CUF isivyoamini uwepo wa Katiba mpya 2015 | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

CUF isivyoamini uwepo wa Katiba mpya 2015

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by Kakke, May 30, 2012.

 1. Kakke

  Kakke JF-Expert Member

  #1
  May 30, 2012
  Joined: Dec 4, 2010
  Messages: 1,797
  Likes Received: 389
  Trophy Points: 180
  [h=1][/h]Written by Ashakh (Kiongozi) // 30/05/2012 // Habari // No comments


  [​IMG]Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Shaweji Mketo, akihutubia mkutano wa hadhara.

  Imeandikwa na Kaaneli Kaale; Tarehe: 28th May 2012
  WAKATI vyama mbalimbali vya siasa vina shauku ya kutumia Katiba mpya katika Uchaguzi Mkuu ujao, Chama cha Wananchi (CUF) kinasema huenda lengo hilo halitaweza kufikiwa kutokana na muda.
  Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Shaweji Mketo, anasema chama hicho kimetafakari na kuona kwamba huenda muda uliyopangwa hautatosha, kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika mchakato mzima wa kukusanya maoni na kuunda Katiba mpya.
  Tume ya kukusanya maoni na kuunda Katiba mpya inajumuisha wajumbe 30 chini ya Mwenyekiti wake Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, ilianza kazi Mei mosi mwaka huu na inapaswa kufanya kazi kwa miezi 18.
  Baada ya kukusanya maoni hayo, yatayawasilishwa kwa Rais kisha Bunge Maalumu la Katiba litaundwa ili kuchambua rasimu na baadaye wananchi watapiga kura ya maoni ili kuikubali au kuikataa rasimu ya Katiba mpya.
  Ingawa hakuna taarifa zinazoeleza itakuwaje kama wananchi watakataa Katiba hiyo, kwa mujibu wa taarifa ya Serikali Katiba mpya inatarajiwa iwe tayari ifikapo Aprili 26, 2014 na inatarajia kutumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
  Mketo ambaye pia ni Naibu Mkurugenzi wa Mipango ya Uchaguzi na Bunge katika chama cha
  CUF, anasema chama chake kimetafakari kwa makini na kuona kuwa kama ukomo wa kuandaa Katiba utapewa kipaumbele itakuwa vigumu kufikia lengo la msingi ambalo ni kuwa na Katiba inayotokana na Watanzania ambayo inakidhi kupata matakwa ya Watanzania.
  Anasema hata kama Katiba hiyo itakamilika Aprili mwaka 2014 muda uliobakia hautatosha kufanya marekebisho ya msingi hasa kuunda Tume Huru ya Uchaguzi, kuandaa taratibu na kuweka misingi imara ya kufanya Uchaguzi Mkuu kwa kuzingatia demokrasia, amani na utulivu.
  Anasema historia kuhusu Katiba, inaonesha kuwa Watanzania wamevumilia kwa muda mrefu kutokana na kitendo cha watu wachache kufanya mabadiliko ya Katiba pasipo kushirikisha wananchi jambo ambalo hivi sasa haliwezekani tena kutokana na ukweli kuwa hivi sasa Taifa linafuata mfumo wa demokrasia ya vyamba vingi ambao unatoa fursa ya watu kutoa maoni ili kuwa na maamuzi shirikishi katika mustakabali wa Taifa.
  Kumbukumbu zinaonesha kuwa wakati wa kuunda Muungano, Baba wa Taifa , Mwalimu Julius Nyerere, alisema baada ya miaka 10 ya Muungano Watanzania watapewa muda wa kujadili aina ya muungano wanaoutaka.
  Hata hivyo jambo hilo halijafanyika badala yake Katiba iliendelea kufanyiwa marekebisho ya mara kwa mara pasipo ridhaa ya wananchi. Kitendo cha wananchi kutokushirikishwa wala kupewa fursa ya kujadili jinsi ya kuimarisha muungano kimesababisha kero nyingi ndani ya muungano na kusababisha watu wa pande zote mbili kuvutana.
  Akitoa mfano wa kero za Muungano ambazo zinapaswa kuchukuliwa kama changamoto
  Mketo anasema malalamiko yaliyotolewa hivi karibuni na Muasisi wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia (CHADEMA), Edwin Mtei, kuwa alihoji ni vipi Tanzania Bara ambayo ina watu takriban 42 milioni inawakilisha na wajumbe sawa na Tanzania Zanzibar ambayo ina watu wasiozidi 1.5 milioni.
  Anasema hoja zilizoibuliwa na Mtei, zina msingi hivyo hazipaswi kupuuziwa, kwa sababu nyuma yake kuna watu ambao nao wanaona jambo hilo kama halina usawa.
  Kwa upande mwingine kauli hiyo imeamsha hisia za baadhi ya Wazanzibari ambao kwa muda mrefu wamekuwa na shauku la kuthaminiwa kama nchi pasipo kujali udogo wa ardhi yao wala
