CUF zaidi kukamatwa

Indume Yene

Platinum Member
Mar 17, 2008
2,959
719
na Waandishi Wetu.
MD




KUKWAMA kwa mazungumzo ya kusaka suluhu ya mpasuko wa kisiasa Zanzibar, na matukio ya hivi karibuni yaliyohusisha kukamatwa kwa watu kadhaa wakazi wa Pemba wakihusishwa na uhaini, yamezidi kuleta msukosuko wa kisiasa nchini.

Katika mwendelezo wa matukio hayo, Chama Cha Wananchi (CUF) kimejikuta katikati ya lawama, kikituhumiwa kuhusika na watu hao ambao waliachiwa jana, huku kwa upande mwingine, kikituhumiwa kuchochea vurugu visiwani Zanzibar kwa sababu za kisiasa.

Matukio kadhaa yaliyotokea jana, yaliyafanya masuala hayo kuchukua sura mpya, na kuonyesha kuwa mwisho wake haupo karibu.

Kutoka Zanzibar, Saada Said anaripoti kuwa, hatimaye watu saba waliokuwa mikononi mwa polisi kutokana na kitendo chao cha kupeleka barua Umoja wa Mataifa kutaka kuundwa kwa serikali ya shirikisho, waliachiwa huru jana na kusafirishwa hadi makwao kisiwani Pemba.

Watu hao walikamatwa usiku wa kuamkia Mei 12, mwaka huu na maofisa wa usalama, na kuchukuliwa hadi Unguja walikoshikiliwa katika vituo kadhaa vya polisi kwa mahojiano.

Kamishna wa Polisi Zanzibar, Khamis Mohammed Simba, alithibitisha kuachiwa watu hao na kusema wameridhika na uchunguzi walioufanya.

Alisema baada ya kukamilisha uchunguzi wa awali, wameamua kuwaachia kwa dhamana watuhumiwa hao, huku Jeshi la Polisi likiendelea kuwasaka watu wengine, kwa tuhuma za kuhusika na suala hilo.

Alisema sambamba na kuwaachia huru, pia Jeshi la Polisi litagharamia safari za watu wote saba hadi nyumbani Pemba.

Kamishna Simba alisema taarifa za kutokea tukio la kutaka kujitenga kwa wananchi wa kisiwani Pemba, ziliandikwa kupitia vyombo vya habari, na tangu hapo walianza kufuatilia taarifa hizo kwa umakini kwa kuzingatia suala hilo linajumuisha masuala ya usalama katika nchi.

“Jeshi la Polisi lilishtushwa sana kusikia jambo geni ambalo hapa kwetu halijawahi kutokea kabisa,” alisema.

Akielezea zaidi alisema, jambo lolote linalotendeka Zanzibar linaweza kuathiri Tanganyika kwa kuwa nchi ya Zanzibar na Tanganyika ziliungana na kuifanya Tanzania, hivyo Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa maslahi ya Tanzania.

Hata hivyo, Kamishna Simba hakuwa tayari kuelezea kile kinachotendeka kutokana na utaratibu wa kazi zao, kwa kuwa kueleza mambo kunaweza kuhatarisha upelelezi na mambo yanayofuatiliwa na jeshi hilo.

Alisema kwa kuwa suala hilo ni kubwa na upelelezi wake unahitaji umakini, wataficha taarifa hizo hadi uchunguzi utakapokamilika, kwani wapo baadhi ya watu waliokuwa wamekamatwa, lakini hawahusiki na tuhuma hizo, na pia wapo wengine ambao hawajakamatwa ambao wanahusika.

Kamishna Simba alisema watu wote watakaopatikana na hatia watashitakiwa chini ya sheria ya makosa ya jinai kwa kutaka kuunda Jamhuri ya Kisiwa cha Pemba na kujitenga na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, jambo ambalo ni makosa kwa mujibu wa sheria za nchi.

Ingawa Kamishna Simba hakutaka kusema watu hao watashitakiwa katika mahakama gani, aligusia kwamba upelelezi utakapokamilika na polisi kuridhishwa na ushahidi walioupata kutoka kwa watu hao, watalifikisha suala hilo mahakamani ili watuhumiwa hao wajibu mashtaka chini ya sheria za makosa ya jinai.

