OFISI ya Taifa ya Mashtaka imeshughulikia mashauri ya jinai 4,429

esther mashiker

JF-Expert Member
May 29, 2018
616
552
1075395


OFISI ya Taifa ya Mashtaka imeshughulikia mashauri ya jinai 4,429 yanayohusu uporaji na uuaji wanyamapori, dawa za kulevya, uhujumu uchumi, rushwa na mauaji nchini.

Akiwasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka ujao wa fedha bungeni jana, Waziri wa wizara hiyo, Dk Augustine Mahiga alisema mashauri hayo yalishughulikiwa tangu ilipoanzishwa Osi ya Taifa ya Mashtaka Februari 13, mwaka huu. Dk Mahiga alisema katika mashauri hayo yanayohusu uporaji na uuaji wanyamapori yalikuwa mashauri 1,293, ambapo mashauri 204 kati ya hayo yamehitimishwa na mengine yanaendelea katika hatua mbalimbali.

Alisema kesi za dawa za kulevya zilizoshughulikiwa katika mwaka huo ni 2,545 na kati ya hizo 756 zilihitimishwa. “Mashauri 591 ya uhujumu uchumi yalishughulikiwa na mashauri 113 kati ya hayo yalihimishwa,” alisema Dk Mahiga. Alisema katika kipindi hicho, jumla ya majalada 234 ya makosa ya rushwa yalipokewa kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ambapo kati ya hayo majadala 56 yaliandaliwa hati za mashitaka na kupatiwa vibali vya kushtaki.

Alisema majalada 94 yalirudishwa Takukuru kwa upelelezi zaidi, jalada moja lilifungwa na majalada 83 yanaendelea kufanyiwa kazi. Alisema katika kesi hizo, washtakiwa waliotiwa hatiani kutokana na makosa hayo, walipewa adhabu mbalimbali zikiwemo vifungo na faini za zaidi ya Sh bilioni 4.8 zililipwa mahakamani na mali zinazokadiriwa kuwa za Sh bilioni 39.64, zilitaishwa kwa amri ya Mahakama.

Alisema baadhi ya mali zilizotaishwa ni madini ya dhahabu na vito vyenye thamani ya Sh bilioni 32.7, mashine ya kupima ubora wa dhahabu yenye thamani ya Sh milioni 305, ng’ombe 2,469, malori manne na magari madogo manne.

“Mali nyingine ni vipande vya mbao 1,506, magunia ya mkaa 100, injini ya boti moja, mitumbwi miwili, nyumba moja, meno ya tembo manne, kemikali lita 260, pikipiki 11 na vilainishi vya injini lita 200. Mali hizo zitaondoshwa kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo,” alisema.

Alisema katika mwaka ujao wa fedha wa 2019/20, wizara hiyo imeweka mkakati wa kuendelea na ujenzi wa mahakama nchini kote zikiwemo Mahakama Kuu mbili zinazoendelea kujengwa katika mikoa ya Kigoma na Mara. “Pia wizara inategemea kuanza kujenga mahakama nyingine katika Mkoa wa Morogoro, Mwanza, Dodoma na Singida.

Pia Mahakama za Wilaya 32 na Mahakama za Mwanzo 20 nchini katika mwaka wa 2019/20. Katika kutekeleza majukumu hayo, wizara hiyo inaomba Bunge liidhinishe na kupitisha Sh bilioni 55.177 kwa ajili ya matumizi ya wizara na Sh bilioni 126.2 kwa ajili ya Mfuko wa Mahakama nchini.
 
Back
Top Bottom