“Nyanyuka upambane bwana Miguu ya kuku.” Kiongozi wa watekaji waliojinasibu kuwa ni maofisa wa jeshi la polisi, alimwambia huku akimwinua na kumpigisha magoti. Wengine walitengeneza duara na kumzunguka.
“Mr Miguu ya kuku, amka uruke kijogoojogoo..” Jamaa alimdhihaki huku akimshushia konde zito usoni mwake, Zuki hakutaka kulikwepa, aliacha lipige palipolengwa. Wale jamaa walianza kumshushia kipigo kwa kupeana zamu, kila aliyepiga alipochoka alimwachia mwenzake nae apige.
Kipigo chao kilimchakaza bwana Zuki Gadu, uso ulivimba na mdomoni alitoka damu nzito iliyochanganyikana na mate, jicho lake moja lilivimba na hakuweza kuona vizuri, masikio yake hayakusikia kwa ufanisi mkubwa, kila kiungo cha mwili wake kilikuwa hoi kwa maumivu.
Licha ya kupigwa sana lakini jambo moja alilokuwa na uhakika nalo ni kuwa, wale jamaa wasingeliweza kumuua na kulikuwa na kitu walihitaji kutoka kwake na ili kurahisisha mambo, aliamua kuwachokoza ili wamwadhibu na baada ya hapo aliamini wangelivuka hatua ya mwanzo waliokuwa wakimuuliza swali tata na kurukia hatua nyingine ambayo hakuwa akiijua. Hila zake zilifanikiwa kwa sababu aliitabiri vema tabia ya kiongozi wa wale watu, alionekana kuwa mjivuni na mtu ambae hakuwa na uzoefu na aina ya kazi kama zile za utekaji, alionekana ni mropokaji hovyo bila kujali alichoulizwa. Utabiri wake ukatimia pale aliposhushwa na kushushiwa kipigo hadi kuwa na hali mbaya, wakamchukua na kumhamishia kwenye nyumba nyingine safi kwa lengo la kumtibia majeraha aliyokuwa ameyapata. Wakati wakingoja tabibu afike kumsaidia mateka wao, maumivu yalimzidi uwezo na akapoteza fahamu. Zuki Gadu p.a.k Miguu ya kuku, hakufahamu kilichokuwa kikiendelea.
*******
3:
Zuki Gadu alipata fahamu baada ya saa zaidi ya sita kupita, akafumbua macho yake na kujipa utulivu wa dakika kadhaa ili kuziweka vema kumbukumbu zake. Dakika moja ilitosha kuzirejesha kumbukumbu za kilichotokea, kisha akazungusha kichwa chake taratibu na kukitazama chumba alichokuwepo. Hakupata chembe ya shaka kujua ya kwamba alikuwa kwenye chumba cha huduma ya kwanza, hakukuwa na vitu vingi zaidi ya kitanda kidogo alichokuwa amelala na meza iliyokuwa na boksi la vifaa vya huduma ya kwanza. Mwili wake haukuwa umefungwa na kitu chochote, majeraha yalikuwa wazi licha ya kunusa harufu kali ya dawa za kuondoa wadudu kwenye vidonda, jicho lake lilikuwa limepungua uvimbe kiasi aliweza kuona vizuri. Mikono na miguu yake ilikuwa imefungwa vema kwenye tendegu za kitanda, jaribio lolote la kujifungua lisingeliweza kuzaa matunda kwa namna walivyokuwa wamemfunga. Zuki hakutaka kujihangaisha kujinasua kwenye kamba alizofungwa, alitulia na kuruhusu ubongo wake ukabiliane na fikra tunduizi na moja ya maswali mengi yaliyopita kichwani mwake ni kuhusu kilichokuwa kipo nyuma ya tuhuma zilizokuwa zikimkabili swahiba wake, Dodi Danga.
“Namfahamu Dodi, hawezi kuua mtu, Dodi ni miongoni mwa watu wachache ambao hawakupenda kukurukakara na vyombo vya ulinzi na usalama.” Aliwaza huku akiwa kalala chali, macho yake yakitizama juu.