“Bado ni mapema kujua watashitakiwa katika mahakama gani kama ya Dar es Salaam au hapa Zanzibar… bado tunakusanya ushaidi,” alisema.

Hata hivyo, waandishi wa habari hawakupewa fursa ya kuonana au kuzungumza na watu hao walioachiwa.

Awali, habari za kuachiwa kwa watu hao, zilitangazwa jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, katika mkutano wake na waandishi wa habari.

George Maziku na Elihuruma Kaguo wanaripoti kuwa, katika mkutano huo, Mwema alisema kuwa kuna uwezekano watu wengine wakakamatwa kuhusu sakata hilo.

Alisema wanaowindwa sasa ni wale ambao walitajwa na watu walioachiwa jana, wakati wa mahojiano na polisi.

Kwa upande mwingine, Mwema aliihusisha CUF na harakati za wananchi hao wa Kisiwa cha Pemba kutaka kujitenga.

Alisema upelelezi uliofanywa na jeshi lake umebaini kuwa wahusika wote wa harakati za kutaka Pemba ijitenge ni wafuasi wa CUF, na kwamba harakati hizo zimechochewa zaidi na uamuzi wa hivi karibuni wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwamba suala la kuundwa kwa serikali ya mseto Zanzibar liamuliwe na wananchi kwa kura ya maoni.

Alibainisha kuwa kitendo cha wananchi wa Pemba kutaka kujitenga kutoka Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, ni uvunjaji wa katiba na sheria za nchi, na kwamba hiyo ndiyo sababu ya msingi ya jeshi lake kuwakamata baadhi ya wananchi kisiwani humo, kwa kuwa kazi ya jeshi lake ni kulinda katiba na sheria za nchi.

Alisema kwamba jeshi lake litawaachia kwa dhamana watuhumiwa saba waliokuwa wanashikiliwa na jeshi hilo baada ya kukamilisha kuwahoji na kupata ushahidi wa kutosha ambao utawezesha kukamatwa kwa watuhumiwa wengine muhimu.

“Maofisa wa upelelezi wa makao makuu kwa kushirikiana na wenzao wa Zanzibar wamekamilisha kuwahoji wale watuhumiwa saba tuliokuwa tukiwashikilia, hivyo kwa sasa tutawaachia kwa dhamana, lakini tutawakamata watuhumiwa wengine waliotajwa kwa mahojiano zaidi,” alisema Mwema.

Katika hali ya kushangaza na kutia shaka uwezo na umakini wa utendaji kazi wa Jeshi la Polisi nchini, Mwema alikiri kuwa jeshi lake halijajua kosa wanalotuhumiwa kutenda watu hao saba, na kwamba litajulikana baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka ya Umma nchini (DPP) kuchambua ushahidi wa polisi na kuamuru watuhumiwa wapelekwe mahakamani.

Akijibu swali la mwandishi aliyetaka kujua kama ule ulikuwa ukamataji wa watuhumiwa kisheria au utekaji nyara, kutokana na kuwepo taarifa kuwa ulifanyika usiku wa manane, huku watuhumiwa wakifichwa mahali kusikojulikana kwa zaidi ya saa 24 zinazoruhusiwa kisheria, Kamanda Mwema alisema Jeshi la Polisi lina utaratibu na sheria zake katika kukamata watuhumiwa na kuwahoji.

Aidha, alishindwa kueleza lengo la polisi kuwahoji watuhumiwa hao saba juu ya ufuasi wao wa kisiasa, huku akikana wasiwasi wa baadhi ya waandishi kuwa jeshi lake linatumiwa na watawala kupambana na chama cha CUF.

“Si nia ya Jeshi la Polisi kujiingiza kwenye malumbano ya kisiasa yanayoendelea hapa nchini, na wala hayo siyo majukumu yake. Hata hivyo, malumbano yoyote ya kisiasa yanatakiwa yawe ya kistaarabu, ya kuvumiliana, ya kupingana bila kupigana na yasiyo na mwelekeo wa kuchochea vurugu au uvunjaji wa amani,” alisema Mwema.

