CUF ya Maalim wachangishana ili kujiendesha

Replica

JF-Expert Member
Aug 28, 2017
1,447
7,832
WAKATI mashauri nane yanayokihusu chama chao yakitarajiwa kunguruma mahakamani ndani wiki mbili kuanzia kesho, Chama cha Wananchi (CUF) upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharrif Hamad umeanza kuchangishana fedha ili kujiendesha.

MAALIM%20SEIF.JPG

Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharrif Hamad.​

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma wa CUF Taifa, Salim Bimani, ilielezwa kuwa Kamati ya Uratibu wa Shughuli za Chama Mkoa wa Dar es Salaam imemteua Rashid Abdallah, Mwenyekiti wa Matawi ya Mkoa wa Dar es Salaam, pamoja na wajumbe wenzake wa kamati ya fedha kukusanya michango hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Abdallah na wenzake wanatakiwa kuwafikia watu wote watakaokuwa tayari kushirikiana na chama hicho katika hatua ambayo ilielezwa kuwa ya kukirejesha chama katika mstari wake.

"Michango hiyo imewekewa utaratibu na udhibiti makhsusi wa kuihifadhi na matumizi yake. Tunachukua fursa hii kuwashukuru wale wote ambao wamekuwa mstari wa mbele kutoa michango yao katika kipindi hiki cha mpito kuelekea ushindi, uimara zaidi na mafanikio makubwa kwa taasisi ya CUF," sehemu ya taarifa hiyo ilieleza.

Taarifa hiyo pia ilibainisha kuwa chama hicho kitakuwa na mashauri manane mahakamani yatayosikilizwa ndani ya siku 15 kuanzia kesho.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kesho kutakuwa na shauri la msingi namba 143/2017 linalowahusu wabunge wanane na madiwani wawili dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Bunge, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Halmashauri za Ubungo na Temeke na Prof. Lipumba na wenzake wanane ambalo litapangiwa utaratibu wa kusikilizwalikiwa chini ya Jaji Mwandambo.

Taariaf hiyo pia ilieleza kuwa Oktoba 25 kutakuwa na shauri dogo namba 479/2017 linalowahusu wabunge wanane na madiwani wawili dhidi ya AG, Bunge, NEC, Halmashauri za Ubungo na Temeke, na Prof. Lipumba na wenzake wanane.

Katika shauri hilo, Jaji Mwandambo anatarajiwa kutoa uamuzi juu ya maombi ya zuio na pingamizi lililowekwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo.

Taarifa ya Bimani pia ilibainisha kuwa Oktoba 31, mbele ya Jaji Ndyansobera, kutakuwa na mashauri sita yatakayosikilizwa likiwemo linalohusisha wabunge 19 dhidi ya Prof. Lipumba ambalo litatajwa kwa ajili ya kupangwa kusikilizwa na shauri namba 28/2017 (Zuio la Ruzuku) ambalo litasikilizwa.

Mengine ni shauri namba 68/2017 (kesi ya msingi ya ruzuku) ambalo litasikilizwa, shauri namba 80/2017 (maombi mapya ya zuio la ruzuku) ambalo litatajwa ili kuanza kusikilizwa na shauri la msingi madai (civil case namba 13/2017) linalohusu uhalali wa wajumbe wa bodi ya wadhamini ya CUF iliyosajiliwa na RITA - Ally Salehe dhidi ya Prof. Lipumba na wenzake (uamuzi juu ya pingamizi unatarajiwa kutolewa).

Pia shauri la jinai namba 50/2017 (contempt of court proceedings) linalowahusu Prof. Lipumba na wenzake, Emmy Hudson - RITA, Jaji Francis Mutungi likihusisha kughushi nyaraka kwa lengo la kuingilia na kuharibu mwenendo wa mashauri yaliyopo mahakamani.

Shauri hilo linatarajiwa kutolewa uamuzi juu ya pingamizi lililowekwa na Wakili Hashimu Mziray kumtaka AG asiwatetee Jaji Mutungi na Emmy Hudson kwa kuwa shauri hilo linawahusu wao binafsi na si kwa nafasi zao.

Kesi hizo zinakuja huku wafuasi wa CUF ikiwa si ajabu kwao kugeuza Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kuwa ukumbi wa masumbwi kutokana na kutwangana kwa sababu mbalimbali, ikiwemo upande mmoja unapojaribu kumzuia Prof. Lipumba kuingia kusikiliza kesi inayomhusu.

KUFUNGWA AKAUNTI
Chama hicho kimekuwa katika mgogoro wa kiuongozi uliosababisha kufungwa kwa akaunti zake katika matawi yote nchini na kunyimwa ruzuku.

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mutungi tangu Agosti mwaka jana alizuia CUF kupewa ruzuku baada ya kuwapo kwa mgogoro wa kiuongozi ndani ya chama hicho uliosababishwa na mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na ofisi ya msajili, Prof. Lipumba kuandika barua ya kujivua uenyekiti wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na baadaye kuandika barua ya kutengua uamuzi wake.

Hata hivyo, Januari 10, mwaka huu, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro, alidai chama hicho kiliibiwa ruzuku ya Sh. milioni 369.378 zilizotolewa na Hazina na kuingizwa kwenye akaunti ya NMB Tawi la CUF Temeke inayodaiwa kumilikiwa na wafuasi wanaomuunga mkono Prof. Lipumba.

Mtatiro alidai kiasi hicho cha fedha kilitoroshwa Januari 5, mwaka huu na kuingizwa kwenye akaunti yenye jina la The Civic United Front yenye namba 2072300456 na kwamba bodi ya wadhamini ambayo ndiyo msimamizi wa akaunti za fedha na mali za CUF, haitambui akaunti hiyo.

Januari 31, CUF inayomuunga mkono Prof. Lipumba ilikiri kupitia kwa Mkurugenzi wake wa Fedha na Uchumi, Thomas Malima, kupokea sehemu ya malimbikizo ya ruzuku ya chama hicho kiasi cha Sh. milioni 369.366 kupitia akaunti namba 2072300456 ya CUF NMB Tawi la Temeke.

Oktoba mwaka jana, vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vilikubaliana kufungua kesi mahakamani dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mutungi na Prof. Lipumba kwa kukiuka sheria ya vyama vya siasa. Mbali na CUF, vyama vingine vinavyoundwa Ukawa ni NCCR Mageuzi, Chadema na NLD.

Siku chache baada ya kutinga mahakamani kuwashtaki wawili hao, Maalim Seif alikiri kuziandikia barua benki zote zenye akaunti za CUF kuziomba kuzifunga hadi pale mgogoro ndani ya chama hicho utatatuliwa kutokana na kile alichokiita njama za msajili kuupatia fedha za ruzuku upande unaomuunga mkono Prof. Lipumba.
 
Back
Top Bottom