Wazidi kuwakataa Warundi, Wanyarwanda EAC
Na Manyerere Jackton, Kibondo
WANANCHI wa kada mbalimbali wilayani Kibondo, wameungana na wenzao kadhaa katika mikoa ya Mara, Mwanza na Kagera, kupinga maombi ya nchi za Rwanda na Burundi kupewa uanachama katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Wakizungumza na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Diodorus Kamala, juzi, wananchi hao walipinga wazi wazo lolote la kuzikaribisha nchi hizo katika EAC.
Mkutano wa juzi ulifanyika katika ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zilizopo eneo la Mabamba, kilometa 20 hivi kutoka mjini Kibondo.
Mmoja wa wazungumzaji alikuwa ni Kapteni Saleh, ambaye alisema Rwanda na Burundi hazijatulia kisiasa, hivyo si vema zikaingizwa EAC.
Tukiziruhusu kujiunga, tutachukua matatizo yao, wapewe muda wajijenge kwanza, alisema.
Ofisa Uhamiaji, aliyejitambulisha kwa jina la Obado, alisema: Muda niliokaa na hawa watu nimeona bado sana, tusiwakaribishe sasa, tuna tofauti nao, sisi tumetawaliwa na Waingereza, wao wametaliwa na wakoloni wengine.
Alipinga wazo la kuwaingiza kwenye jumuiya ambako wanaweza kupewa hati za kusafiria na vibali vya kuishi nchini kwa miezi sita.
Kama sasa wanaingia kama wahamiaji haramu, itakuwaje baada ya kuwapa pasipoti? alihoji Obado.
Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kibondo, Twaha Ramadhan (SSP), aliungana na wazungumzaji wengine, kupinga Rwanda na Burundi kujiunga EAC.
Msimamo kama huo umetolewa na wananchi na viongozi kadhaa wa Shirati, Utegi, Musoma mjini (Mara), Isingiro, Mrongo, Rusumo, Kabanga (Kagera), na Mwanza mjini (Mwanza).