Wenyewe wahoji matumizi ya ruzuku, kususia Bunge la Katiba.
Wadai Mbowe amejilipa milioni 700 za chama chao kinyemela .
Washinikiza kuitishwa mkutano Baraza Kuu ili kuhoji viongozi,
BAADHI ya wajumbe wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wameshusha tuhuma kubwa dhidi ya uongozi wa juu wa chama hicho, huku Katibu Mkuu, Dk. Wilbroad Slaa, akiwapuuza na kuwaita wajinga wanaohangaikia matumbo yao badala ya kusoma na kuelewa Katiba ya chama chao.
Mbali na Slaa, Mbunge wa Ubungo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chadema, John Mnyika, alizungumzia suala hilo bungeni mjini Dodoma jana, akisema watu hao wanatumika ili kuvuruga juhudi za kisiasa za Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu msimamo wake dhidi ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
Kwa upande wao, wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, wajumbe hao takriban 78 kupitia wazungumzaji wao walisema uongozi wa kitaifa wa chama chao umefeli kiuongozi.
Kiongozi wa wajumbe hao, Athumani Balozi alisema uongozi wa Chadema baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2010 umewasaliti Watanzania kwa sababu ya kushabikia migogoro ndani ya chama hicho, na hasa dhidi ya wanachama wanaohoji harufu ya ufisadi wa fedha za ruzuku zilizoongezeka baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2010, kutoka shilingi milioni 56 hadi milioni 239, kwa mwezi.
"Matendo haya ya viongozi wetu ni unafiki wa kisiasa, kiasi cha kutumia mabilioni ya shilingi kwenda kumshambulia ama kummaliza kisiasa kiongozi mwenzao (Zitto Kabwe) na kuacha ujenzi wa chama ukiendelea kuporomoka," "Kwenye ujinga huu, hakuna wa kumlaumu zaidi ya Mwenyekiti wetu Freeman Mbowe na na Katibu Mkuu Dk. Wilbrod Slaa.
Hawa wanafaa sasa kuhukumiwa na Watanzania wanaopenda mabadiliko ya kweli kwa kurudisha nyuma jitihada za kuwakomboa na kukiimarisha chama na badala yake, wamekuwa wakitumia nguvu kubwa na rasilimali nyingi za chama kujiimarisha wao wenyewe," alidai.
Ubadhirifu wa fedha, mali za Chadema Kwa mujibu wa wajumbe hao, chama chao hadi sasa kimepokea jumla ya shilingi bilioni 10.038 kama ruzuku kutoka serikalini ili kijiendeshe, lakini cha kusikitisha kwa kipindi chote hicho na kiasi chote hicho cha pesa chama chao hakina hata jengo moja.
"Ofisi mikoani kote tunapanga kwenye fremu za maduka na hata pango la fremu hizo tunajilipia wenyewe kwa kuchangishana, Mbowe na Slaa wanatumia mabilioni haya kuruka kwa chopa huku chini tunaendelea kumenyeka kwa kigezo cha ukamanda. Huu ni utumiaji mbaya wa mali za chama," alisema Balozi.
Alieleza kusikitishwa na kitendo alichomhusisha nacho Mbowe akidai anajilipa madeni aliyokikopesha chama, kiasi cha zaidi ya milioni 700. "Sasa tunashindwa kuelewa deni hili ni deni gani lisiloisha? Je, deni hili alikikopesha chama kwa mkataba gani, aliusaini mbele ya nani huo mkataba wa mkopo? Taratibu za chama kukopa zipo wazi je, zilifuatwa? Haya ni matumizi mabaya ya fedha za umma," alidai.
Alieleza vile vile kusikitishwa na kitendo cha Mbowe kukiuzia chama magari aliyodai ni chakavu, kwa zaidi ya milioni 600, huku akijua ni chakavu na kwamba kabla ya kukiuzia chama alikuwa anakikodisha magari hayo.