Watu hao saba walikuwa miongoni mwa 12 kutoka Kisiwa cha Pemba, waliowasilisha barua yao hivi karibuni kwenye ofisi za UNDP jijini Dar es Salaam, wakitaka Umoja wa Mataifa kuishinikiza Serikali ya Tanzania kukipa uhuru Kisiwa cha Pemba.

Kitendo hicho kilielezewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Mkamu wa Rais (Muungano), Muhammed Seif Khatib, kuwa ni uhaini dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakati huo huo, Salehe Mohamed anaripoti kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesisitiza kuwa CUF imeamua kutumia hali ya mambo visiwani Zanzibar hivi sasa ili kuchochea vurugu.

Kauli hiyo ya CCM ilitolewa jana Dar es Salaam na Kaimu Mkuu wa kitengo cha Propaganda Idara ya Itikadi na Uenezi, Tambwe Hiza, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu matamshi ya viongozi wa CUF juu ya mazungumzo ya muafaka, na kauli za kashfa wanazozitoa kwa viongozi wa CCM.

Alisema CUF, imekosa mwelekeo wa kisiasa visiwani Zanzibar baada ya kushindwa kuingia serikalini, hivyo inatafuta ajenda ambayo itawafanya wasikike katika masikio ya jamii, ndiyo maana wameamua kudai kuwa kuna machafuko au yatakuja katika visiwa hivyo.

Aidha, Hiza alisema chama hicho kimekuwa kikiwashinikiza wanachama wake kujitenga, kuandaa mazingira ya kuanzisha vurugu Zanzibar, kutupa vikaratasi vya uchochezi vyenye lengo la kuishinikiza serikali kukubaliana na matakwa yao.

Alisema mazunguzo ya muafaka yanatokana na vyama vya siasa, na hivyo kupanga kuanzisha machafuko kwa kutumia kisingizio cha wananchi si jambo la busara.

Hiza alisema tatizo kubwa lililopo hivi sasa ni CUF kukataliwa kuhusishwa kwenye serikali, hivyo kuamua kutoa kauli za uchochezi za kutaka kuleta machafuko nchini bila sababu yoyote.

Alisema CUF walikuwa wakiomba angalau wachaguliwe mawaziri wawili au watatu kutoka chama chao kabla ya kuelekea katika uchaguzi ujao, lakini ombi hilo lilikataliwa na Rais Aman Karume kwa madai ya kufanywa hivyo ni kinyume cha katiba.



Natumaini jeshi la Polisi litafanya kazi yake kwa mujibu wa sheria na wasije waakanza kuendeshwa kwa hisia za kisiasa na wakaja na staili kama zile za Salmin Amour. Polisi kuweni makini sana, msiingize siasa katika utendaji wenu na hili balaa likaanza kuenea kote maana mnajua nguvu ya wananchi wakiamua kusimamia jambo. Na always wananchi hushinda wakiamua hivyo.
 
Hii ni jinsi gani serikali ya awamu ya nne,imeprove failur.Kuwakamata wapemba si suluhu,ya wao kutaka kujitenga,bali ni kuongeza tatio juu ya tatizo.Busara na hekima ndio mda mwafaka kwa viongozi kuonyesha,na sio kutumia nguvu for nothing
 
This case has no merit. Walichofanya hawa jamaa ni cha busara sana kwenda UN kuomba wasikilizwe katika petition yao ya kutaka kuwa na jamhuri yao.

Hakuna uhaini kwenda UN kwa kudai uhuru wa haki zako. Kama ni uhaini, basi ile safari ya Nyerere kwenda kudai Uhuru UN ilikuwa batili na ya kihaini!

CCM na Serikali yake wameendekeza dhuluma, unafiki na ulaghai kwa muda mrefu na hili suala la muafaka litawatokea puani na kuwaangamiza kuliko hata Ufisadi.
 
Nimechoka na taarifa za wapemba na waunguja
Namshauri JK aruhusu visiwa vyote hivi viwili vijitenge hata kesho ikiwezekana.
Hakuna chochote tunachopata toka kwao,zaidi ya kero za kisiasa zisizoisha,kumbe wenzetu wana agenda zao nyuma ya pazia.
Natamani kuiona Tanganyika mpya na yenye maendeleo soon.
 
Back
Top Bottom