Deus Kibamba: Kwa kigezo cha Viwanja Bora, Nani Ataishinda Morocco Uenyeji wa AFCON 2025?

Pfizer

JF-Expert Member
Mar 25, 2021
305
519
Na Deus M Kibamba

Morocco: Nilitembelea viwanja mbalimbali vya mpira wa miguu nchini Morocco kwa lengo la kuvipima kwa viwango vya kimataifa vinavyowekwa na FIFA na CAF kwa ajili ya michuano ya Kombe la Dunia 2026 na CAF kwa ajili ya kombe la mataifa mwaka 2025 nikafarijika sana kwamba Afrika tuko juu, tena juu sana. Kwa viwango vya FIFA, tayari viwanja vingi vya Moroccovimekidhi vigezo kiasi cha kuruhusiwa kutumika katika hatua za mchujokuelekea makundi mwaka 2022.
IMG-20230208-WA0009.jpg

Katika mwezi October mwaka 2021, Morocco ilizipokea timu za mataifa mbalimbali zilizokuja kucheza mechi kwa ajili ya kufuzu michuano ya FIFA 2022 Qatar. Sababu kubwa ya timu hizo kuchagua Morocco ilikuwa ni kwa ajili ya kucheza katika viwanja vyenye miundombinu na huduma zinazofikia viwango vya FIFA ili watakapofuzu kwenda Qatar wasiende kupata mshangao. Hiyo ilikuwa ni kati ya tarehe 12 – 16 Oktoba.

Mwezi mmoja baada ya mechi hizo yaani kuanzia tarehe 12 November 2021, Morocco pia ilipokea ugeni kutoka nchi 10 zilizokuja kujikabidhi kwa nchi hiyo kwa ajili ya mechi kama hizo za kufuzu Kombe la Dunia 2022. Itashangaza wengi kuwa kutokana na kuwa mechi nyingi katika hizo zingepaswa zichezwe katika nchi nyingine, baadhi ya mechi zilichezwa huku mwenyeji wa mechi akiwa siyo Morocco.

Kwa mfano, katika mechi iliyopigwa siku ya Ijumaa tarehe 12 Novemba 2021 kuanzia saa 2 usiku kwa saa za Morocco, Sudan alikuwa mwenyeji wa Morocco katika uwanja wa kisasa wa Prince Moulay Abdellah jijini Rabat. Siku hiyo hiyo, Burkina Faso walikutana na Niger katika bonge la uwanja uliopo Marrakech kuanzia saa 8 Mchana huku Burkina Faso wakiwa ndio wenyeji wa Niger. Siku iliyofuata, Liberia ilimenyana na Nigeria katika kundi C kwenye uwanja wa kisasa wa Tangier, kusini magharibi mwa Morocco. Mwenyeji wa mechi hii iliyoanza saa 11 jioni alikuwa niLiberia.

Kwa mechi za Kundi E kwa timu za Afrika kuelekea Qatar, Guinea Bissau walikutana siku ya Jumatatu tarehe 15 Novemba 2021 katika uwanja wa Marrakech kwenye mechi ambayo filimbi yake ilipulizwa saa 11 jioni kuashiria kuanza kwa kabumbu. Aidha, kulikuwa na mtanange kati ya wenyeji Morocco na Guinea iliyopigwa tarehe 16 Novemba ikianza saa 2 usiku kwa saa za Africa Magharibi ambayo ni sawa na saa 4 usiku kwa saa za Afrika Mashariki. Mechi hii ilipigwa katika kituo cha kisasa cha michezo cha Mohammed V, Jijini Casablanca.

Baada ya Kombe la Dunia kukamilika nchini Qatar, FIFA hawakuishia hapo na Morocco. Iliamuliwa kuwa michuano ya Kombe la Dunia klabu la FIFA 2022 izinduliwe na kufanyika Morocco.Ilikuwa ni bahati kubwa kwangu kwamba wakati ninatembelea nchi hiyo ilikuwa ndiyo wiki ya uzinduzi wa mashindano hayo yanayozidi kupata umaarufu duniani baada ya kuanzishwa na FIFA mwaka 2000. Ni kwa vigezo hivyo hivyo vya miundombinu bora ya viwanja na sehemu za kufikia, Morocco ilichaguliwa kuwa mwenyeji wa mashindano hayo pia. Katika mechi ya uzinduzi wa michuano hiyo, timu ya Al-Ahly ya Misri ilimenyana na Aucland City FC ya New Zealand ambapo Afrika tuliweza kushinda. Mechi nyingine ambayo niliishuhudia ilikuwa ni kati ya wenyeji Wydad Casablanca na Al-Hilal ya Saudi Arabia. Kusema ukweli, wachambuzi walikuwa wametabiri kuwa mechi hii ingekuwa ngumu sana kutokana na ubabe wa timu zote mbili.

