Dereva wa mwendo kasi'

Mwanahabari Huru

JF-Expert Member
Mar 9, 2015
14,243
34,903
Ikiwa ni asubuhi na mapema kabisa huku tukielekea elekea kuuaga mwaka dereva wetu anaanza kuiondoa gari taratibu kabisa kuelekea safari ya matumaini. Kwa kuwa si muda mrefu tangu gari yetu itoke garage, dereva wetu ilibidi aendeshe gari chini ya uangalizi mkubwa wa mafundi makenika kutoka ile garage ambapo gari yetu ilikuwa ikitengenezwa.

Hata hivyo kadri muda ulivyokuwa ukienda dereva alizidi kupata uzoefu na kutokuhitaji msaada tena. Basi tukawa tunaendelea na safari yetu iliyojaa kila aina ya vikwazo. Kwa kuwa gari yetu ilikaa garage kwa muda mrefu ni dhahiri kwamba uimara wake ulipotea na hivyo zilihitajika nguvu za ziada ili safari yetu izidi kuwa ya matumaini. Katika hilo dereva wetu alidai kuwa hatotuangusha badala yake atafanya kila litakalowezekana ili tufike salama. Kwa kipindi kirefu ambacho gari yetu ilikuwa garage tulisumbuliwa na njaa, tukachomwa na jua kali,kunyeshewa mvua, tulihisi kiu na adha mbali mbali. Hata hivyo tuliahidi kumpa ushirikiano wa kutosha dereva wetu wakati wote wa safari yetu.

Dereva alikuwa mwaminifu kweli kweli. Kila mara gari yetu ilipokuwa inayumba alitutia moyo akituahidi tutafika salama -tusiogope. Pale tulipohisi kiu hakusita kutupatia maji ya kunywa. Tulipohisi njaa alitupatia chakula. Abiria wengi tulimpenda kutokana na busara na maneno yake ya hekima. Tuiendelea na safari yetu tukiwa na matumaini makubwa kuwa tutafika salama huko tuendako. Hata hivyo baada ya safari ya muda mrefu, dereva wetu akatuambia amechoka na angependa amuachie mtu mwingine ashike usukani. Wengi hatukuwa tayari kuendeshwa na dereva mwingine lakini alizidi kutusisitiza kwamba anahitaji kupumzika. Tukawa hatuna budi kukubaliana na wazo hilo.

Dereva mwingine akashika usukani na tukazidi kuendelea na safari. Barabara kipindi cha dereva huyu wa pili ilikuwa nyembaba sana huku giza
nene likiwa limetanda mbele yetu. Ndani ya gari kulikuwa na joto jingi huku watu wenye magari makubwa wakitaka 'kutu-overtake'. Ndipo dereva akaamrisha milango na madirisha ya gari ifunguliwe. Kufunguliwa kwa milango na madirisha ya gari yetu kulitupa wasaa wa kuomba maji, chakula, madawa, mavazi, n.k kutoka kwa wale watu wenye magari makubwa. Hii pia ilitoa fursa kwa baadhi ya abiria kushuka ndani ya gari na kwenda kujitafutia kile ambacho walikihitaji kwa wakati ule. Ikumbukwe kuwa kipindi cha yule dereva wa kwanza milango na madirisha vilikuwa vimefungwa. Tulipata kila tulichokitaka tukiwa humo humo ndani ya gari kwa ya ruhusa ya dereva wetu.

Basi safari ikaendelea. Wale watu wenye magari makubwa wakawa wanatusogelea kwa ukaribu sana. Dereva wetu naye hakuwa mchoyo hata kidogo, akawaruhusu watu-overtake. Abiria nao nao tulipewa ruksa ya kufanya lolote lile ndani ya gari. Ukae, usimame, ulale kwenye siti vyote ilikuwa ruksa kwa abiria yoyote yule kufanya. Baada ya kutembea maili kadhaa akaona ni vema amuachie dereva mwingine. Abiria tukawa hatuna pingamizi lolote kuhusu uamuzi huo. Tulichokuwa tukiamini ni kufika salama huko tuendako.

