Rubawa
JF-Expert Member
- Dec 25, 2015
- 2,055
- 3,267
Na Ahmed Rajab
BADO hatuna hakika nini hasa kilichotokea Alhamisi iliyopita kwenye kisiwa cha Nzuwani (Anjouan). Siku hiyo Rais Azali Assoumani alikuwa akifanya kampeni katika sehemu za vijijini za kisiwa hicho cha pili kwa ukubwa miongoni mwa visiwa vinne vya Comoro.
Serikali ya Azali imedai kwamba rais alinusurika chupuchupu kuuawa ulipotokea mlipuko karibu na alipokuwako. Inasema kuwa kwanza walinzi wa rais wakifikiri lilikuwa shambulio la roketi. Juu ya mlima waligundua waya zilizotegwa ili patokee mlipuko msafara wa rais utapopita.
Wapinzani wa Azali, wakiwa pamoja na chama kikuu cha upinzani cha Juwa, wamekanusha shtuma hiyo. Wanasema kuwa hakukuwa na mpango wowote wa kumuua Rais ila huo ulikuwa mpango wake mwenyewe wa kujidai kwamba ati akitaka kuuawa.
Pande zote mbili zimelihusisha tukio hilo na uchaguzi ambao umepangwa ufanywe Machi 24. Upande wa serikali umesema kwamba lengo la shambulio hilo lilikuwa kuuzuia uchaguzi usifanyike.
Upande wa upinzani nao umesema kuwa lengo la serikali kurubuni shambulio hilo la uongo ni kuwatia watu hofu wasende kupiga kura siku ya uchaguzi.
Hofu ni moja ya hila zinazotumiwa na watawala wa kidikteta kuufanya uchaguzi usiwe huru. Wapigakura hujihisi kuwa hawako huru kwenda kupiga kura zao wakihofia kuzuka kwa fujo zinazoweza kusababisha umwagaji wa damu.
Kadhia kama hiyo iliyotokea Nzuwani Alhamisi iliyopita inaweza pia kutumiwa na serikali kuwa ni kisingizio cha kukupiga marufuku chama kikubwa cha upinzani au kuwapiga marufuku wagombea uchaguzi wa upinzani wasishiriki katika uchaguzi.
Azali hadi sasa hakuchukua hatua yoyote kati ya hizo mbili. Kwa hali ilivyo visiwani Comoro, mchuano wa kuwania urais Machi 24 utakuwa mkali sana na amekwishaonywa kwamba akichukuwa hatua yoyote kati ya hizo atazidi kuupalilia moto wa kisiasa visiwani humo .
Inavoonyesha ni kwamba Azali amekwishaanza kubanwa na kile kitanzi alichojitia kama nilivyoeleza katika sahafu hii miezi kadhaa iliyopita. Amewaudhi wengi kwa hatua zake za kimabavu tangu zile za kubadili katiba na za kuwakandamiza wapinzani, hususan wafuasi wa hasimu yake mkubwa rais wa zamani Ahmed Abdallah Sambi, mwenyeji wa Nzuwani.
Safari hii ilikuwa zamu ya Nzuwani kutoa rais lakini Azali amebadili Katiba kwa kuyafuta makubaliano ya Fomboni yaliyomaliza mgogoro mkubwa wa kisiasa visiwani humo. Makubaliano ya Fomboni yaliyotiwa saini 2001 katika mji wa Fomboni, kisiwani Mwali (Moheli), yanakipa kila kisiwa fursa ya kutoa rais kwa kipindi cha miaka mitano. Rais hupatikana kwanza kwa utaratibu wa mchujo kwa wagombea watatu katika kisiwa kinachohusika na baadaye kupigiwa kura na visiwa vyote kumchagua rais.
Katika kampeni zao wapinzani wote wenye kuugombea urais wameahidi kukirudishia urais kisiwa cha Nzuwani 2021 pindi mmoja wao akishinda. Wamesema kwamba kufanya hivyo ni kurejesha utawala wa kisheria.
Hatua ya Azali ya kuinyima Nzuwani haki yake ya safari hii kutoa rais imekifanya kisiwa kizima kimgeukie na kumpiga pande. Azali ana maadui wengi pia katika visiwa vingine, pamoja na cha Ngazidja atokako yeye. Kwa hakika, ninaweza kusema kwamba sijapatapo kumuona rais wa Comoro mwenye kuchukiwa zaidi yake Azali.
