Wanachama 1,328 waikimbia CUF
Baadhi ya viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, wakiangalia kadi za chama hicho zilizorudishwa na wanachama eneo la Mbagala Zakhem wilayani humo jana.(PICHA: MOSHI LUSONZO)
Chama cha Wananchi (CUF) kimepata pigo baada ya wanachama wanaodaiwa kufikia 1,328 wakiwemo viongozi wakuu wa wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam kujivua uanachama na kurudisha kadi zao.
Tukio la kurudisha kadi hizo lilitokea eneo la Mbagala Zakhem jana, ambako wanachama hao wakiongozwa na Mkurugenzi wa Haki za Binadamu Wilaya ya Temeke, Salum Sudi, walieleza kuwa wako mbioni kujinga na chama kipya cha Alliance for Democracy Change (ADC) kinachodaiwa kuwa kiongozi wake ni Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed.
Pamoja na kadi hizo, vitu vingine vilivyokabidhiwa mbele ya Mhamasishaji Mkuu wa CUF Mkoa wa Tanga, Salim Dayadaya, ni pamoja na bendera na fulana.
Akitoa tamko la kuondoka kwenye chama hicho, Sudi, alisema kwa awamu hiyo ya kwanza viongozi pekee walioungana na wanachama hao kurudisha kadi ni 12 wa ngazi mbalimbali wa wilaya ya Temeke.
Alisema uamuzi wa kujitoa kwenye chama hicho umechukuliwa baada ya kugundua kuwa kuna ukweli katika hoja za Hamad kwamba CUF inaongozwa katika misingi ya usultani na upendeleo.
Alidai kuwa kabla kuamua kurudisha kadi, walikuwa watiifu kwa kukitumikia chama hicho, lakini walibaini ukweli huo baada ya kuona mambo mbalimbali hayaendeshwi sawa.
Sudi alisema Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, anaendesha chama hicho kifalme pamoja na kufanya upendeleo wa wazi kwa upande wa Zanzibar, jambo ambalo limewafanya uvumilivu wao ufikie kikomo.
Maalim Seif alijitengea kiasi kikubwa cha pesa katika Uchaguzi Mkuu upande wa Zanzibar, lakini upande wa Bara alitenga pesa ndogo sana wakati kijografia Tanzania Bara ndio ilitakiwa kuwa na bajeti kubwa kutokana na eneo lake, alisema Sudi.
Alisema kuwa hata mawakala wa chama hicho upande wa Zanzibar walipewa posho ya Sh. 15,000 wakati wa Tanzania Bara walipewa Sh. 4,000 na wengine hawakulipwa kabisa.
Kwa msingi huo, tumeamini hoja ya Hamad kuwa chama hiki kinafanya kazi kwa upendeleo, tunamuunga mkono na tunamuahidi kuwa nyuma yake ndani ya chama kipya, alisema.
Habari zinasema kuwa ADC kipo mbioni kupatiwa usajili wa muda wiki ijayo.
Alipoulizwa Hamad juu ya kuondoka kwa wanachama wa CUF, alisema kuna kila dalili muda wa kufa kwa CUF umewadia kuanzia Zanzibar hadi Tanzania Bara.
Alisema wanachama waliojiengua wilayani Temeke ni kama mvua za rashasha tu na kukifananisha chama hicho sawa na kioo kilichopasuka kinachohitaji kuondolewa.
Mimi sishangai jambo hilo, nimeeleza toka zamani kuwa CUF imekufa kuanzia Zanzibar hadi huku Bara, hakitakiwi na watu kutokana na uongozi wao mbaya, alisema Hamad.
Aliongeza: Hata Mwalimu Julius Nyerere alisema kioo kikiingia vumbi huwa kinafutwa, lakini kikipasuka kinaondolewa, muda wa kuiaga CUF umefika.
Hata hivyo, alikanusha taarifa ya kuanzisha chama kipya cha siasa kwa kueleza kuwa hawezi kufanya kitu kama hicho kwa sababu anaheshimu maamuzi ya mahakama kwa kuwa shauri lake la kupinga kufukuzwa kwenye chama hicho bado linaendelea.
Aliongeza kuwa amewahi kusikia kuwa wanachama wenzake wameanzisha chama hicho, lakini hajawahi kwenda wala kuomba uanachama.
Alipotafutwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara, Julius Mtatiro, kutoa ufafanuzi kuhusiana na kuondoka kwa wanachama hao, hakupatikana kutokana na simu yake ya mkononi kuzimwa.
Hamad alitimuliwa katika chama hicho mwishoni mwa mwaka jana kwa madai kuwa anachochea mgogoro, lakini alifungua kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dar es Salaam kupinga maamuzi hayo, anayodai kuwa yalikiuka amri ya mahakama. Bado anaendelea na ubunge wake.
CHANZO: NIPASHE