Kudo
JF-Expert Member
- Nov 2, 2017
- 1,821
- 6,122
RIWAYA; DOMOKAYA.
NA; BAHATI K MWAMBA.
SIMU; 0758573660/0658564341.
1.
Walishushwa kwenye basi la wafungwa na kuamriwa kuchuchumaa huku wakiwa wamefungwa pingu za miguu na mikono, afya zao hazikuwa imara sana, wengi walionekana dhoofu na wenye nyuso za kukata tamaa. Nyuma yao walisimama maofisa wa kikosi maalumu kutoka jeshi la Magereza, bunduki mikononi mwao na nyuso zenye shari zilikuwa nyuma ya migongo mahabusu na wafungwa waliokuwa wamechuchumaa.
Mahabusu na baadhi ya wafungwa ambao walikuwa wamerejea mahakamani baada ya rufaa zao kuanza kusikilizwa, waliinuliwa na kuongozwa kuingia kwenye sero maalumu ndani ya majengo ya mahakama kuu kanda ya Dar es laam, ulinzi ulikuwa mkali ndani na nje ya sero huku baadhi ya ndugu wa mahabusu na wafungwa wakizuiliwa kuwaona ndugu zao kama walivyozea siku za nyuma. Baadhi walijaribu kupenyeza rupia ili angalau wazisikie sauti za ndugu zao waliokuwa wakisota gerezani, lakini siku hiyo mambo hayakuwa kama walivyozoeshwa huko nyuma ambapo walitoa rushwa kwa maofisa wa magereza wanaokuwa kwenye mlango wa chumba cha watuhumiwa ndani ya mahakama, ili wazogoe na ndugu zao kwa uhuru zaidi kuliko wanavyokuwa wamekwenda kuwatembelea moja kwa moja gerezani.
Watu walijiuliza kuhusu kilichokuwa kikiendelea siku hiyo pale mahakamani, hawakupata jawabu na hakukuwa na kuwapa jawabu hilo kwa sababu itifaki ilizingatiwa, walitakiwa kukaa sehemu ya mapumziko na kungojea majina yao kuitwa ili wakasikilize uendeshwaji wa kesi za ndugu na jamaa zao. Viulizo hivyo kuhusu ulinzi mkali kwa mahabusu na wafungwa havikuwa kwa ndugu pekee, hata baadhi ya wafanyakazi wa mahakama walishangaa ijapokuwa walielewa ulinzi wa namna ile huwa ni kwa wafungwa hatari na wenye kesi kubwa, walishangaa kwa sababu hawakumbuki mara ya mwisho kuona tukio kama lile ilikuwa ni wakati gani tangu waajiriwe kama watumishi ndani ya mahakama kuu.
Mshangao huo haukuwa kwa wafanyakazi hao pekee, mshangao uliwakuta hadi wafungwa na mahabusu waliokuwa kwenye msafara ule wenye ulinzi mkali, hawakuwahi kuwa kwenye uangalizi mkubwa namna ile tena wengi wao wakiwa wamedhibitiwa kwa pingu za mikono na miguu.
Wengi wao licha ya kushangaa baadhi yao kufungwa namna ile lakini hawakuhofia sana kwa sababu asilimia kubwa, walikuwa wakifahamiana kwa maana ya kukaa mahabusu kwa muda mrefu, lakini kati ya wote hao, ni mtu mmoja tu ambae hakuwa akifahamika miongoni mwao na mtu yule alikuwa ni mahabusu kwa sababu alikuwa hana nguo maalumu za wafungwa.
Mtu yule alikuwa ni dhaifu ukimtizama, vidonda vibichi vilikuwa vimejenga himaya kwenye mwili wake kuonesha alipitia shuruba kabla ya kujumuishwa miongoni mwa mahabusu waliokuwa wamekwenda kusikiliza mienendo ya kesi zao. Wengi walijiuliza kuhusu mahabusu yule ambae alionekana kuwa mkimya wakati wote huku akiwa ni mwenye kukata tamaa.
Kukata tamaa au kuzama kwake mawazoni hakukuwa sababu kwa wenzake waliokuwa wameswekwa sero moja yenye hewa nzito ndani yake, walihisi pengine ni kwa sababu ya ugeni wake gerezani na tuhuma zilizomkabili, sababu kubwa iliyowafanya wajiulize ni namna ilivyotokea na wakajikuta wamepandishwa gari moja na yule bwana na kanuni ya usafirishwaji wao ikiwa imebadilika na kuwa yenye ulinzi mkali kuanzia gerezani hadi mahakamani.
