Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk.
Reginald Mengi, ameliomba Jeshi la
Polisi mkoani Tabora kuhakikisha
linawakamata na kuwafikisha
mahakamani wote waliohusika na
kukatwa kiwiko cha mkono mlemavu
wa ngozi (albino), Suzan Mungi (35)
na kutangaza dau la Sh. milioni 10
taslimu kwa mwananchi yeyote
atakayetoa taarifa zitakazosaidia
kukamatwa kwa watu hao.
Pia ameahidi kubeba jukumu la
kuwasomesha watoto wawili wa
Suzan, ambaye mumewe, Mapambo
Mashili, aliuawa kikatili kwa kupigwa
na kitu chenye ncha kali kifuani na
kichwani wakati akijaribu kumnusuru
mkewe (Suzan) asikatwe mkono wake
na watu hao katika tukio hilo.
Katika tukio hilo, watoto hao wawili
wameripotiwa pia kujeruhiwa na
kulazwa hospitali.
Dk. Mengi alisema hayo alipokutana
na viongozi wa Chama cha Albino
Tanzania (TAS), ofisini kwake, jijini
Dar es Salaam jana.
Alisema amefikia uamuzi huo
kutokana na kuguswa na uchungu wa
madhara yaliyowasibu albino na
wengine, ambao wamekuwa ama
wakikatwa viungo vya miili yao au
kuuawa kabisa kwa sababu ya
ulemavu wao.
Ingekuwaje wewe ni mwanaume na
Suzan ni mkeo, au ni mtoto wao, au
mdogo wako au ni mtu wako wa
karibu? Ungejisikiaje? Niwaachie
Watanzania jibu la hilo swali.
Tunachukua hatua gani kuwalinda
watu hawa. Mtu hachagui, hakuzaliwa
wala hakuomba kuwa mlemavu.
Mungu hafanyi makosa katika kazi
yake, alisema Dk. Mengi.
Aliongeza: Uongozi wa Jeshi la
Polisi uchukue hatua za haraka hata
ikibidi nyumba kwa nyumba
wachukue hatua ili liwe fundisho kwa
wengine na tuonyeshe kuwa
tunawajali hawa wenzetu. Kama kuna
mganga amehusika achukuliwe hatua.
Kama kuna mtu anatafuta madaraka
achukuliewe hatua kali. Naliomba
Jeshi la Polisi Tabora wahusika
washikwe, wafikishwe mahakamani ili
anayehusika aonje machungu.
Aliyetumwa kukata mkono, mganga na
kila aliyehusika wote
washughulikiwe.
Alisema yeye hana madaraka ya
kuchukua, hivyo atatoa mchango
wake kwa kumpa kiasi hicho cha
fedha mwananchi yeyote atakayetoa
taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa
wahusika na uhalifu huo, ikiwa ni
pamoja na kuwasomesha watoto hao.
Naye Katibu Mkuu wa TAS, Ziada
Nsemo, alimshukuru Dk. Mengi
akisema ni mtu wa kwanza nchini
kuguswa moyoni na kujitokeza
hadharani kukemea vitendo vya
ukatili vinavyofanywa dhidi ya albino.
CHANZO: NIPASHE