“Kuna kitu kipo nyuma na hicho ndicho kilichonileta huku ili kumsaidia, akipotea ina maana itanilazimu kutafuta mtu mwingine mwaminifu kama yeye aweze kusimamia mradi wa kulea watoto yatima na watu wenye mahitaji maalumu” Alizidi kuwaza huku ari ya kujinasua kwa mabazazi wale ikiongezeka.
“Aliye nyuma ya kutekwa kwangu ni nani? Ndiye aliyenyuma ya sakata la Dodi? Anapanga nini juu yetu?” Alijiuliza maswali mengi bila kupata majibu, wakati akiendelea kujiuliza, akakumbuka kitu kingine cha muhimu kwake.
“Yuko wapi Bob Rando? Yupo salama kweli?” Alipojiuliza kuhusu rafiki yake huyo, ile ari ya kujinasua ikaongezeka kwa sababu alihitaji majibu ya kila swali na hakukuwa na wa kumjibu kama angeliendelea kulala kitandani.
“Mimi si mgonjwa wa kulala kitandani, nahitaji majibu.” Alijiambia mwenyewe huku akipinda shingo yake kutizama kamba zilizokuwa zimifunga mikono yake, akataka kufanya jambo japokuwa hakujua kama atafanikiwa, lakini kabla ya kulitekeleza jambo hilo, pale ndani aliingia mtu, akaahirisha alichotaka kufanya na hesabu zake akazihamishia kwa yule mtu. Yule aliyeingia nae hakuwa na wema wala huruma, alikuwa na jambo lake zito kwa Zuki.
Chumba kikafukuta joto, joto la kifo na uhai.
Nani mshindi? Mimi sijui.
***********
Kwenye moja ya ofisi ndani ya gereza fulani ndani ya jiji la Dar, kulikuwa na ugeni. Ugeni wa mtu aliyejitambulisha ya kuwa ni mwanasheria wa kujitegemea kutoka moja ya kampuni za wanasheria hapa nchini. Mwanasheria yule hakuwa peke yake, alikuwa ameambatana na mwandishi wa habari kutoka moja ya vituo vikubwa vya habari nchini. Mwanasheria yule alikuwa anaelekea kuwazidi hoja maofisa wa jeshi la magereza kwa kile alichohitaji, hoja zake zilibeba uzito zaidi kwa kuwa pembeni yake alikuwepo mwanahabari ambae hakuwa na mipaka kwenye habari za aina ile kama wangeruhusu jambo lile ligeuzwe habari, iwe kwa kutaka ama kutokutaka na endapo habari jngelifika nje ya gereza, ajira zao zingelikuwa mashakani.
“Mimi naondoka, lakini tambueni ni kosa kisheria ofisa wa jeshi la magereza kuzuia mwanasheria kukutana na mteja wake ndani ya gereza, tena nikiwa nimefuata taratibu zote.” Mgeni aliwaambia maofisa waliokuwa kwenye ile ofisi huku akiwa amesimama.
“Aah siyo kama tumekuzuia ila tumepewa zuio la mtu yeyote kuonana na huyo mahabusu na…” Ofisa mmoja aliyekuwa na nyota moja begani alijaribu kutetea.
“Mimi namhitaji huyo mtu aliyetoa zuio la watu kuonana na Dodi Danga.” Mgeni alifoka.
“Itoshe kusema hatujapewa haturuhusiwi kuruhusu mtu yeyote kuonana na Dodi Danga.” Afande aliendelea kushikilia msimamo wake.
“Naomba nikuoneshe nguvu ya sheria.” Mgeni alisema huku akiinua simu yake na kuzitafuta namba fulani kisha akapiga.
“Unampigia nani ndugu.” Afande mwingine aliyokuwa kwenye chumba cha masijara aliuliza huku akimtizama yule mwenye nyota mbili ambae alikuwa haelewi lengo la Mgeni wao kupiga simu.
“Nampigia waziri wa utawala bora, kisha nitampigia waziri wa mambo ya ndani.. Au hamuamini?” Mgeni alisema huku akiwaonesha kioo cha simu yake.
“Hii namba bila shaka mnayo hapa ofisini kwenu.” Alisema huku akirejea kupiga baada ya muito wake kutopokelewa na mhusika.
“Nitamtajia namba zenu za kazi mlioko humu kwa sababu ni ninyi mlionizuia, huyo aliyewatuma endeleeni kulihifadhi jina lake.” Alizidi kupiga mikwara.