Walishangaa kwa sababu ili uwe mahabusu ni lazima kesi yako iwe imewahi kutajwa mahakamani, lakini wao hawakuwahi kumuona yule bwana hapo kabla na hata kwenye kundi la mahabusu waliokuwa wakingojea tarehe za kesi zao, hakuwemo. Wao walimkuta ndani ya basi chini ya ulinzi mkali na walipotimia kwa idadi ikalazimu na wengine watendewe kama alivyokuwa ametendewa mtu yule, walifungwa pingu mikononi na miguuni huku idadi ya maofisa ikiwa ni kubwa tofauti na siku zingine. Maajabu kwao yalikuwa ni kuona msafara wao ukisindikizwa na gari nne, mbele mbili na nyuma mbili huku maofisa wengi wakiwa kwenye gari hizo na silaha mikononi mwao.
“Kwani leo kuna nini?” Mfungwa mmoja alisikika akimuuliza mwenzake kwa sauti ya chini sana.
“Kwa hiyo uliambiwa mimi ni mnajimu? Au uliambiwa nina ukoo na sheikh Shariff Majini nitabiri kinachoendelea?” Mfungwa aliyeulizwa alimtolea uvivu mwenzake kwa kuwa hata yeye alikuwa kwenye sintofahamu.
Ndani ya sero yule bwana mkimya alitengwa na wenzake, aliamriwa kukaa kwenye kona ya chumba huku ofisa mmoja akiwa kando yake na bunduki mkononi. Hakika ilikuwa ni ajabu ofisa wa magereza kukaa ndani ya chumba cha sero na watuhumiwa, chumba ambacho hakikufaa kwa lolote na ilionekana kipo maalumu kwa ajili ya watuhumiwa tu na si watu wengine, kilikuwa kichafu na chenye harufu nzito. Maswali mengi kwao kuhusu mtu yule hakukuwa na wa kuyajibu, walibaki watazamaji na kungojea hatima ya kesi zao.
Wakati wengine wakijiuliza maswali mengi kuhusu mahabusu huyo, mhusika mwenyewe nae alikuwa kwenye viulizo vingine ambavyo hakuwa akijua mwisho wake, wakati wenzake wakimuona akiwa kajiinamia, mwenzao alikuwa amezama kwenye tanuri kubwa la mawazo.
“Kwa nini kila kitu kinaonesha mimi ndiye niliyehusika na vifo vyao wote?” Alijiuliza huku akijaribu kukumbuka baadhi ya matukio yaliyomfanya afike pale.
“Hata jua lingeamua kugeuka kamwe nisingeinua kisu kumuua mke wangu wala yule hawala wake, nisingeweza.” Aliwaza huku akitikisa kichwa peke yake bila kujijua, kisha aliinua uso wake na kutizama juu, alihisi akitazamana na sura ya mke wake iliyojaa majonzi na uso wa majuto.
“Ulinitesa kwa maumivu ya mapenzi, nilikulilia wivu huku nikiwa na fukuto la maumivu moyoni mwangu lakini hukunielewa, bado umekufa kifo chako ila mimi naadhibiwa kwa ajili yako. Ni lipi kosa nililokutenda hadi uamue kunipitisha njia hii?” Alisema kwa sauti ndogo ambayo haikuwafikia watu wengine waliokuwa kwenye kile chumba maalumu kwa mahabusu.
“Ok, tuyaache hayo, ni kweli ulikuwa umeolewa mara ya pili? Je, ni mimi mume wa kwanza au nilikuwa ni wa pili nisiyetambuliwa?” Aliendelea kuongea huku chozi likichukua himaya kwenye mashavu yake kwa kutengeneza mchirizi kuelekea kidevuni.
“Nijibu basi, au bado unanidharau? Bado hujafurahi na haya ninayopitia?” Alizidi kuongea huku wakati huu akiongeza sauti kidogo kiasi baadhi ya mahabusu waligeuka na kumtazama huku ofisa aliyekuwa akimlimda, akipiga hatua kumfuata.
“Yaani unataka kuchanganyikiwa kabla hata ya kumuona Jaji?” Ofisa alimwambia huku akimalizia kwa kucheka kicheko cha unafiki.
“Usiwe muoga, wewe ni mwanaume, jikaze.” Alimwambia kwa mara nyingine huku akiendelea kutabasamu kwa dhihaka.
Jamaa alikaa kimya bila kumjibu askari yule ambae hakuwa akijua kilichokuwa kikimsibu mahabusu wake, alichojali wakati huo ni kila mmoja ndani ya sero kufuata utaratibu ikiwa ni pamoja na kukaa kimya, mahakamani siyo sehemu ya kupiga kelele.
Wakati hayo yote yakitokea, mahabusu wengine walikuwa wakiendelea kuitwa kwenda kujitetea kwa tuhuma zilizokuwa zikiwakabili.
