SEHEMU YA 03
“Dada mnakwenda? Dada vipi hapo?” aliuliza Godwin huku akimwangalia Winfrida na Happiness, hakutaka kuridhika, akawafuata na kuwashika mkono na kuwavutia kwake kama walivyokuwa wakifanya wapiga debe wengine.
Japokuwa alishikwa kibabe lakini Winfrida akachanganyikiwa, mapigo ya moyo wake yakapiga kwa nguvu, akahisi mwili wake ukipigwa na shoti ya umeme, mguso ule ulimchanganya na kujikuta akiachia tabasamu pana.
“Unakwenda dada? Ingia! Twende dada! Kuna siti za kumwaga, utakaa na ukichoka utalala,” alisema Godwin.
Hiyo ndiyo ilikuwa siku ya kwanza kuonana na Godwin. Moyo wake ulichanganyikiwa, aliporudi nyumbani, alijilaza kitandani na kuanza kumfikiria mwanaume huyo. Alionekana kuwa mvuta bangi, aliyepigwa na maisha lakini kwa Winfrida hakujali, alimpenda, kwa jinsi alivyokuwa, kwa muonekano wake uleule, moyo wake ukamkubali kwa asilimia mia moja.
Safari za kwenda Makumbusho hazikuisha, kila siku alikuwa akielekea huko hata kama hakuwa na kitu chochote kile. Alipofika, hakupanda kwenye daladala yoyote ile, alisimama pembeni na kumwangalia Godwin jinsi alivyokuwa akiita abiria, moyo wake ulimuonea huruma lakini hakuwa na jinsi.
“Mbona unapata tabu hivi! Hutakiwi kupata tabu hata kidogo,” alisema Winfrida huku akimwangalia mwanaume huyo.
Moyo wake ukafa na kuoza, penzi likaingia moyoni mwake kwa kasi kubwa. Darasani alipokuwa akisoma, hakusoma kwa raha, aligubikwa na mawazo tele na muda mwingine alikuwa akizungumza peke yake kama kichaa.
Happiness aliligundua hilo, alijaribu kumuuliza Winfrida kilichokuwa kikiendelea lakini msichana huyo hakuwa radhi kumwambia zaidi ya kumdanganya kwamba alikuwa na matatizo ya kifamilia.
“Kweli?”
“Ndiyo Happy! Siwezi kukuficha chochote kile,” alisema Winfrida huku akimwangalia rafiki yake usoni, ili kumdanganya zaidi, akamtolea tabasamu pana.
Happiness hakuhoji sana, alimuacha Winfrida ambaye aliendelea kuteseka kila siku moyoni mwake. Safari za kwenda Makumbusho ziliendelea huku lengo lake kila siku likiwa lilelile la kumuona mwanaume huyo ambaye tayari aliingia moyoni mwake, akavuta kiti na kutulia kabisa.