Kwanza anapingwa kwa namna anavyotawala na kwa kushindwa kuwaondolea wananchi shida zao za kimaisha. Pia wengi wa wapinzani wake wanasema wanaona aibu kwa jinsi alivyoidhalilisha nchi yao kwa kujipendekeza kwa Saudi Arabia na kujifanya kibaraka wao katika Umoja wa Kiarabu.
Comoro ilikuwa ni miongoni mwa nchi za mwanzo zilizo wanachama wa Umoja huo zilizoiunga mkono moja kwa moja Saudi Arabia na tawala za kifalme za Ghuba katika ugomvi wao na Qatar.
Kabla ya hapo mnamo 2016 Azali alivunja mahusiano ya kiserikali baina ya Comoro na Iran, adui mkubwa wa Saudi Arabia. Januari mwaka huu aliushangaza ulimwengu na kuwahamakisha wengi duniani aliposema anashangazwa kuona dunia ikipiga kelele kuhusu kifo cha Adnan Khashoggi, mwandishi wa Saudi Arabia aliyeuliwa katika ubalozi mdogo wa nchi yake huko Uturuki. Azali aliuliza: “Kuna ubaya gani Msaudi anapoouliwa katika ubalozi wa Saudi Arabia?”
Azali aliyasema hayo katika hafla iliyohudhuriwa na Hamad bin Muhammad Alhajiri, balozi wa Saudi Arabia aliye Comoro, wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa barabara moja kuu uliogharimiwa na Saudi Arabia. Comoro inaitegemea sana Saudi Arabia kwa fedha za kugharimia miradi ya maendeleo. Mwaka jana Saudi Arabia iliahidi kuipatia Comoro dola za Marekani milioni 22 kugharimia miradi ya maji na ujenzi wa barabara visiwani humo.
Kuna tetesi kwamba Saudi Arabia inamsaidia Azali katika ufumaji wa njama zake za kutaka kusalia madarakani. Saudi Arabia inataka Azali abakie madarakani ili iweze kuitumia Comoro katika jukwaa la siasa za kimataifa na pili ili iwe na sauti kubwa katika mauzo ya mafuta yanayochimbwa Comoro.
Kwa mujibu wa vyanzo vyangu vya habari mnamo Februari 25 na Machi 8 ndege za Saudi Arabia za kubebea shehena za silaha zilitua kwenye uwanja wa ndege wa Hahaya, nje ya Moroni, mji mkuu wa Comoro.
Hamna shaka yoyote kwamba Azali anaicheza ngoma inayopigwa Riyadh. Hivi karibuni amekuwa akizihamishia Comoro chuki za Saudi Arabia dhidi ya mashi’a wa Iran. Kwa mfano, alipokuwa akisalisha sala ya Ijumaa kwenye kijiji kimoja cha Nzuwani alisema katika hotuba yake ya Ijumaa: “Nchi yetu hatutaki mashi’a; hatutaki mashi’a watutawale.” Pia alicheza na lugha aliposema: “Sisi si mbwa”, akitumia neno la Kifaransa “chien” (mbwa) linalotamkwa kama “shi’a”.
Wakati mwingine alisema kuwa mashi’a ni magaidi na Comoro haitaki magaidi. Pamoja na kuwafurahisha watawala wa Saudi Arabia, Marekani na Ufaransa, nchi nyingine ambayo Azali yuko karibu sana nayo, rais huyo wa Comoro kwa matamshi hayo dhidi ya mashi’a amekuwa akimpiga kijembe Sambi, sahibu wake wa zamani.
Miongoni mwa vyama vikuu vya upinzani Azali anakiogopa zaidi kile cha Juwa kilichoasisiwa na Sambi anayendelea kuwa rais wake. Chama hicho kina wafuasi wengi mno Nzuwani na wiki iliyopita mgombea wake wa urais Mahmoud Ahmada alipofanya mkutano wa hadhara kisiwani humo ilikuwa kama kisiwa kizima kilihudhuria mkutano kwa umati wa watu waliomiminika. Mahmoud alivutia umati wa watu katika mkutano alioufanya karibuni Moroni.
Pamoja na kuwa mgombea urais wa chama cha Juwa, Mahmoud pia ni wakili muhtasi wa Sambi na Azali anahofu kwamba lau Mahmoud Ahmada akishinda uchaguzi watu wa Sambi watamlipizia kisasi kwa maovu aliyomtendea Sambi.
Mgombea mwengine wa urais, waziri wa zamani Fahmi Said Ibrahim naye pia amekuwa akivutia umati wa watu katika mikutano yake. Miongoni mwa wagombea 11 wa urais, tukiwaacha hao wawili, wengine wanaotajwa sana ni Mwinyi Baraka, gavana wa zamani wa kisiwa cha Ngazidja na Soilihi Mohamed “Campagnard” (Mshamba, jina la utani alilopewa tangu utotoni). Huyu alikuwa pamoja na Azali jeshini na kama Azali alipata mafunzo ya kijeshi katika vyuo vya kijeshi vya Morocco na Ufaransa.
Campagnard alipata umaarufu visiwa vya Comoro vilipovamiwa mara ya mwisho na askari wa kukodiwa wa kizungu wakiongozwa na Bob Denard. Campagnard alisimama kidete na alipigana na Denard, na akapigwa risasi na kujeruhiwa mguuni. Hadi leo anatembea kwa kuchuchumia.
Kinyume na alivofanya yeye, Azali, aliyekuwa na cheo kikubwa zaidi yake jeshini, alikimbilia ubalozi wa Ufaransa akitaka Wafaransa wampe hifadhi. Siku hiyo ndipo Campagnard alipoanza kujulikana kama shujaa na Azali kama mwoga.
Wakati mikutano ya upinzani ikiwa inahudhuriwa na watu kwa hiari yao, wakijilipia wenyewe nauli za kwenda mikutanoni, ile ya Azali inajazwa na watumishi wa serikali. Wanatishwa kuwa kama hawendi basi watafukuzwa kazini.
Kwa sasa Azali anaungwa mkono na mwanasiasa Ali Houmeid Msaidie aliyebandikwa lakabu ya “sungura” kutokana na ujanja wake wa kisiasa uliomwezesha kuwatumikia marais mbalimbali katika nyakati tofauti. Alianza kwa kumtumikia Tajiddine bin Masoud na waziri mkuu Abbas Djoussouf baada ya kifo cha kutatanisha cha Mohamed Taki punde baada ya kurudi kutoka ziarani Ufaransa na Uhispania. Pia aliwatumia marais Said Mohamed Djohar na Ikililou Dhoinoune.
Alikuwa mgombea mwenza wa makamu wa rais Mohamed Soilihi Mahmadou ambaye safari hii ameenguliwa na Mahakama ya Kikatiba. Msaidie aliyewahi kuwa katibu mkuu wa chama cha CRC cha Azali sasa anamuunga mkono tena akiwa mkuu wa kampeni yake ya uchaguzi na msemaji wake mkuu.
Msaidie ana mahusiano maalum na Tanzania na anatumika kama kiungo baina ya Azali na duru za watawala wa Tanzania. Ndani ya Ubalozi wa Tanzania mjini Moroni kuna afisa mmoja (jina tunalihifadhi) mwenye urafiki mkubwa na waziri wa mambo ya ndani wa Azali, Daud “Kiki”. Huyu ni mtu aliye karibu sana na Wafaransa na aliwahi kuwa rais wa Jumuiya ya Mshikamano baina ya Ufaransa na Comoro.
Mambo yanavyokwenda inaelekea kwamba Azali atashindwa sana hasa ikiwa patakuwa na waangalizi wa kweli wataosimamia kidhati uchaguzi huo hasa kutoka jumuiya ya Sadc. Dhana iliyopo, mijini na vijijini Comoro, ni kwamba Azali amekwishaanza kuuchakachua uchaguzi. Tetesi zilizovuja kutoka duru zake zinasema kwamba amekwishapanga katika duru ya kwanza apate ushindi wa asilimia 55 za kura.
Kwa hivyo, bila ya uchaguzi kuwa wa haki na huru Azali atashinda kwani vyombo vyote vya kuthibitisha matokeo ya uchaguzi, vikiwa pamoja na Tume ya Uchaguzi na Mahakama ya Kikatiba, vimejazwa wateule wake.
Baruapepe: aamahmedrajab@icloud.com; Twitter: @ahmedrajab
Sent using Jamii Forums mobile app