Huu ni unyanyasaji, unampa mtu karatasi ili isainiwe muda atakaoingia uwanjani na kutoka, sasa uhuru wa kuamua uko wapi?. Pia Gharama zilizotumika kusafirisha watu toka Tanzania Bara na Unguja, hii yote ni kuhujumu rasilimali za walipa kodi. Soma habari chini.
Sherehe za Mapinduzi zashangaza Z'bar
Salma Said na Exuper Kachenje
RAIS wa Zanzibar, Amaan Abeid Karume ameshangazwa na wananchi wa visiwa hivyo wanaoshabikia uhuru aliouita kuwa ni wa bandia, uliotolewa na Uingereza kwa Sultani mwaka 1963, badala ya kuenzi mapinduzi yaliyofanywa na wananchi mwaka 1964.
Akihutubia kilele cha sherehe za maadhimisho ya miaka 45 ya Mapinduzi ya Zanzibar, zilizofanyika kwenye Uwanja wa Gombani mjini Chake Chake, Pemba, Rais Karume aliwashutumu wananchi na baadhi ya wasomi kwa kushabikia uhuru huo.
"Kwa bahati mbaya mpaka sasa wapo baadhi ya watu wanaoamini kuwa uhuru uliotolewa na Uingereza ulikuwa kwa wananchi wa Zanzibar. Jambo hili si kweli," alisema Karume, ambaye baba yake, Abeid Karume aliongoza mapinduzi hayo yaliyouondoa utawala wa Kisultani.
"Waingereza walikuwa wanaihami Zanzibar kutokana na hofu za watawala wa Kisultani dhidi ya Wajerumani ambao wakati huo walikuwa wakitawala Tanganyika."
Rais Karume alisema kitu cha msingi kwa Wazanzibari ni kuendelea kujisifia utaifa mkubwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wenye wadau wawili ambao aliwataja kuwa ni Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.
Alisema malengo ya mapinduzi yametimizwa kwa kutekelezwa ilani ya Chama Cha Mapinduzi, kikiendeleza yale ya Afro Shirazi (ASP) kilicholeta ukombozi kwa Zanzibar katika kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania nchini.
Alisema pia malengo ya mapinduzi hayo ya Januari 12 mwaka 1964 yametimizwa kutokana na nchi kuondokana na ubaguzi, chuki na uhasama na kuendelea kuishi kwa umoja na mshikamano.
Wakati Uingereza ikiondoka mwaka 1963 utawala wa Zanzibar kwa Sultani wa Oman, ambaye kabla ya uhuru alitawala hadi ukanda wa pwani ya Bara. Hata hivyo, wananchi hawakuridhika na utawala huo na wakapanga kumuondoa sultani kwa kufanya mapinduzi yaliyotekelezwa Januari 12, 1964.
Hata hivyo, baadhi ya watu, wakiwemo wanasiasa na wasomi, wamekuwa wakipinga mapinduzi hayo wakidai kuwa, yaliua baadhi ya ndugu zao na wamediriki hata kuadhimisha sherehe zao za uhuru, badala ya Mapinduzi.
Jana, sherehe za Mapinduzi zilikosa msisimko uliozoeleka wakati zinapofanyika kisiwani Unguja.
Uwanja wa Gombani ulikuwa umepambwa vizuri, lakini mamia ya wananchi walijitokeza kusherehekea kwenye kilele cha maadhimisho hayo walionekana kushangilia kwa staili yenye kutia shaka.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi ndani ya Uwanja wa Gombani walisema kuwa, walilazimika kufika katika sherehe hizo kwa kuwa walipewa vipande vya karatasi vilivyotakiwa kusainiwa na kuhakikiwa wakati wanapotoka na kuingia uwanjani hapo ndiyo maana hawakutoka hadi mwisho.
Hilo lilithibitishwa na Waziri Kiongozi Shamsi Vuai Nahodha aliyesema katika hotuba yake kwamba, alikuwa haamini kinachotokea jinsi watu walivyojaa uwanjani hapo, akimaanisha kuwa hakutegemea umati mkubwa.
Kwenye Uwanja wa Ndege wa Karume ulio Chake Chake, zilionekakana ndege ndogo za kukodi zikitua na kuruka mithili ya daladala, wakati meli zote zilikuwa zimejaa wananchi kutoka Unguja na Tanzania Bara.