Wakiwa katika jezi yao nyekundu mithili ya wekundu wa msimbazi hapa Tanzania, Wydad waliingia kwa mikwara huku wakishangiliwa na uwanja uliojaa mashabiki na kupambwa kwa rangi za bendera ya Morocco. Mechi hizi za uzinduzi pia zilishuhudia wimbo rasmi wa FIFA ukikaribisha dunia Morocco kwenye michuano hii ukizinduliwa na kupigwa huku wamorocco wakiuimba kana kwamba ndio wimbo wa taifa lao. Ingawa Wydad ilikuwa ya kwanza kuliona lango la Wasaudia, kibao kiligeuka ghafla kwa Al-Hilal kusawazisha na kulazimisha kuongeza muda wa nyongeza ambapo wakati wa matuta, Wydad walitolewa katika michuano hiyo.

Ukiachana na FIFA, Shirikisho la Soka barani Afrikapia lina viwango vyake vya miundombinu ya soka ambavyo hutumia kuchagua wenyeji wa Michuano yake. Kwa upande wa AFCON, CAF imeweka bayana kuwa nchi inayoomba kuwa mwenyeji wa michuano ya 2025 lazima japo ikidhi kigezo cha viwanja vyenye viwango. Kwa mujibu wa CAF, nchi inayoweza kuchaguliwa kuandaa AFCON 2025 ni lazima iwe na viwanja bora, vya kisasa angalau sita. Kati ya hivyo, viwili lazima viwe na uwezo wa kuingiza angalau watazamaji 40,000 kila kimoja kwa wakati mmoja na viwili vingine japoviwe na uwezo wa watu 20,000 kilakimoja huku viwili vya mwisho viwe angalau na uwezo wa kuingiza watu 15,000 kila kimoja kwa wakati mmoja.

Kwa vigezo hiyo vya CAF, Morocco imekidhi na kupitiliza ikizingatiwa kuwa kituo cha michezo cha Mohammed V pekee kina viwanja vinne vyenye uwezo wa mahitaji ya CAF. Aidha, vipo viwanja katika miji yote mikubwa ya Nchi hiyo ambavyo uwezo wake unazidi mahitaji ya CAF. Kwa mfano, uwanja wa Ibn Batouta katika Jiji la Tangier pekee una uwezo wa kubeba watu 65,000.

Viwanja vingine vya Morocco vyenye uwezo unaohitajikana CAF na idadi ya watu vinavyoweza kubeba ni pamoja na: Prince Moulay Abdellah, Rabat (65,000); Marrakech (45,240); Hassan II, Agadir (45,000) na uwanja wa Mohammed, Casablanca ambao una uwezowa kuingiza watu 65,000 kwa wakati mmoja.

Kwa viwanja hivyo, na vingine vyenye uwezo wa watu 20,000 mpaka 30,000 ambavyo ni vingi, sina uhakika kama Morocco itapata mshindani wa kuwa mwenyeji wa michuano ya AFCON 2025. Kwa kuwa mimi si ofisa wa CAF, kinachobaki ni kusubiri na kuona uamuzi utakaotolewa na Shirikisho hilo la Soka barani Afrika. Kutokana na kutambua uzito wa ombi la Morocco baadhi ya Nchi zilizokuwa zimeomba kama Guinea tayari zimejiondoa katika kinyang’anyiro hicho.
Tusubiri tuone!

Deus Kibamba Ni mtafiti Na mchambuzi wa Masuala ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa. Pia, ni Mhadhiri wa Masuala ya Diplomasia na Sheria za Kimataifa katika Chuo Cha Diplomasia, Kurasini, Dar es Salaam. Anapatikana kwa nambari: +255 788 758 581 na barua pepe: dkibamba1@gmail.com
 
Umeacha kupigania Katiba mpya kupitia ile taasisi yako ya Jukwaa la Katiba! Umehamia kwenye kuipigia debe Morocco kupata nafasi ya kuandaa Afcon 2025!! Kweli njaa haina baunsa.
 
Back
Top Bottom