EDO KUMWEMBE: Apumzike kwa amani Iddy Mobby, kisha tujitafakari

Oldmantz

JF-Expert Member
Jan 24, 2023
428
996
mobby-pic.jpg

Aliondoka kwao akiwa kijana mwenye ndoto njema. Ndoto ya kutokuwa tapeli wala kibaka. Ndoto ya kucheza soka. Naamini aliondoka kwao akiwa hajaenda sana shule. Usishangae, hata wanasoka wa Ulaya huwa hawana muda wa kwenda shule. Wanaishi kwa kuzitumikia ndoto zao za uwanjani na wanafunga vitabu kwa muda.

Idd Mobby. Jana mwili wake uliwekwa katika sanduku tayari kwa kurudishwa kwao Shinyanga na leo atazikwa kwao. Kifo ni fumbo la ajabu. Jinsi maisha yalivyokwenda kasi. Juzi alikuwa anafanya mazoezi Mtibwa. Akajisikia vibaya akawahishwa Dodoma usiku wa manane. Akafariki. Leo anazikwa.

Kifo chake kimenipa pigo. Sikuwahi kumfahamu kwa karibu sana zaidi ya kumuona uwanjani akicheza. Beki shupavu kama alivyo. Ni miongoni mwa mabeki wa timu za kawaida za msimamo wa Ligi ambao walikuwa mashupavu na ambao walikuwa wamebakiza hatua moja kutua katika timu kubwa kama Simba, Yanga na Azam.

Kando yake marehemu Idd wapo wachezaji kama Abdallah Mfuko wa Kagera, Abdul Mangalo wa Singida Big Stars, Nurdin Chona wa Prisons na wengineo. Ni mashupavu hasa. Na wamewahi kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa.

Idd anakuwa mchezaji wa pili aliyeandikishwa katika timu za Ligi Kuu kufariki kwa msimu wa pili mfululizo. Msimu uliopita tulimpoteza Ally Mtoni Sonso. Msimu huu tumempoteza Idd. Kifo chake kimenitafakarisha mambo mengi.

Kimenitafakarisha namna ya ndoto ya vijana wanaotafuta maisha inavyoweza kukatika ghafla. Unapambana na maisha kujaribu kujikwamua au kuikwamua familia yako halafu ghafla kila kitu kinayeyuka ndani ya siku moja tu.

Hapa kuna mambo mawili. Jambo la kwanza huwa tunasema kwamba siku yako ya kufa ikifika basi utakwenda. Lakini kuna umuhimu wa kuangalia afya za wachezaji wetu. Ni kweli wachezaji wetu huwa wanapimwa afya kikamilifu? Sina uhakika sana.

Picha za msimu huu zinamuonyesha Idd akiwa ameshikilia jezi yake akitambulishwa kuwa mchezaji mpya wa Mtibwa akitokea Polisi Tanzania. Ni kweli alipimwa afya? Au tunaonyeshwa tu picha ya mchezaji akitambulishwa?

Tatizo hili lipo kwa wachezaji wa timu zetu zote. Katika zile mbio na sarakasi za kumsaka Aziz Ki, naamini rafiki yangu Injinia Hersi Said aliubeba mkataba wake na kwenda zake Ivory Coast kumnasa Aziz. Tuliona picha za Aziz akiwa na mkataba. Umewahi kumuona akipimwa afya?

Jioni ambayo Abdul Suleiman ‘Sopu’ aliwapiga Yanga hat-trick katika pambano la fainali kati ya Coastal Union na Yanga pale Arusha, Simba na Azam zikaenda kasi kuinasa saini yake. Inadaiwa usiku huo huo Sopu alisaini mkataba wa Azam. Hivi walikuwa na muda wa kumpima afya kabla ya kumpa mkataba?

Kuna mambo yanatafakarisha lakini huwa tunaishi kwa kumuachia Mungu tu. Nina uhakika kuna wachezaji wengi wa Ligi Kuu ambao kama likipitishwa fagio la uhakika la vipimo vya afya vya uhakika basi si ajabu watashauriwa wasicheze soka.