Basi ndipo dereva wa tatu akaingia ndani ya gari. Tukaianza tena safari yetu.Ni dhahiri kwamba kila dereva alibeba tumaini jipya kwa abiria. Tofauti na dereva aliyetangulia ambaye aliruhusu milango na madirisha yote yafunguliwe, dereva huyu alijaribu kuifunga milango na madirisha japo hakubana sana ili hewa iingie ndani ya gari. Abiria walikuwa kimya sana kipindi cha dereva huyu. Mara nyingi hakutaka kusikia maelekezo kutoka kwa kila abiria zaidi ya otingo na wasaidizi wake wengine. Hata pale abiria walipotaka kupaza sauti zao juu ya mwenendo wa gari waliamriwa wanyamaze. Licha ya hayo yote lakini dereva alijitahidi ku-icontrol gari kwa kiasi chake. Tukaendelea na safari.

Utaratibu wa kupokezana vijiti mio goni mwa madereva wa gari hili ukawa umeshazoeleka. Kama walivyofanya madereva waliotangulia, baada ya hatua kadhaa za safari yetu ilibidi dereva huyu nae apumzike. Akaja dereva mwingine ambaye alikuwa ni wa NNE tangu tulipoianza safari yetu.

Dereva wa NNE alipokelewa kwa bashasha kubwa sana na abiria walio wengi. Abiria wengi walimfananisha na yule dereva wa kwanza. Dereva huyu alikuwa anaonekana mcheshi mwenye kutabasamu wakati wote wa safari. Tukaianza tena safari chini ya dereva wetu huyu mpya. Akawa ametuahidi vitu vingi vya kuvutia. Akatuhakikishia ya kwamba safari yetu itakuwa ni yenye furaha tele. Kadri safari yetu ilivyokuwa ikiendelea dereva akaanza kuiyumbisha tena gari yetu. Ghafla abiria wakaanza kuhisi tofauti na vile walivyokuwa wakiahidiwa. Mara wakaanza kupiga mayowe na kumuomba dereva awe makini. Dereva huyu hakujali. Aliendelea kuruhusu kelele za abiria huku safari ikiwa inaendelea. Ilifika mahala akawa anaipaki gari pembeni na kwenda kupiga stori na wale watu wenye magari makubwa huku abiria wake wakiwa wanahisi njaa na kiu ndani ya gari. Abiria wakaanza kumchukia sana dereva huyu wakitamani na yeye apumzike aje dereva mwingine. Kama kawaida safari ikaendelea na hatimaye dereva huyu akakamilisha hatua zake alizotakiwa atuendeshe. Abiria walifurahi sana kuona dereva huyu anapumzika.

Haya sasa! ndani ya gari dereva mwingine akaushika usukani. Kama ilivyokawaida kwa abiria wa gari hili kushangilia na kujenga imani kubwa kwa kila dereva anayeingia, dereva huyu mpya nae akapokelewa kwa nderemo na vifijo vingi.

Wakati huu tumeshatoka uchochoroni tupo mjini ambapo barabara ni pana na magari ni mengi. Tunaianza tena safari yetu tukiwa na dereva wetu mpya aliyepachikwa jina la "DEREVA WA MWENDO KASI". Jina hili alipewa na abiria wakiamini ataliendesha gari kwa spidi kali itakayofanya tufike haraka huko tuendako. Abiria wengi wakafikiria kwamba tulichelewa kufika kutokana na spidi ndogo ya madereva waliotangulia.

Tunaendelea kukatiza mitaa mbali mbali. Kwa kuwa sasa tupo mjini, bara bara imepambwa kwa taa na alama mbali mbali zinazomuelekeza dereva kuendesha gari kwa usalama ili asije akasababisha ajali.