“Naomba usubiri kidogo ndugu Wakili msomi.” Ofisa mwenye nyota mbili alimwanbia mgeni wake huku akihangaika kuzungusha mkonga wa simu ya mezani. Sekunde chache baadae aliushusha chini na kumtazama mgeni wake.
“Ulisema unaitwa nani?” Alimuuliza mgeni.
“Wakili msomi, Rashidi Chota.” Mgeni alijitambulisha.
“Sawa bwana Rashidi Chota, nimeambiwa usitumie zaidi ya dakika kumi kuongea nae, lakini uende peke yako na huyu mwenzako abaki hapa.”
“Hapana!” Mwandishi alikataa kisha akasema..
“Ninakibali kutoka mamlaka husika kufanya mahojiano na Dodi Danga” Mwandishi alisema huku akiweka barua mezani, barua ambayo ilikuwa na mihuri mitatu kutoka ofisi alizotaja.
Ofisa alibaki kuduwaa na asijue achukue hatua gani, kukataa alitaka na kukubali alitaka. Mwishowe akaamua kurejea kumpigia aliyekuwa amempigia awali, alieleza shida yake kisha akasikiliza kidogo na kurejesha mkonga kwenye kitezo.
“Wote wawili mtaonana nae ila atatangulia bwana Rashidi Chota, kisha utaingia wewe.” Afande alisema, sekunde chache baadae alimuita ofisa mwingine mwenye cheo cha chini na kumpa maelekezo ya kuwapeleka wageni kwenye vyumba maalumu kwa ajili ya kukutana na mteja wao.
Wakati Wakili Rashidi Chota na Mwandishi Kumbi wakielekea kuonana na Dodi Danga, kwenye moja ya ofisi ya kiongozi wa ngazi za juu pale gerezani, kulikuwa na jambo linaendelea. Kiongozi huyo alikuwa ameshika simu yake akiwasiliana na mtu fulani.
“Sasa inakuwaje mtu anafika ngazi zote hizo ninyi hamfahamu?” Alimfokea aliyekuwa akizingumza nae.
“Unakataa nini wakati Mwandishi huyo yupo hapa na ni Mwandishi kutoka kituo cha taifa, unahisi amekosea gereza?... Au mnataka nifukuzwe kazi ili mnilipe ninyi?” Bwana jela aliendelea kumfokea mtu wa upande wa pili.
“Ooh, kwa hiyo unanitisha kisa kupokea muamala? Basi naurejesha na kesi ikifika nasema ulikosewa nikaurejesha.” Bwana Jela alitamba. Akakaa kimya sekunde chache kisha akashusha pumzi nyingi na kutabasamu.
“Eeh, mambo ndiyo hayo sasa. Picha zao nawatumieni sasa hivi.” Alisema na kukata simu kisha akainuka haraka Kwenye kiti chake na kuelekea kwenye ofisi fulani ambayo haikuwa mbali na ofisi yake. Huko aliingia na kuomba vijana waliokuwa wakifuatilia baadhi ya kamera za usalama pale gerezani, wawashe kamera za vyumba vya mazungumzo ya faragha.
“Mrekodi hizo picha zote na nazihitaji ofisini kwangu.” Aliwaamuru na bila kisubiri jibu lao, alitoka kwenye zile ofisi na kurejea ofisini kwake.
Wakati bwana jela alipokuwa akirejea ofisini kwake, Dodi Danga alikuwa akikaa kwenye kiti na kutazamana na mgeni wake.
“Pole sana bwana Dodi Danga.” Rashidi Chota alianzisha mazungumzo kwa sauti ya chini ili asisikilizwe na ofisa mmoja aliyekuwa ndani ya kile chumba akiimarisha ulinzi.
“Bob Rando…” Dodi alianza kuongea kwa sauti dhaifu huku akioneka kudhoofika kuliko kawaida.
“Hey, usiniite jina langu, hapa nimejitambulisha kwa jina la Rashidi Chota na nipo hapa kama mwanasheria wako.” Bob alimpasha mwenzake.
“Kwa nini umejihatarishia maisha namna hiyo? Hii kesi ina watu wenye nguvu sana nyuma yake.” Dodi Danga alisema huku akionekana kutopendezwa na uwepo wa Rashidi Chota wa bandia.
