Dokta Ulimboka achafua Bunge

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,322
33,126
Ni malumbano makali Chadema,CCM
headline_bullet.jpg
Manyanya amfananisha na Hitler
ulimboka%283%29.jpg

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Steven Ulimboka.


Kuyumba kwa Mwenyekiti wa Bunge, Sylvester Mabumba na kauli zilizojaa hisia kali na kashfa ni miongoni mwa mambo yaliyofunika Bunge na kutishia mustakabali wa mjadala kuhusu sakata la kutekwa, kuteswa na kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Steven Ulimboka.

Hali ilianza kubadilika baada Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi, kutaka Bunge liunde tume huru kuchunguza sakata hilo, vinginevyo serikali haitaaminika katika kadhia hiyo.

Mbilinyi maarufu kama “Mr. Sugu”, alisema hayo wakati akichangia mjadala wa hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani, kuhusu makadirio ya matumizi ya fedha kwa mwaka 2012/2013, bungeni jana.

Alisema masaibu yaliyomkuta Dk. Ulimboka, hayatofautiani na yaliyowakuta wabunge wawili wa Chadema; Highness Kiwia (Ilemela-Chadema) na Salvatory Machemli (Ukerewe), ambao walishambuliwa na kujeruhiwa kwa sababu tu ya kusema ukweli.

Wakati Mbilinyi akizungumzia kadhia hiyo ya Dk. Ulimboka, Mabumba, alimtahadharisha kuwa katika kuzungumzia suala hilo ahakikishe awe na ushahidi.

Alisema Rais wa Sudan, Omar Al-Bashir, alipotaka kuishambulia Darfur, hakutumia majeshi rasmi ya nchi hiyo, badala yake alitumia “Janjaweed”.

Kutokana na hilo, alisema kama serikali haikuhusika, basi waliohusika na kadhia ya Dk. Ulimboka watakuwa ni kikundi cha kigaidi cha “Janjaweed”.

“Kwa hiyo, kama serikali haikuhusika, basi hapa kwetu kuna elements (dalili) za Janjaweed,” alisema Mbilinyi.

Kauli hiyo ilimfanya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk. Mary Nagu, kusimama na kuomba utaratibu.

Aliporuhusiwa na Mwenyekiti wa Bunge, Mabumba, Dk. Nagu alinukuu kanuni ya Bunge inayomzuia mbunge kuongea bungeni jambo ambalo hana uhakika nalo, hivyo akamtaka Mbilinyi kuthibitisha kauli yake.

Mabumba alisimama na kumweleza Mbilinyi kuwa tangu mapema alikuwa amekwisha kumtahadharisha kutoongea jambo kama hilo bila ya kuwa na ushahidi, hivyo akamtaka atoe ushahidi.

Mbilinyi alirejea na kusema Dk. Ulimboka alitekwa na dunia nzima inajua hilo.

Kauli hiyo ilimfanya Mabumba kusimama tena kwa nia ya kumwelekeza jambo Mbilinyi, lakini wakati akiwa amesimama, Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, naye pia alikuwa amesimama kuomba Mwongozo wa Spika.

Hata hivyo, Mabumba akiwa amesimama, alimwamuru Lissu kukaa chini, lakini Lissu akiwa amejawa na hasira, alikataa kutii amri hiyo.

Lissu alianza kujibizana na Mwenyekiti huyo wa Bunge, ambaye alimtishia kuwa iwapo ataendelea kutotii amri yake ya kukaa chini atamtoa nje ya ukumbi wa Bunge.

Lissu alikaa, lakini akiwa amekaa aliendelea kujibizana na Mabumba.

Baadaye, Mabumba alimtaka Mbilinyi kuendelea kuchangia mjadala wa hotuba hiyo, lakini azungumze jambo lingine kama hana ushahidi wa suala la Dk. Ulimboka.

Mbilinyi alimweleza Mabumba kuwa kauli yake ililenga kubadili jambo ambalo hakulizungumza na kwani hakusema kuwa Tanzania kuna Janjaweed.

Alisema kutokana na namna kadhia ya Dk. Ulimboka ilivyo, Bunge linapasa kuunda tume huru kama vile ilivyounda kamati teule ya kuchunguza kashfa ya kampuni ya Richmond iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe.

“Vinginevyo, katika hili (la Dk. Ulimboka) serikali haitaaminika,” alisema Mbilinyi.

Hata hivyo, Mbilinyi alisema yaliyotokea kwa wabunge wa Chadema na kwa Dk. Ulimboka ni kosa ambayo yanajulikana katika Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC) kuwa ni matoso. “Hii ni toture,” alisema.

Hali ya mabishano makali ilikuwa mbaya zaidi wakati akichangia mbunge wa Viti Maalum na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa (CCM), Stella Manyanya, ambaye alisema kuwa Chadema wanahusika na mgomo wa madaktari, hali iliyomuinua Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, akitaka mbunge huyo wa CCM kuthibitisha kauli yake.

Manyanya pia alikwenda mbali zaidi akisema kuwa shambulizi dhidi ya Dk. Ulimboka ni mpango wa Mungu wa kumuokoa asiendelee kuongoza mgomo huo kwani watu wengi wangekufa naye angekuwa kama aliyekuwa Kansela wa Ujerumani Adolf Hitler aliyesababisha vita kuu ya II ya dunia.

Hata hivyo, Mabumba baada ya kusikia alichotaka Mnyika, alimwambia kuwa ni vema akathibitisha yeye kwanza kwamba Manyanya alisema uongo kama alivyokuwa ameeleza awali Lissu kuwa kanuni za Bunge zinataka anayetuhumu mwenzake kusema uongo aeleze kwanza ukweli ni upi.

Hata baada ya Mnyika kusema kuwa akiwa kama kiongozi wa Chadema kwa nyadhifa mbalimbali, hakuna kokote ambako chama chao kimekaa na kusema kuwa wanaunga mkono mgomo, bado Mabumba hakuzingatia hoja hiyo ili kumtaka Manyanya afute au athibitishe kauli dhidi ya Chadema.

Hata kabla ya Mabumba kusema lolote, aliibuka Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba (CCM) na kusema kuwa ana uhakika kuwa Chadema wanaunga mkono mgomo na kusoma hotuba ya msemaji wa kambi ya upinzani kuhusu makadirio ya Utumishi iliyowasilishwa jana kuwa wanaunga mkono harakati za migomo ya watumishi wa umma.

Mabumba alisema kuwa kila aliyepewa taarifa amesikia, lakini Bunge likikaribia kuahirishwa, Mbunge Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali, alitolewa nje ya ukumbi wa Bunge baada ya kuomba muongozo kwa kusimama mfululizo na kukaidi amri ya mwenyekiti ya kumtaka akae.






CHANZO: NIPASHE
 
Back
Top Bottom