Mwalimu Nyerere aliwahi kutamka hadharani bila kufinya maneno kuwa serikali ya CCM inanuka wakati ana zungumzia Tanzania na hatima ya uongozi.Ni kweli mwalimu aliona mbali sana na alikuwa na kipaji cha kuitwa mwalimu kutokana na maono yake.
Ukisikiliza hotuba za mwalimu Nyerere utagundua kuna kitu zaidi ya uzalendo ndani ya moyo wake.Miongoni mwa matamko yake,aliwahi kusema"ukiweza kumwambia mkeo kwa ukali kuwa,Ikulu ni mahali pa takatifu,basi hata marafiki zako watakuogopa na kukuheshimu"mwisho wa kunukuu.
Maneno haya ya mwalimu leo hii yamegeuka shubiri ndani ya CCM,kutokana tu na kuacha yale mwalimu aliyaona yana athari kubwa kwa mustakabali wa chama na nchi.Leo hii mwalimu akijaliwa akafufuka na kukuta uozo aliokuwa akionya na sasa ndiyo umeshika kasi nadhani angekufa mara ya pili kwa uchungu.
CCM ya leo si CCM ya mwalimu.Maadili,madhumuni,miiko na misingi ya chama imetupwa mbali na kuachia usisi,umimi na undugunazion umetawala.Leo hii maskini gani anayeweza kusimama kugombea nafasi ya uongozi ndani ya chama akapita.Hata wale wanaopita bila kupingwa katika chaguzi za ndani ya chama ni matajiri wakubwa.Toka lini ukasikia mkulima wa Chakware,Tanganyika masagati,ipililo na masanwa wamepitishwa bila kupingwa.Hali hii ndo iliyopelekea CCM kukimbiwa na umati mkubwa kujiunga na upinzani wakitafuta pambazuko jipya.
Ukiangalia majina ya wajumbe waliochaguliwa utagundua kuwa chama hiki si cha wakulima na wafanyakazi kama walivyoaminishwa wananchi zama hizo.Leo kuna watu kama Dickson Membe,Fred Lowasa.Ashura Hussein Mwinyi,Ridhiwani Kikwete,Beny Samwel,Debora Mwandosiya,Irene Pinda,Felister Ndugai,Christopher Ndejembi,,Sharifa Bilal,Hawa Kigoda,Judith Mukama na Jarome Msekwa.Majina haya na mengineyo mengi unafikiri yana ashiri nini katika mustakabali wa amani na udugu aliotuachia mwalimu.
Majina kama haya ndiyo yalisababisha wananchi wa Libya kutokuwa na imani na Gadaffi hata kama aliwajali kwa kila kitu.Wananchi waliamini Hayati Gaddaffi alijali sana watu wa familia yake na kuwapa upendeleo kuliko wananchi wengine wowote.
Cha msingi katika mada hii ni jinsi ya kukifanya chama hiki kuwa na malengo ya kifamilia zaidi kuliko matakwa na madhumuni ya waasisi wake.Kwa staili hii kutokana na matokeoya chaguzi za ndani ya chama nina uhakika uchaguzi huu utaibua makundi zaidi ya yaliyokuwemo kwasababu chama sasa kinaendeshwa kama vanguard party(wateule wachache).
Hata falsafa ya kujivua gamba nayo imewekwa pembeni na watu kujikita zaidi na uchaguzi wa 2015 kuliko kuangalia matatizo ya wapiga kura kama walivyo ahidi kwenye manifesto yao.Watuhumiwa wa ufisadi nao wamerudi kwa kishindo kiasi cha kuwadondosha wapinga ufisadi,hali ni tete kila mmoja ana jaribu kuweka vision ndani ya chama kwa kigezo cha kuisaidia CCM kushinda 2015,kwa nguvu zaidi ya pesa,ubabe zaidi ikibidi na uwizi zaidi.
Wako wapi wadhamini wa chama kina Peter Kisumo na wenzake,wamegubikwa na nini kiasi cha kushindwa kukemea yanayotokea.Chama kimekosa dira na mwelekeo,yaliyosemwa na marehemu Horace Kolimba leo yamejitokeza hadharani.Imekuwa ni kawaida sasa kumsakama anaye kosoa kuliko kuyafanyia kazi yale aliyoyalalamikia.Kwa mtazamo wangu mzimu wa Horace Kolimba utaendelea kukitafuna chama badala ya kuangalia nini walichokosea kiasi cha mtendaji mkuu wa chama kwa wakati kufikia kutoa tamko hilo.
Mwisho,wanachama madhubuti walio ndani ya chama hawatatishwa na kuzibwa midomo yao kukemea maovu kwa kunyima au kukatwa majina yao makusudi.Cha msingi mkiona hali inazidi kuwa tete na chama mnakipenda fanyeni harakati za makusudi kufanya mapinduzi ya kukiimarisha chama kwa kukemea kila uozo ndani ya vikao na hata nje ya vikao.Dhamira ya kweli tu ndiyo silaha madhubuti kuelekea njia bora ya kukinusuru chama.Angalieni yaliyoisibu KANU na maprofesa wa siasa kwa vyama vikongwe visivyotaka kutazama wakati na matarajio ya wakati husika.