“Usijali kuhusu mimi, uwepo wangu hapa ni njia ya kusafisha ili wanasheria wa kweli waje kwenye hii kesi yako.” Bob alimwambia dhamira yake.
“Msiendelee kuhatarisha usalama wa wengine, hii namwachia Mungu.” Dodi alisema huku chozi likishuka.
“Acha uzwazwa bwana mdogo, Mungu anakazi nyingi sana za kufanya, usidhani yupo kushugulikia matatizo yako tu na kikubwa nikwambie, Mungu humalizia kazi iliyokwishaanzwa. Ukianza biashara, yeye hutia mkono wake ufanikiwe na kamwe hakuanzishii yeye. Hata wale waovu huwalipa kwa kile walichokianzisha, ndiyo sababu waovu huishia pabaya na wenye wema huishia pazuri, Mungu hilipa sawa na matendo yako.” Bob Rando p.a.k Rashidi Chota, alimpa somo dogo Dodi Danga ambae hakutia neno zaidi ya kukaa kimya.
“Nataka unipe mwanga wa sakata hili kwa haraka haraka.” Bob alimwambia.
“Nenda kwenye nyumba ya zamani ya Zuki iliyoko Tegeta, kwenye boksi la kuhifadhi namba za Luku, kuna ujumbe hapo.” Dodi alimpa maelekezo.
“Good..” Dodi alisema na kunyamaza kidogo kisha akaendelea.
“Kwa kuwa muda wangu nilihisi hautatosha kuongea na wewe, niliambatana na mtu mwingine ambae ungelihitajika kuongea nae kwa kirefu zaidi.”
“Yupo wapi mtu huyo?”
“Yupo kwenye foleni nje ya chumba hiki.. Lakini kwa kuwa kuna sehemu naweza kuanzia, naomba ukatae kuongea nae…”
“Una maanisha nini?”
“Namaanisha unayo haki ya kukataa kuongea na mgeni yeyote, tumia haki yako kumkataa.”
“Ni vipi kama hataukuta ujumbe huo, huoni kama utakuwa umekosa vyote?”
“Nikiukosa, atarejea tena” Dodi alisema huku akiinuka na kabla ya kupiga hatua nyingine, alimtazama Dodi kwa macho makavu.
“Nini!” Dodi alishangaa aina ya jicho lile, alijua kuna jambo.
“Una uhakika huhusiki na yaliyotokea?” Bob alimuuliza kwa sauti kavu tofauti na mwanzo.
“Hakika hakuna ninalojua.” Dodi alijibu.
“Basi usikae kinyonge. Ngoja tuuze roho hadi tununue wako” Bob alimwambia.
“Kuwa makini Bob!” Dodi alimuonya.
“Siitwi Bob, naitwa Rashidi Chota..” Bob alinyamaza kidogo kisha akasema,
“Miguu ya kuku kakanyaga ardhi hii. Vimba mwanangu.” Bob alitabasamu na kusukuma kiti nyuma kisha akapiga hatua kuelekea mlangoni, nyuma yake alisindikizwa na jicho la Dodi Danga aliyekuwa amejawa na furaha baada ya kusikia uwepo wa Zuki Gadu p.a.k Miguu ya kuku. Alijihisi mshindi japo hakujua ameshinda mtihani upi kati ya mingi iliyokuwa mbele yake.
“Ahsante Mungu.” Alisema huku akisimama, askari aliyekuwa kando alimfuata na kumpa taarifa ya uwepo wa mtu mwingine aliyehitaji kuonana nae.
“Nimechoka, sihitaji kuongea na mtu mwingine tena. Nirejeshe ninakotakiwa kuwa.” Alisema huku akisukuma kiti nyuma na kupata nafasi ya kurudi nyuma huku akiiacha meza ya mazungumzo ikiwa haina mtu. Askari hakuwa mbishi alielewa haki za mahabusu na wafungwa wake, moja ya haki hiyo ni kuheshimu maamuzi yao ambayo hayaingiliani na utendaji kazi wake. Alimsindikiza kurejea kwenye sero yake huku yule mgeni aliyekuwa akisuburi, aliishia kupewa taarifa na kutakiwa kurejea siku nyingine.
