Dar: NGO's zamtwisha Chalamila mzigo wa changamoto za kikodi

Nyakijooga

Senior Member
Dec 9, 2018
123
202
Kufuatia baadhi ya malalamiko mbalimbali kutoka kwa wadau wa mashirika yasiyo ya kiserikali Mkoa wa Dar es salaam kuhusu changamoto za kikodi wanszodai kukumbana nazo, Msajili wa mashirika hayo (NGO's), Vicky Mayao, amewataka kuwa na kamati maalum itakayohusika na kukusanya malalamiko yao ya kikodi kwa ajili ya kuyafikisha kwenye Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili yatafutiwe ufumbuzi.

Vicky Mayao ameyaeleza hayo wakati akizungumza katika Jukwaa la Mashirika yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Dar es salaam ambalo linafanyika kwa siku mbili kuanzia leo 28 na 29 Julai 2023, katika ukumbi wa maktaba kuu chuo kikuu Dar es Salaam.

Ambapo amesema kuwa kupitia kamati ndogo inayotokana na wadau hao intakiwa kuendelea na mchakato wa mazungumzo. Akidai kuwa njia hiyo inaweza kuleta suluhu kwa baadhi ya changamoto ambazo zinalalamikiwa.

"Kuna kamati ndogo ya kikodi ilianzishwa, nasema warudi mezani sababu sheria za kodi zipo hatuwezi kuzibadilisha hapa, hata tunavyomtaka kamishna hawezi kuja hapa natamani turudi kwenye kamati ya Majadiliano," amesema Mayao

Kwa upande wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACONGO) kupitia mwakilishi wake Mkoa wa Dar es Salaam, Jane Magigita baadhi ya NGO zilianzisha mchakato wa Majadiliano na TRA kuona namna ambavyo sheria za Kodi zinapaswa kuangaliwa upya na kuweka mazingira rafiki kwa mashirika kufanya kazi kwa ufanisi

Pia amewasilisha maombi manne kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Albert Chalamila, ikiwemo kuiomba Ofisi yake kuona umuhimu wa kutenga fedha kwa ajili ya kuwezesha utendaji wa baraza hilo, sambamba na kupitia ofisi yake kuchochea marekebisho ya sheria Kodi inayotekelezwa kwa sasa na wadau hao.

"Ombi letu kwa Ofisi yako kuchochea marekebisho ya sheria za Kodi kama ilivyofanya kwa wafanyabiashara na sasa kumetulia. Pia, kutenga Bajeti Maalum Kila mwaka itakayosaidia kuwezesha NACONGO ngazi ya Wilaya na mkoa, pamoja na Ofisi ya mwakilishi wa Baraza Mkoa" amesema Jane Magigita

Aidha kwa upande wa Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu, Wakili Onesmo Olengurumwa amesema kuwa kumekuwepo na changamoto ya TRA kutoza kodi kwenye vyanzo vya kifedha ambavyo hivitakiwi kutozwa, akitolea mfano 'mchango wa matembezi ya hiari'

"Kuna changamoto ya fedha zinazopatikana kupitia mchango wa matembezi ya hiari kutozwa Kodi, fedha za matembezi ya hiari ni mchango kama ruzuku nyingine wala hairuhusiwi kutozwa kodi" amesema Onesmo Olengurumwa.

Hata hivyo Olengurumwa amewasilisha ombi juu la NGO,s kupewa msamaha wa jumla, "Tunaomba tupate msamaha wa riba na faini, naomba TRA hili likafanyiwe kazi"

Ombi hilo amelitoa ikiwa ni kufuatia kuwepo kwa baadhi ya mashirika nchini ambayo yanatajwa kukumbana na changamoto kwenye maeneo ambayo ameyabainisha, hali ambayo imepelekea baadhi ya mashirika kukosa sifa za kuendelea kutambuliwa rasmi.

Kufuatia hoja hizo, madai pamoja na mapendekezo Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Albert Chalamila ameshauri hoja hizo kuwasilishwa kwa njia ya nyaraka ili waweze kushirikiana na mamlaka nyingine ikiwemo TRA na Bunge katika kuleta suluhu ya masuala mbalimbali ambayo yamewasilishwa.

Lakini amewahasa wadau hao kuendelea kuwa waadilifu na kuzingatia maadili pindi wanapotekeleza majukumu yao huku akiahidi kuwa balozi katika mchakato wa mabadiliko unaolenga kuleta suluhu kwa baadhi ya changamoto ambazo zimetajwa na wadau.

Jukwa hilo limeandaliwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NACONGO) Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo imefanyika mjadala mabalimbali hususani iliyogusia masuala ya kikodi, sheria ya Kuzuia utakatishaji fedha na ufadhili wa ugaidi. Ambapo kwa siku ya kesho mjadala unatarajiwa kujikita kuangazia mwelekeo wa mashirika yasiyo ya kiserikali na jinsi yanavyoweza kukabiliana na changamoto za uendelevu zilizopo na zijazo, sio tu katika ngazi ya kitaifa, bali pia kimataifa.
 
Back
Top Bottom