Rafiki yetu, Sergio Aguero alishauriwa aachane na mpira huku uwanjani akionekana kuwa fiti. Hii inatokana na vipimo vya mara kwa mara. Lakini ni huyu huyu Aguero ambaye alihama kutoka Independiente ya kwao Argentina, akaenda zake Atletico Madrid ya Hispania, akaenda zake Manchester City na kisha akarudi zake Barcelona.

Huku kote ambako alipita alikuwa anapimwa na kuonekana yuko fiti. Kutokana na kuzoea tabia ya kupimwa mara kwa mara ndio maana ilikuja kugundulika tatizo baadaye. Hii ina maana hata kama wachezaji wetu huwa wanapimwa lakini inabidi warudie kufanya hivyo mara nyingi.

Hatuwezi kujua Idd alikuwa ametembea na tatizo lake kwa muda gani. Inawezekana lilikuwa suala la muda tu kabla ya kumtokea kilichomtokea. Nadhani tuanze kuwa makini na suala la vipimo vya afya. Lakini hapo hapo kuna jambo la pili ambalo inabidi tumuachie Mungu tu. Kuna wachezaji waliwahi kuanguka uwanjani licha ya kwamba walipimwa afya zao na kuonekana wapo fiti kucheza soka. Haya ni maajaliwa ya Mwenyezi Mungu na kukubali tu kwamba siku yako ikifika hakuna ujanja.

Machi mwaka huu, Marehemu Marc-vivien Foe atatimiza miaka 20 tangu afariki uwanjani katika dimba la Gerland pale Ufaransa katika michuano ya Kombe la Mabara iliyokuwa inafanyika nchini humo. Huyu ni mchezaji ambaye alikuwa anapimwa afya kila uchao.

Mwenyezi Mungu aliamua tu kumchukua kwa shambulio la moyo. Kuna mambo ambayo yanazuilika na kuna mambo ambayo hayazuiliki. Miezi michache tu iliyopita Foe alikuwa amepimwa afya yake katika klabu ya Manchester City ambako alikuwa anacheza kwa mkopo akitokea klabu ya Lyon.

Marehemu Cheickh Tiote, staa wa zamani wa Ivory Coast naye alianguka uwanjani wakati akicheza soka la kulipwa nchini China. Ni miongoni mwa wachezaji wa Afrika ambao walicheza katika klabu kadhaa za Ulaya na barani Asia ambapo kuna vipimo vizuri lakini bado alianguka uwanjani.

Kitu cha msingi tunachofundishwa katika msiba wa Idd ni kwamba inabidi kwanza tuchukue tahadhari kama wanadamu na kuwaweka wachezaji wetu katika vipimo vizuri. Baada ya hapo tunaweza kumuachia Mungu.
Kwa mfano katika suala la Christian Erikssen wa Manchester United. Alianguka uwanjani wakati akiiwakilisha timu yake ya taifa katika michuano ya Euro. Wakati ule alikuwa anacheza Inter Milan na alikuwa amepitia vipimo vizuri vya afya.

Baadaye alipata shambulio la moyo akiwa uwanjani. Baada ya tukio lile madaktari walifanya kazi yao vema na wakamuwekea vifaa ambavyo vinamruhusu kucheza tena soka bila ya shaka. Hawajakurupuka kumruhusu kurudi uwanjani.

Ni hao hao ndio ambao walimkataza Aguero asirudi uwanjani, lakini ni hao hao ndio ambao wamemruhusu Erikssen kurudi uwanjani. Mungu anaweza kufanya lolote lakini kwa upande wao wamejaribu kutimiza wajibu. Tunapaswa kuanza kazi ya kutimiza wajibu kabla ya kugeukia pande nyingine.

Kitu kingine cha kusikitisha katika soka letu ni kwamba bado pia tuna wachezaji ambao hawataki kushughulika na madaktari wetu na badala yake wanaenda kwa waganga. Huwa inashangaza kidogo lakini ndio hali halisi.

Credit: Mwanaspoti
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom