Kwako Dr. Slaa,
Nimekufahamu kwa takribani miaka 6. Ninafahamu baadhi ya tabia zako, unavyovipenda na usivyopenda. Wewe ni mtu mzima sana kwa sasa na kila ufanyacho kinachukuliwa kuwa kimefanywa na mtu mzima mwenye maamuzi na tena maamuzi thabiti. Baadhi ya sifa ulizonazo ni pamoja na
1. KIONGOZI: Wewe ni kiongozi na hakuna anayeweza kubisha hili. Umekuwa kiongozi tangu shule ya msingi, sekondari, vyuo, kanisani na kwenye taasisi za umma. Wakiitwa viongozi ambao ni "Multisectoral" basi wewe umo. Umeweza kuwaunganisha watu wa kada zote. Umeongoza siasa za nchi hii kwenye mfumo wa vyama vingi na umefanya mabadiliko makubwa. Umeweza kukifanya chadema kuitwa kweli chama cha upinzani. Umejenga na kutetea hoja zako bungeni na zilikuwa ni kwa maslahi ya taifa na siyo chama. Dr. Slaa wewe ni kiongozi na utabaki na kuendelea kuheshimiwa sana.'
2. MCHA MUNGU: Dr. hakuna aliye na shaka hata chembe kwamba wewe ni mcha Mungu. Umekulia muda mrefu sana kanisani ukimtumikia Mungu na wanadamu. Unajua nini maana ya UTU na nini maana ya UBINADAMU. Umekuwa ukiwatumikia wananchi wa Tanzania na sio wa chadema. Utakumbukwa kwa hilo na hakuna wa kukuondolea hiyo karama.
3. MSEMA KWELI: Wewe umekuwa msema kweli pale panapohitajika kusema kweli una umesimamia ukweli. Wewe siyo mtu wa kuyumbishwa useme hili wala lile. Ukweli ni ukweli kwako na hauwezi kubadilika ukawa uongo
4. MSIMAMO: Wewe ni mtu mwenye misimamo. Ukisema hapana kwa jambo la hapana basi ndiyo itakavyokuwa na hakuna wa kukubadilisha. msimamo wako ndio uliofanya chadema ikasisima na kufika hapo ilipo sasa.
5. MAAMUZI: Umekuwa ni mtu mwenye maamuzi na kuyasimamia ili kuona mwisho wake. Maamuzi yako huwa unatumia busara kubwa na yanaheshimiwa.
Yako mengi ambayo naweza kuandika kitabu lakini kwa leo naomba niishie hapo niandike lile linipasalo kuandika:
Dr. Slaa kwa sasa nchi imefikia kiwango kikubwa cha demokrasia ambayo inahitaji watu makini, wavumilivu, wenye misimamo, na watakaotetea demokrasia ya kweli. Katika maandiko matakatifu kuna maneno ya kusamehe na kusamehewa. Binadamu kwa hulka yao ni watu wa kukosea, wanaombana msamaha na shughuli zinaendelea. Najua wewe ni Mkristo na unajua nini maana ya kusamehe.
Sasa Dr. Slaa, ninavyokufahamu wewe kubadilisha misimamo yako ni vigumu sana ila kwa hili nitakaloandika hapa tafadhali nisome kwa umakini mkubwa:
Chadema na UKAWA vinapita kwenye wakati mgumu sana kisiasa. Kuna watu ambao jamii imewaamini na kuwapa dhamana na wewe ukiwa mmoja wako. Pamoja na kwamba "inasemekana" mlihitilafiana kwenye baadhi ya mambo, kuna jambo moja kubwa sana umefanya ambalo linadhihirisha sifa za kiongozi aliyekomaa.
Dr. wewe ni MVUMILIVU, MSTAHIMILIVU, MKOMAVU na USIYEKURUPUKA. Ulishawahi kusema wewe siyo mtu wa kukurupuka na kwa kawaida huwa ukiongea unahesabu kila neno litokalo kinywani mwako.
Kwa waraka huu Mhe. Dr Slaa, nakuomba kwa UKOMAVU wa kisiasa ulioonyesha tangu kuanza kwa mchakato wa wagombea wa urais na hasa UKAWA tafadhali sana USITETEREKE na naamini mpaka sasa maneno yako ya kuwa HUKURUPUKI yametimia. Umekuwa kimya bila kusema lolote. Ni vema ukawa kimya hivyo ila nishauri UENDELEE NA SHUGHULI ZA CHAMA. Likishapita hili la uchaguzi basi mtakaa tena kama chama kuangalia mlikojikwaa.
Dr. naweza kuwa naandikia mwenyewe lakini wako wengi wenye mawazo na mwono kama wa kwangu. Dr. ninakujua, ninakufahamu, tunaomba kama utaongea na press hakikisha unatoa neno la kujenga na siyo kubomoa.
Prof. Lipumba amefanya ndivyo sivyo. Siyo kwa wakati huu alitakiwa kufanya alivyofanya. It is costful kwa chama cha CUF na UKAWA. Dr. endelea kumeza hizo shubiri Mungu atakurimu.
Makene hakikisha mzee anapata huu waraka wangu.
Naomba kutoa hoja.