Dar: Zaidi ya nyumba 100 zatitia

figganigga

JF-Expert Member
Oct 17, 2010
25,492
54,890
Zaidi ya nyumba 100 zatitia Dar
ZAIDI ya nyumba 100 zilizoko katika bonde la Kingugi kata ya Kilungule Manispaa ya Temeke, jijini Dar es Salaam, zimebomolewa na maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na kusababisha kukosa makazi na mali zao kupotea.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliwatembelea na kuwapa pole wananchi hao huku akiwataka wahame kwenye maeneo hayo kwasababu wanaishi maeneo hatarishi.

Alisema wananchi hao wanalazimika kujipanga kwenda kuishi maeneo salama kwa kuwa kila mwaka wanakumbushwa kuhama maeneo kama hayo kwa usalama wao.

"Rai imekuwa ikitolewa na viongozi waliopita, lakini kunakuwa na sababu mbili ya watu kutotii rai ikiwa ni pamoja na uduni wa kipato na uwekaji wa vipaumbele, rai ikitolewa kwamba muondoke hakikisheni mnahama," alisema.

Makonda alisema maeneo mengi wanayoishi wakazi hao ni hatarishi kwasababu asilimia 60 ni bahari kama ilivyo Zanzibar ambayo wataalamu wanasema asilimia kubwa ni bahari.

Aidha, Makonda alisema kuna changamoto kwa wakazi wa Dar es Salaam kuweka makazi ya kudumu kwasababu baadhi ya nyumba zinadondoka na kusababisha athari kubwa kwa maisha yao na kurudisha nyuma maendeleo yao.

"Niwe mkweli sina fungu la kuwapa hivyo lazima Mkoa tutafute majibu ya kudumu mvua zikiisha tufanye mkutano tuangalie tunafanyaje tufike mahala tuweke mkakati wa kudumu tusipoteze maisha kwa kuangukiwa na nyumba kama ilivyotokea hapa," alisema.

“Kama kuna kitu hamjakielewa kwetu viongozi njoo tukubaliane tupate maelezo ili tuweze kujenga nyumba za bei nafuu zilizo salama, naamini kati yenu hakuna mtu maskini," alisema.

"Tuchukue hatua najua hakuna wa kuhukumiwa kati yenu kama kuna mahala kuna maeneo makubwa yametwaliwa na serikali inaweza kuyafuta na itafanya hivyo ili mpate makazi bora," alisema.

Aidha, Makonda alisema baadhi ya watu hurejea katika maeneo hayo yanapokauka na kujenga tena jambo ambalo linaashiria kwamba hakuna mwananchi maskini.

Aliwataka wapangaji kukataa kupanga maeneo ya mabondeni kwasababu ni hatari kwa maisha yao.

“Ombi langu kwa wapangaji ni kwamba hakuna sababu ya kupanga kwenye nyumba zilizojengwa kwenye maeneo hatarishi, diwani hana fedha za kukujengea nyumba hakuna mtu atakayewajengea wasiwadanganye," alisema.

Aliongeza kuwa nyumba 200 haziko katika hali salama na kuwataka wananchi kwenda kujihifadhi sehemu nyingine ili wataalam wapime maji yaliyopo ardhini ili kuepusha maafa zaidi.

Chanzo: Nipashe
 
Back
Top Bottom