"Masikitiko yetu ni kitendo cha Mbowe kununua Landcruiser V8 VX 2 kwa pesa za chama na kiaha kuja kukiuzia chama, lakini kama haitoshi mpaka leo hii, gari hizo zimesajiliwa kwa majina ya Mbowe Hotels.
Haya ni matumizi mabovu mno ya mali za umma na kwamba yampasa sasa ajitathmini kama anapaswa kuendelea kuwa kiongozi mtetezi wa wanyonge ama mnyonyaji wa wanyonge.
"Tunahuzunishwa na kitendo cha Dk. Slaa kutufanyia huduma ya kutuuzia ukombozi, haiwezekani kwa akili ya kawaida, Ukawa Katibu Mkuu unayelipwa zaidi ya milioni 130 kwa mwaka na chama halafu, makatibu na viongozi wako wa mikoani wanalipwa sifuri kwa mwaka.
Huu ni udalali na unafiki wa kisiasa," alidaiMadai mengine ya wajumbe hao ni uongozi kuvunja katiba na kanuni za chama chao kwa kususia Bunge la Katiba bila kuruhusiwa na vikao halali vya chama.
"Bunge la Katiba lilikuwa ni mazao ya juhudi zetu sisi wana-Chadema tuliopambana nchi nzima kuidai Katiba.
Chama chetu kilikuwa na fursa kubwa ya kutuwakilisha kwenye kuandika Katiba hiyo na kufanya marekebisho makubwa kwa kadri tulivyoazimia.
Lakini kususa Bunge la Katiba lililotokana na sheria mliyoshiriki kuitunga, ni kutufanya sisi sote tunaowakilishwa na viongozi hawa tuonekane ni majuha.
Madai mengine ni kutoitishwa kwa mkutano wa Baraza Kuu la Chadema kinyume cha Katiba yao inayoagiza Baraza hilo liitishwe kila baada ya miezi 12.
"Tunawaagiza viongozi wetu waitishe haraka mkutano wa Baraza Kuu ili pamoja na mambo mengine, wajieleze mbele ya wajumbe ni kwa nini tusiwachukulie hatua za kinidhamu kwa makosa ya ubadhirifu, kusaliti ndoto za Watanzania na kuhamasisha mgawanyiko na ubaguzi ndani ya chama," alisema.
Majibu ya Dk. Slaa Mwandishi wetu Chalila Kibuda kutoka jijini Dar es Salaam anaripoti kwamba, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.Wilbroad Slaa alizungumzia madai hayo akisema wajumbe hao wa Baraza Kuu la chama hicho ni wajinga na hawasomi Katiba ya Chadema.
Alisema kulipwa mishahara kwa mwaka milioni 130 hilo si si suala lake bali ni la Kamati Kuu ya Chadema iliyopitisha viwango hivyo vya mishahara.
Slaa alisema kuhusu kulipwa mishahara kwa makatibu wa wilaya walisitisha kutokana na kutafuta nyenzo cha chama ikiwemo magari katika kila kanda, pikipiki katika kila wilaya pamoja na kadi za uanachama.
Alisema wajumbe hao ni wajinga kutokana na kushindwa kusoma Katiba, kuhangaika na matumbo yao kwa ajili ya kuichafua Chadema kuelekea Uchaguzi Mkuu, 2015.
Alisema kuhusu kutoka nje ya Bunge ni suala la mchakato wa Katiba na si suala la chama na kwamba baadhi ya wajumbe hao ‘walishashughulikiwa' kutoka maeneo yao anashangaa kuona wanatoa taarifa hizo za kijinga kwa ajili ya masilahi ya matumbo yao.
"Watu hao ni wajinga na wanatakiwa kupuuzwa, nawaomba waandishi muwe mnabeba vitu vya msingi kuelekea Uchaguzi Mkuu kuna vitu vingi vya kijinga vitapatikana," alisema Dk. Slaa.