Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe
Moto wa mawaziri wa kuwashughulikia watendaji na watumishi wa serikali wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali, ikiwamo kushindwa kuwajibika katika maeneo yao ya kazi, umezidi kusambaa, ambapo safari hii Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ametengua uteuzi wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Paul Chizi.
Pia amewasimamisha kazi watumishi wengine wanne wa vitengo vya uhandisi, sheria, fedha na biashara vya shirika hilo.
Hatua hiyo imechukuliwa na Waziri Mwakyembe zikiwa zimepita siku chache baada ya mawaziri wengine; Dk. Abdallah Kigoda (Viwanda na Biashara) na Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), kuwasimamisha kazi viongozi waandamizi wa sekta zinazogusa wizara wanazoziongoza.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Omar Chambo, alisema kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari jana kuwa hatua dhidi ya Chizi imechukuliwa kutokana na uteuzi wake kutofuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Hivyo, kupitia Sheria Na. 8 ya mwaka 2008 na kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2003 Na. 17 (4), Mheshimiwa Dk. Harrison Mwakyembe, Waziri wa Uchukuzi ametengua uteuzi wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania kuanzia Juni 5, 2012, alisema Chambo.
Alisema kanuni hiyo inaeleza bayana kuwa kama mtumishi atakuwa ameteuliwa kwa kukiuka kifungu cha 17 (1) au (3) cha kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2003, itakuwa na mamlaka ya uteuzi kutengua uteuzi wa utumishi wake mara moja.
KAPTENI LUSAJO ATEULIWA
Kutokana na hatua hiyo, Waziri Mwakyembe amemteua Kapteni Lusajo Lazaro, kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL kuanzia jana.
Chambo alisema Waziri Mwakyembe pia amewasimamisha kazi watumishi wengine wanne wa ATCL, akiwamo Kaimu Mkurugenzi wa Uhandisi wa Shirika hilo, John Ringo, kutokana na ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Alisema ukiukwaji huo wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, ulitishia uhai wa chombo hicho muhimu cha taifa.
Wengine waliosimamishwa, ni Amini Mziray (Mwanasheria), Justus Bashara (Kaimu Mkurugenzi wa Fedha) na Josephat Kagirwa (Kaimu Mkurugenzi wa Biashara).
Alisema kupitia ukiukwaji huo, itaundwa kamati ya wajumbe watatu wenye uelewa wa mambo ya fedha na sheria ili kuchunguza matumizi ya fedha iliyopokelewa kuanzia mwanzoni mwa Mei, mwaka huu.
CHIZI AZUNGUMZA
Saa chache baadaye jana, Chizi alinukuliwa na Televisheni ya ITV akisema aliteuliwa kukaimu nafasi hiyo Agosti, mwaka jana, hivyo amepokea na anakubaliana na uamuzi uliochukuliwa dhidi yake.
Kabla ya uteuzi wake, ATCL ilishindwa kuendesha shughuli zake, hivyo akateuliwa kurudisha hadhi ya shirika hilo na kwamba alijitahidi kufanya kazi hiyo kwa uwezo wake.
Kama uteuzi umetenguliwa nashukuru kwa hilo, alisema Chizi na kuongeza kabla ya uteuzi wake kutenguliwa alikuwa tayari kishaingia mkataba wa kununua ndege ya pili ya shirika.
Nawashukuru Watanzania kwa ushirikiano, hususan vyombo vya habari na wote waliokuwa wakifurahia huduma za shirika. Nitachangia kwa njia nyingine ambazo nchi itaona zinasaidia, alisema Chizi.
Mei 17, mwaka huu, Waziri Kigoda aliiagiza Bodi ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kumsimamisha kazi Mkurugenzi wake Mkuu, Charles Ekelege.
Hatua hiyo ilichukuliwa dhidi ya Ekelege kupisha taratibu za kisheria, ikiwamo kufanyika uchunguzi dhidi yake.
Waziri Kigoda alisema moja ya sababu iliyomfanya Rais Jakaya kikwete afanye mabadiliko ya uongozi katika wizara hiyo, ilikuwa ni TBS, baada ya kuwapo mjadala mkubwa bungeni kuhusu utendaji wake.
Wakati akitangaza mabadiliko ya Baraza lake la Mawaziri Mei 4, mwaka huu, Rais Kikwete alizungumzia azma ya serikali kuchukua hatua kwa watendaji wengine wa serikali na taasisi zake ambao alisema ni chanzo cha mabadiliko hayo.
Kikwete alisema mawaziri wamekuwa wakijiuzulu hata kwa makosa ambayo si yao na kwamba serikali itaanza kuchukua hatua kwa watendaji, wakiwamo makatibu wakuu, wakurugenzi wa wizara, watendaji wakuu wa mashirika na taasisi za umma pamoja na bodi za mashirika husika.
Kadhalika, Mei 29, mwaka huu. Balozi Kagasheki ambaye awali alikaririwa akisema yuko katika vita kali dhidi ya wahujumu wa wanyamapori, aliwasimamisha kazi vigogo Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) pamoja na askari 28 wa wanyamapori wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa).
Hatua hiyo ilichukuliwa na Waziri Kagasheki kutokana na vifo vya faru wawili vilivyoripotiwa hivi karibuni.
CHANZO: NIPASHE