Maadhimisho hayo yamefanyika kisiwani Pemba wakati Uwanja wa Amaan ulio Unguja ukiwa katika matengenezo makubwa.
Akizungumzia muafaka wa CCM na Chama cha Wananchi (CUF), Rais Karume alitaka kuendelezwa kwa mazungumzo baina ya vyama hivyo vikuu visiwani baada ya kukwama kwa miezi kadhaa sasa.
Alisema hiyo ni moja ya changamoto kubwa zinazoikabili serikali yake kwa kuwa, ndizo zitaleta amani na utulivu wa nchi na akakiri kuwepo kwa tofauti kubwa za kimtizamo baina ya vyama vya siasa, ingawa alisema ni jambo la kawaida kwa vyama kutofautiana.
"Jambo la msingi na muhimu zaidi katika mazingira tunayoishi... ni utamaduni wa kuendelea kuzungumza kwa uwazi zaidi tofauti zetu ndani ya vikao rasmi na kuzitafutia ufumbuzi," alisema Karume.
Akizungumzia hali ya uchumi wa Zanzibar, Rais Karume alisema uchumi unaendelea kukua kwa kasi ya kuridhisha, akitaja kiwango kuwa kimefikia asilimia 6.5 kwa mwaka ingawa kiwango hicho kilikuwa chini ya matarajio ya awali ya asilimia 6.8.
"Nchi imebadilika katika kipindi kigumu cha mageuzi ya siasa, uchumi na maendeleo na sasa uchumi umekuwa kwa asilimia 6.5 ingawa kiwango hicho kilikuwa chini ya matarajio ya awali ya asilimia 6.8... lakini tumeweza kupiga hatua kubwa," alitamba Rais Karume.
Alisema ukuaji wa uchumi umesababisha kuongezeka kwa thamani ya pato la taifa kutoka Sh510.0 billioni mwaka 2006 hadi kufikia Sh588.4 billioni kwa mwaka 2007.
Hata hivyo alisema hali ya mfumko wa bei haukuwa mzuri katika mwaka 2007 na hivyo kusababisha kasi ya mfumko wa bei kwa bidhaa mbalimbali na kuongeza hali ngumu ya maisha kwa wanaanchi.
"Kasi ya mfumko wa bei ilibaki tarakimu mbili na kuwa asilimia 13.1 kutoka asilimia 11.4 mwaka 2006," alisema Rais Karume katika hotuba yake.
Alisema hali hiyo imewaongezea wananchi ukali wa maisha na kupanda kwa gharama za maisha katika visiwa vya Zanzibar na kuwa serikali inalitambua tatizo hilo na ipo mbioni kulitafutia ufumbuzi.
Alieleza mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa na serikali yake, akitaja sekta ya maji, elimu, afya, miundombinu ya mawasiliano na barabara pamoja na utawala bora unaotekelezwa kwa vitendo chini ya utawala wake.
Alisema maendeleo yaliofikiwa na Zanzibar ni makubwa katika kipindi cha miaka 45 na aliwataka wananchi kujivunia maendeleo hayo na kuachana na watu wenye kuyabeza ambao hawana macho ya kuyaona.
Rais Karume aliwaalika watu wa mataifa mbalimbali, kutembelea visiwa vya Zanzibar kujionea namna ya uhuru mpana wa wananchi katika kujiamulia mambo yao bila ya kuingiliwa na mtu au serikali.
Alisema kushamiri kwa demokrasia miongoni mwa wananchi ni dalili tosha ya kuwepo kwa utawala bora na kuwa, serikali itaendelea na mikakati yake kuhakikisha inaendelea kuheshimu misingi ya demokrasia na utawala bora.
Rais Karume aliuambia umati unaomsikiliza kwamba, kumekuwepo na mafanikio makubwa katika kuimarisha miundo mbinu katika sekta mbalimbali, ikiwemo barabara za mjini na vijijini katika visiwa vyote vya Unguja na Pemba.
Alisema ujenzi wa barabara hizo umesaidia kuboresha hali za maisha ya wananchi kuwa bora na kupunguza umasikini uliokuwa unawakabili.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa ngazi za juu, akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Kikwete, Makamu wa Rais, Dk Ali Mohammed Shein na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Wengine ni marais wastaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa.
Source:
Mwananchi Read News