Stephano Mgendanyi
JF-Expert Member
- May 16, 2020
- 3,119
- 1,428
DKT. SAMIA KUJENGA VITUO 50 VYA KUHIFADHI PARACHICHI
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Mbeya kuwa Serikali imejikita katika kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi, kwa kuwekeza katika mazingira bora ya kazi na biashara.
Akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Tukuyu mkoani Mbeya katika mkutano wa kampeni leo Septemba 5, 2025, Dkt. Samia amebainisha kuwa moja ya maeneo ya kipaumbele ni sekta ya kilimo, hususan uzalishaji wa parachichi, ambao sasa umepata soko la kimataifa.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali imepanga kujenga vituo 50 vya kuhifadhi parachichi nchini, ambavyo vitakuwa na miundombinu ya baridi ili kuongeza muda wa uhifadhi wa zao hilo.
Miongoni mwa vituo hivyo, viwili vitajengwa wilayani Rungwe, mkoani Mbeya.
“Vituo hivi vitahifadhi parachichi kwa muda wa hadi miezi mitatu ili tukisubiri mataifa mengine yakamilishe msimu wao wa uzalishaji na sisi tuweze kuuza parachichi zetu kwa bei nzuri sokoni,” amesema Dkt. Samia.
Kuhusu zao la chai, Dkt. Samia ameeleza kuwa Serikali itaunda timu maalumu kwa ajili ya kufanya tathmini ya mashamba na viwanda vya chai, ambavyo vimekabidhiwa kwa kampuni binafsi lakini hazijatekeleza majukumu yao ipasavyo.