoni ambazo bado zinashamiri katika baadhi ya maeneo hususani vijijini.

“Sheria ya ndoa ya 1971 ya Tanzania inatoa uhuru kwa msichana mwenye umri wa miaka 14 hadi 15 na mvulana mwenye miaka 18 kufunga ndoa, wakati huohuo kwa mujibu wa Katiba nchini Tanzania umri sahihi wa utu uzima ni miaka 18 na kuendelea.

“Ingawaje Serikali imefanya maboresho kadhaa ya Sheria ya Ndoa ya 1971 lakini bado Sheria hiyo haikufanyiwa maboresho kwenye umri wa msichana kuolewa jambo ambalo linakoleza mjadala wa wadau wa Sheria, Watetezi wa kijinsia na wanaharakati wa Haki za Binadamu.”

Ushuhuda
Mazingira ya utoaji mimba usio salama yanawakumba mabinti wengi wakiwemo wanafunzi wa vyuo na wanashiriki kutoa ujauzito katika njia ambazo sio salama.

Alizungumza na Clouds FM, shuhuda mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa anasema “Nilipata ujauzito nikiwa chuo, iliniumiza na kunishangaza, Mwanaume ambaye nilimbebea mimba sikuwa na mipango naye, nikaamua kuitoa kwa njia ambazo nazijua mwenyewe.

“Nilipata maumivu makali sana, nilidanganya kwa wazazi kuwa ninashida na wakanitumia Ths. 300,000.”

Mbali na maelezo hayo kuna huduma baada ya mimba kutolewa au kutoka yenyewe ambayo Mwanamke anatakiwa kuipata, Dr. Elias Kweyamba anaelezea:

“Huduma imekuwepo lakini haikuwa imetengenezewa muongozo mzuri, changamoto tunayopigana nayo ni kuongeza uelewa kwa jamii, inapotokea Mwanamke ameharibikiwa mimba anakuwa na hofu ya kusimangwa au kutengwa na hali hiyo inawafanya wanashindwa kwenda katika vituo vya afya.

Mikataba ya kimataifa kuhusu elimu ya afya ya uzazi
Tanzania ilikubali kusaini Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu – Mkataba wa Nyongeza wa Haki za Wanawake Barani Afrika maarufu kwa jina la MKATABA WA MAPUTO uliotungwa kuwa sehemu ya nyongeza ya Mkataba wa Haki za Binadamu na Watu wa Mwaka 1981.

IBARA YA 14 (2c) YA MKATABA WA MAPUTO
Kuna mengi ndani ya mkataba huo ambayo Tanzania imeyachukua na kuyatumia lakini kuna moja ambalo halijachukuliwa kwa ukubwa kama inavyotakiwa, suala hilo lipo katika IBARA YA 14 (2c).

Kipengele hicho kinahusu masuala ya afya ya uzazi hasa katika kutoa mwanya kwa Mwanamke kutolewa/kutoa mimba pale anapokabiliana na mazingira kadhaa ambayo yanaweza kuwa hatarishi kwake.

IBARA YA 14 YA MKATABA WA MAPUTO (2c) inatoa uwanja mpana wa kulinda haki ya afya ya uzazi kwa Wanawake, mfano wa baadhi ya ‘situation’ ambazo zimeruhusu mwanamke kutoa mimba mbali na suala la afya ya mwanamke:
~Unyanyasaji wa kingono
~Kufanya mapenzi na mtu wa ukoo
~Iwapo mimba inahatarisha akili au afya ya kiumbe cha tumboni
 
Back
Top Bottom