Dossa Aziz katika wakati wake kukimbilia kuunda TANU

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,920
30,263
DOSSA AZIZ KATIKA WAKATI WAKE KUKIMBILIA KUUNDA TANU 1950

Tulikuwa tumekaa barazani kwa Dossa Aziz nyumbani kwake Mlandizi nyakati za asubuhi kama saa nne mimi, Ally Sykes na mama mmoja Mmarekani Mweusi mwandishi wa Washington Post.

Huyu mama alikuwa mgeni wa Ally Sykes.

Pembeni ya mabaki ya landrover mbele ya nyumba wa Dossa Aziz, Ally Sykes alikuwa ameegesha Mercedes Benz yake rangi ya bluu iliyokoza, yaani ‘’dark blue.’’

Dossa Aziz akanyoosha kidole chake cha shahada akaniambia, "Nimetembea Tanganyika nzima na Nyerere kwenye Land-rover hii."

Miaka mingi sana Ally Sykes na Dossa Aziz walikuwa hawajaonana.

Walikumbatiana kwa mapenzi makubwa mimi nikiwaangalia na kuvuta hisia watu hawa walikuwaje katika ujana wao wakati wanapigania uhuru wa Tanganyika.

Tofauti baina yao ilikuwa kubwa sana.

Wote walikuwa watoto kutoka familia kubwa mashuhuri na tajiri katika Dar es Salaam ya miaka ile na wote walikuwa wafadhili wakubwa wa TANU na harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika.

Dossa alikuwa amepigwa na ufukara.

Hayo hapo chini ndiyo niliyoelezwa na Dossa Aziz siku ile na akanifisha na kunikutanisha ndani ya mazungumzo na Sued Kagasheki kama alivyokuwa miaka ya 1950:

‘’Mwaka wa 1951 Kenyatta kwa mara nyingine aliitisha mkutano mwingine baina ya KAU na TAA mjini Arusha (mwaka wa 1950 Abdul Sykes alifanya mkutano wa siri na Kenyatta Nairobi).

Katika ujumbe alioutuma kwa TAA, Kenyatta alisisitiza kuwa uongozi wa chama cha TAA uende mkutanoni na silaha.

TAA iliwateua Abdulwahid, Dossa Aziz na Stephen Mhando kuhudhuria mkutano huo.

Abdulwahid alikuwa na bastola aliyopewa wakati wa vita na ofisa mmoja mzungu kama zawadi.

Ilitokea kuwa siku ya kuzaliwa ya Mzungu yule ilikuwa sawa na yake na kwa sababu yule Mzungu akampa bastola yake kwa ukumbusho.

Dossa Aziz alikuwa na bunduki iliyokuwa ikipiga risasi tano kwa mfululizo.

Haijulikani kama Mhando alikuwa na silaha.

Wajumbe wa TAA walisafiri kila mtu peke yake kupoteza lengo.

Dossa Aziz alikuwa wa kwanza kuondoka kuelekea Arusha kupitia Dodoma.

Siku zile kulikuwa hakuna barabara ya moja kwa moja kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha.

Wasafiri waliotaka kwenda Arusha ilibidi wasafiri wapitie Dodoma.
Dossa Aziz alifungasha ile bunduki yake ya risasi tano.

Mjini Dodoma, Dossa Aziz alipokelewa na Mwalimu Ali Juma Ponda, katibu wa TAA Central Province.

Baada ya kuelezwa na Dossa kuhusu ule mkutano wa TAA na KAU uliopangwa kufanyika Arusha, Ponda aliwaarifu Dossa Aziz kuwa kulikuwa na mapigano makali kati ya Mau Mau na vikosi vya Waingereza yaliyosababisha viongozi wa KAU kusakwa na kukamatwa.

Ponda alimfahamisha Dossa kuwa ingelikuwa vigumu katika hali kama hiyo kwa Kenyatta na ujumbe wake kuja Arusha.

Dossa Aziz aliamua kuvunja safari ya Arusha na kuelekea Mwanza kwa gari la moshi kukagua matawi ya TAA.

Mwanza, Dossa Aziz alipokewa na Dr Joseph Mutahangarwa, makamu wa rais wa TAA katika kanda ya ziwa.

Dr Mutahangarwa alikuwa Mwafrika wa kwanza kufuzu udaktari.

Baada ya kuelezwa kuhusu ule mkutano wa Arusha, Dr Mutahangarwa alimwonya Dossa kuhusu hatari ya mwenendo aliokuwa akichukua Abdulwahid kama katibu na kaimu rais wa TAA.

Dr Mutahangarwa alimweleza Dossa hatari ambazo TAA na uongozi wake ungezikabili pindi serikali ikigundua kwamba TAA ilikuwa ikijaribu kuunganisha mapambano ya TAA na yale ya KAU.

Hofu hii aliyoonyesha Dr Mutahangarwa ilikuwa bila wasiwasi wowote hofu ya kweli kabisa kwa sababu KAU ilikuwa inaunga mkono harakati za Mau Mau na Waingereza waliamini kuwa uongozi wa mapambano yale ulikuwa ukitoka KAU na Kenyatta wakiwa na Kaggia walishukiwa kuwa kati ya viongozi hao.

Kutoka Mwanza Dossa alipanda meli hadi Bukoba ambako alipokewa na Chifu Rutinwa pamoja na mwanasiasa mkongwe, Ally Migeyo na Suedi Kagasheki na wanachama wengine wa TAA katika tawi la Bukoba.

Aliporudi Dar es Salaam, Dossa alikamatwa katika stesheni ya gari moshi na kupelekwa Central Police.

Kituo hiki kilikuwa mkabala la lango kuu la steshini ya treni.
Dossa alipelekwa pale na kuhojiwa.

Ofisa wa Polisi Mzungu alitaka kujua kwa nini Dossa alikuwa akisafiri na bunduki.

Baba yake Dossa, Aziz Ally aliingilia kati na Dossa akaachiliwa huru bila ya kufunguliwa shtaka lolote.

PICHA: Dossa Aziz, Sued Kagasheki, kushoto wa kwanza Ali Juma Ponda na picha ya mwisho wa kwanza kulia waliosimama ni Dr. Joseph Mutahangarwa na kushoto ni Dr. Luciano Tsere na aliyekaa ni Dr. Vedasto Kyaruzi.

336784711_230646489427892_835704980372944547_n.jpg

Dossa Aziz

337524453_549358067300564_2393189686870707087_n.jpg

Suedi Kagasheki

337358454_883289956295542_7246513004971779869_n.jpg

Kushoto wa kwanza Ali Juma Ponda

337368002_186740894105372_5659850832767832064_n.jpg

Kulia wa kwanza waliosimama Dr. Joseph Mutahangarwa wa kwanza kushoto Dr. Luciano Tsere na aliyepakata mtoto ni Dr. Vedasto Kyaruzi
 
Back
Top Bottom