Hata hivyo dereva huyu hataki kuziangalia na kuzizingatia alama hizi za usalama bara barani. Hata pale abiria wanapomshauri awe makini katika uendeshaji wake hataki kuwasikia. Mara nyingine abiria wanaoonekana kuleta usumbufu hutolewa ndani ya gari na kuachwa wakiwa wanaranda randa mitaani. Dereva anajiamini sana. Hataki ushauri wa mtu yoyote iwe otingo ama abiria. Hata zile alama za usalama barabarani ambazo ndio muongozo halisi juu ya matumizi bora na salama ya barabara hataki kuzifuata. Anachoamini yeye ni kuongeza spidi ya gari ili tuweze kufika mapema huko tuendako. Baadhi ya abiria wanafurahia na kusema huyu ndiye dereva waliyekuwa wakimsubiria kwa muda mrefu. Hata hivyo abiria walio wengi wameanza kuwa na hofu juu ya mwenendo wa dereva huyu. Wengi wameshaanza kuwa na hofu juu ya safari hii. Ni kweli tunataka kufika mapema ila siyo kwa spidi hii. Spidi ya kutokuzingatia alama za barabarani.

Ghafla, dereva anaanza kusababisha ajali ya kwanza na kujeruhi abiria kadhaa. Hofu miongoni mwa abiria inazidi kutanda. "Tutafika salama kweli?" baadhi ya abiria wanaanza kujiuliza? Wengine wanaanza kujutia na kutamani bora hata angeendelea yule dereva aliyetangulia. Wanazidi kupiga kelele lakini 'dereva wa mwendo kasi' yeye hajali. Lengo lake kubwa ni kuhakikisha tunafika mapema mwisho wa safari yetu.

Safari inaendelea. Ghafla hapa na pale gari inapata pancha, mara tukienda mbele kidogo tunaambiwa gia ina matatizo. Dereva wa mwendokasi.....dereva wa mwendo kasi. Baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa dereva huyu baadhi ya mafundi makenika kutoka katika karakana maarufu hapa mjini wamegoma kututengenezea gari letu. Sasa safari yetu imejaa hofu tupu. Hatuna uhakika wa kufika salama huko tuendako.....dereva wa mwendo kasi kajitia ukiziwi. Hataki kuambiwa akasikia....hataki kukosolewa akajirekebisha. Bado safari ni ndefu.....Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujaalie tufike salama!

Mwanahabari Huru
 
Mimi..
Namshauri Suka wa Mwendo Kasii azidi kutupia Gia..
Hizi alama za Barabarani nying zimefutika nyingine zilisha gongwa..

Mtaani tunasemaga ''Suka Lisimamiee Hatujaonaa badoo''
 
Hawa ndio waandishi wa habari wa enzi za mwendo kasi. Wamekuzwa kwenye jamii ambayo inatumia saa tisa za siku moja katika kusikiliza na kuamini uongo halafu inatumia saa tatu zinazobaki kabla jua halijazama katika kusikiliza habari zenye ukweli.

Very poor journalism ambayo ni kielelezo cha elimu kuachwa ikajiendea tu na kuzalisha watu wasio na uwezo wa kujenga hoja na kuitetea nchi yao pale wanapotakiwa kufanya hivyo.
 
Upo vizuri sana katika lugha ya picha

Haya tuanaendelea na dereva wa mwendo kasi, wengi wameshashushwa njiani na wengine kujeruhiwa

Tuombe Mungu tufike salama
 
Hawa ndio waandishi wa habari wa enzi za mwendo kasi. Wamekuzwa kwenye jamii ambayo inatumia saa tisa za siku moja katika kusikiliza na kuamini uongo halafu inatumia saa tatu zinazobaki kabla jua halijazama katika kusikiliza habari zenye ukweli.

Very poor journalism ambayo ni kielelezo cha elimu kuachwa ikajiendea tu na kuzalisha watu wasio na uwezo wa kujenga hoja na kuitetea nchi yao pale wanapotakiwa kufanya hivyo.
Tupo kwenye Hoja ya dereva wa Mwendokasi
 
Back
Top Bottom