“Lakini sikuuwa mimi, nilimpenda mke wangu na nisingeliweza kufanya hivyo, tena nimuue na bwana'ake! Nisingeweza.” Aliendelea kuwa mawazoni huku akionekana kuumia kwa kilichokuwa kikitokea dhidi yake.
“Lakini ni nani aliua na kwa nini aliwaua? Kwa nini mimi ndiye nionekane nimeua?” Aliendelea kujiuliza huku dhahiri akionekana kuumia moyoni mwake.
“Dodi Danga!” Sauti nzito ya afande ilisikika kutokea mlangoni.
Mahabusu waligeuka nyuma na kumtazama jamaa aliyekuwa ametengwa peke yake, angalau walielewa aliitwa Dodi Danga kwa kuwa aliinuka baada ya jina kutajwa. Dodi alipita kando yao taratibu huku akivuta miguu yake ambayo ilibanwa vema na pingu za miguuni, nyuma yake alikuwepo ofisa wa magereza akiwa ameshika bunduki yake. Ukimya ulikuwa mkubwa na kilichosikika ni hatua zake, mlangoni alipokelewa na moafisa wengine ambao walimuongoza kuelekea kwenye chumba cha mahakama. Nje ya mlango wa mahakama kulikuwa na watu wengi wenye kamera na wengine simu za mkononi, alishangaa namna walivyochangamka baada ya kumuona, waligombea kupata nafasi ya kumpiga picha za kila aina, mnato na zile picha mjongeo. Dodi alishangaa na kuingiwa mfadhaiko, hakuwa amejiandaa kwa tukio kama lile na wala hakuwa amehisi kuna jambo litatokea la namna ile.
“Kwa nini napigwa picha na hawa waandishi? Au ni kawaida yao kuwapiga picha kila mahabusu wanaopita kuingia kwenye chumba cha mahakama?” Alijiuliza bila kupata jibu huku wakati huo maofisa waliokuwa nyuma yake wakimsukuma atembee haraka, lakini angeliwezaje kutembea haraka ikiwa amefungwa pingu miguuni? Angelitembea haraka wakati alikuwa amefungwa mikononi? Hakika aliona anaonewa kulazimishwa kufanya mambo ambayo waliomlazimisha walijua hataweza kuyafanya, lakini kikubwa aliona hawakuwa na utu ndani yao na walikiuka haki za binaadamu hadharani.
“Kwani huko nje kinaendelea nini?” Alijiuliza huku akiingia kwenye chumba chumba cha mahakama, aliongozwa kuingia kizimbani na askari wawili wakasimama pembeni ya kizimba. Kwa mara nyingine mshangao ulijenga himaya kichwani mwake, watu wengi sana walikuwa kwenye kile chumba cha mahakama na wengine walikosa nafasi ya kukaa na walibaki wakiwa wamesimama kwa utulivu mkubwa. Hakukuwa na taratibu za mwanzo za kimahakama kama vile; kuingia kwa Jaji na wazee wa baraza, askari wa mahakama kuamuru watu kusimama wakati wa kuingia kwa Jaji na taratibu nyinginezo. Yote hayo hayakufanyika kwa sababu tayari kesi kadhaa zilikuwa zimeshasikilizwa na yule Jaji na baraza lake, hayo hayakumshitua Dodi Danga, kilichomshitua ni namna kesi yake ilivyokuwa imeharakishwa kupelekwa mahakama kuu bila kupitia ngazi nyingine za kimahakama hadi kufikia hatua ya kupangiwa Jaji wa mahakama kuu kuisikiliza kesi yake.
Dodi Danga alishangaa kwa kuwa kesi ilikuwa imefika mahakama kuu na hakuwa amepewa nafasi ya kumpata wakili wake au serikali kumpa wakili kama angeshindwa kumudu gharama binafsi za mwanasheria anaemuamini.
“Tuhuma zangu ni kubwa sana na ninayo haki ya kuwa na mwanasheria atakae simamia kesi yangu, iweje hadi sasa kesi inasomwa ikiwa sina wakili? Au nitapewa fursa hiyo baada ya shitaka kusomwa kwa mara ya kwanza?” Alijiuliza huku akimtizama Jaji aliyekuwa amekaa kwenye meza yake akiendelea kupitia makabrasha yake, alizungusha macho na kumtizama karani wa mahakama namna alivyokuwa bize kukusanya karatasi zilizokuwa mezani kwake, mwisho alimalizia kwenye viti vitatu vilivyokuwa na mawakili watatu ambao hakujua walikuwa upande gani, wa mashitaka dhidi yake ama watetezi wake, alisubiri kuona kitakachofuata.