Nje ya gereza wageni wa Dodi Danga walipanga gari moja huku dereva akiwa ni Bob Rando. Waliondoka kwenye viunga vya gereza huku kazi yao ikiwa imefanikiwa kwa kiasi kikubwa, walipongezana wakati wakiendelea na safari yao.
“Ila wewe jamaa ni noma aisee!” Mwandishi alianza kuongea huku akimtizama mwanasheria bandia.
“Huamini kama mimi ni mwanasheria?” Bob alimuuliza huku akicheka kwa kebehi.
“Asiyekujua anaweza kuamini.. Ila umeuvaa uhusika pale ofisini hadi nikatamani kuachia cheko.” Mwandishi aliendeleza mjadala.
“Unashangaa uhusika wa dakika chache hizo, nimewahi kukaa Congo nikiwa mchungaji kwa zaidi ya miaka mitano, nikaaminika na uchungaji wangu, nikauza silaha nyingi kwa mgongo wa utumishi, mwisho wa siku nikapotea bila kuaga.” Bob alimpasha asiyoyajua huku akiangalia kioo cha upande wake, akaishia kuguna.
“Oya Kisu! Hebu kuwa makini na hiyo pikipiki nyuma ya hilo gari jeupe.” Bob alimwambia mwenzake huku yeye akiwa makini kutizama mbele, alihitaji kuwa na uhakika na kile alichokihisi kuhusu watu waliokuwa kwenye pikipiki. Kila alipokuwa akiongeza mwendo na wao waliongeza huku wakionekana kutokutaka kuipita gari iliyokuwa mbele yao.
“Huu ni mkia wa fisi, wapo na sisi.” Kisu alimwambia Bob.
“Twende tuwabwage hapo mataa.” Bob alisema huku akiipita gari moja iliyokuwa mbele yake kisha akaongeza mwendo zaidi na kuweka umbali fulani na ile pikipiki.
“Chukua hayo mafuta upake kioo cha mbele usawa wa mtu kupita.” Bob alimwelekeza mafuta yalipokuwa kwa kumnyooshea kidole, Kisu akayachukua na kufanya kama alivyoelekezwa.
“Chukua kilicho chako na ukikumbatie vizuri kabisa.” Bob aliendelea kumwelekeza Kisu ambae alitii maelekezo bila kuhoji.
Mita chache mbele kulikuwa na foleni ya magari baada ya taa nyekundu kuwaka kuashiria magari ya upande wao kusimama.
“Tunawabwaga hapa.” Dodi alisema huku akizima gari na kuweka mkono wake mmoja pale alipoelekeza kupakwe mafuta fulani ya kuvunja vioo, alisukuma kidogo na kioo kilitawanyika.
“Nenda zako, usipite mlangoni.” Bob alimwelekeza Kisu ambae kwa kasi alichomoka na kuwa juu ya boneti kisha akaruka na kutua mbele ya gari, Bob nae alifuata na kuliacha gari tupu.
“Tunyooshe mbele wale wajinga wasitune kama tumetoka.” Bob alimwambia mwenzake huku akianza kutembea kwa kasi kuelekea mbele, Kisu nae alipita upande mwingine na kusonga mbele huku akigeuka kutazama nyuma.
“ Wana wanachomoa zana kuelekea kwenye gari letu.” Kisu alimwambia Bob.
“Achana nao, vuka upande wa pili na…” Bob alisema huku akihamia njia nyingine, nyuma yake Kisu alifuatia. Walipiga hatua chache baada ya kuvuka na masikio yao yakasikia mirindimo ya risasi, walipogeuka walishuhudia watu wawili waliokuwa wamepakizana kwenye pikipiki, wakilishambulia gari lao kwa risasi kisha wakaondoa pikipiki kwa kasi na kuacha taharuki ikiwa imetanda kwenye barabara ile.
“Wajinga walidhamiria kutugeuza tenga kwa risasi zao.” Kisu alisema huku akiwatizama wale jamaa walivyokuwa wakiharakisha kukimbia na pikipiki yao.
“Acha walipwe ujira wa kazi ambayo hawajaifanya.” Bob alisema huku akisimamisha bajaji na kumshitua mwenzake wapande kuelekea mahali fulani
*****
Tukutane baadae