  uchache wa watu kwa kuwa tangu enzi za mababu walikuwa na utawala kamili unaojitegemea.
  Kauli hiyo imechochea harakati za kikundi kinapinga muungano na kwamba jambo hilo halipaswi kufumbiwa macho. Uzoefu unaonesha kuwa hata nchi ambazo zimefanya mabadiliko ya katiba kama vile Kenya, Zimbambwe na Ghana, zilitumia muda mrefu ikilinganishwa na muda ambao Tanzania inataka kutumia.
  Kwa kuwa Tanzania imekabiliwa na changamoto nyingi kuhusu Muungano inapaswa kutenga muda wa kutosha kuunda Katiba mpya na kufanya marekebisho kwa kuzingatia maoni ya watu wengi.
  “Suala la Muungano limekuwa likifumbia macho wakati kuna kero nyingi, mfano watu wa nchi moja wana idadi tofauti ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu, Zanzibar wanapiga kura tano wakati Tanzania bara wanapiga kura tatu,” Mketo anaeleza.
  Wakati Wazanzibari wanapiga kura nyingi zaidi, wizara ambazo sio za Muungano kama vile Afya ya Wizara ya Afya Zanzibar, zinatumia nembo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati Wizara ya Tanzania Bara zinatumia nembo ya Muungano, wakati Waziri wa Afya Tanzania bara hana mamlaka katika Wizara ya Afya Zanzibar.
  “Leo Rais wa Zanzibar hana mamlaka Bara yaani akija Bara anakuwa kama Waziri asiyekuwa
  na Wizara maalum…hilo linawakera sana Wazanzibar pasipo kujali tofauti zao hivyo ni vyema kuwapa Watanzania fursa ya kuchagua aina ya Muungano wanaoutaka,” anasisitiza.
  Mketo anasema upungufu huo umefumbiwa macho kwa muda mrefu jambo ambalo
  linasababisha manung’uniko ya chini kwa chini hivyo sasa ni kipindi muafaka cha kujadiliana kwa kina na kwa uwazi ili kuimarisha Muungano.
  Marekebisho ya Katiba ya Zanzibar yaliyofanyika hivi karibuni inataja wazi kuwa Zanzibar ni nchi jambo linalowapa Wazanzibar nguvu kubwa zaidi ya kudai haki zao pasipo kujali udogo wa nchi hiyo kijiografia.
  Ingawa Zanzibar ina idadi ndogo ya watu ikilinganishwa na bara kisheria wana nguvu kwa kuwa kama kama idadi kubwa ya Wazanzibari watapiga mchakato wa Katiba upande wa Tanzania bara haitaweza kufanya mabadiliko ya Katiba pasipo kuafikiana na Zanzibar.
  Mketo anasema shauku ya baadhi ya viongozi wa siasa kutaka kutumia Katiba mpya katika uchaguzi mkuu ujao kinaweza kusababisha Tanzania kuwa na Katiba bomu na yenye matatizo kuliko iliyopo sasa.
  Kwa mtazamo wa CUF, ili kupata Katiba mpya inayokidhi matakwa ya Watanzania wote, ni vyema kuondoa kipengele kinachosema kwamba Katiba hiyo itatumika katika uchaguzi mkuu ujao kwa sababu kipengele hicho kinaweza kuwa kikwazo.
  Wakati mchakato wa kuunda Katiba mpya unaendelea ni vyema kila Mtanzania ajiulize, tunataka Katiba kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao au Katiba ambayo itakidhi matakwa ya Watanzania wa kizazi cha sasa na kizazi kijacho?”
  Jibu la swali hilo linaweza kutoa angalizo na kuwezesha mchakato wa kuunda Katiba mpya kufanyika kwa makini zaidi na kufikia tamati katika hali ya amani na utulivu.
  CUF inahofu kuwa kama angalizo hilo halitatolewa mapema wanasiasa wanaweza kutumia nafasi hiyo kuvuruga amani ya nchi kwa kisingizio kwamba Serikali imekiuka makubaliano ya kutumia Katiba katika uchaguzi ujao.
  Kama uchaguzi mkuu utatumika kama kikwazo cha kuongeza muda wa kuunda Katiba mpya ipo hatari ya kurudia makosa ya nyuma ambapo tume ziliundwa na kukusanya maoni ambayo yaliwekwa pembeni na badala yake wataalamu wakatumiwa kuunda Katiba bila kuzingatia
  maoni ya wananchi.
  “Katika Tume ya sasa kuna wataalamu wa kuunda katiba ambao walishiriki kuunda katika ya mwaka 1977…kama utatokea mgongano watu hao wanaweza kutumia uzoefu wao kuunda Katiba pasipokuzingatia maoni ya wananchi,” alisema.
  Ili kuzuia mgongano huo ni lazima kuwekeza kwenye maslahi ya Taifa na kuunda Katiba mpya isiyo egemea upande wowote na yenye kutoa wigo mpana wa kukuza demokrasia ya
  nchi kwa kuzingatia umoja wa Kitaifa, amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania kwa kuweka mbele muungano wa Watanzania.
   
Loading...