CHRISTMASS vs X-MASS

Rosh Hashannah

JF-Expert Member
Sep 13, 2017
3,415
2,042
Vijana kadhaa wameniomba nirudie maelezo kuhusiana na maneno “CHRISTMAS” na “X-MAS” maana wanachanganywa na wenzao. Kifupi, maelezo yanayosambazwa kwenye mitandao yetu ni kwamba “Christmas” ni sahihi na “X-mas” siyo sahihi. Maelezo haya yanayosambazwa si sahihi, ni ya uongo. Ni ushuhuda wa kutojua tu jinsi jina la Kristo linavyoandikwa kwa herufi za Kigiriki (Kiyunani). Wanatatizwa na kitu kidogo tu "X" yaani "Chi" iliyo herufi ya kwanza ya jina "Kristo" kwa Kigiriki.
Ndiyo hivyo tena, "Usichokijua ni kama usiku wa giza".
Basi tuwekane sawa hapa. Tukianzia kwenye maneno hayo, kwa karibu kabisa tunarudi kwenye maneno ya lugha ya Kiingereza cha enzi tatu:-
1. Kiingereza cha zamani,
2. Kiingereza cha enzi ya miaka ya kati (karne 5 hadi15) na
3. Kiingereza cha siku hizi.

Kwa Kiingereza cha zamani “Christmas” ilitamkwa “Cristes maesse” na maana yake ilikuwa “Christ’s festival” yaani sikukuu ya Kristo.
“Crist” ndiyo “Christ” ndiyo Kristo. Kristo maana yake “Mpakwa” ndiyo inayotafsiri jina la Kiebrania (lugha ya Wayahudi) “Meshiah”, yaani “Mpakwa wa Bwana” . “Meshiah” ndiyo tunayotamka sisi Waswahili kama Masiya au Masiha.
Neno “maesse” maana yake “festival” yaani sikukuu au sherehe. Katika Kiingereza za enzi ya kati “Cristes maesse” ilinyooshwa na kuwa “Cristemas” ndipo katika Kiingereza cha siku hizi ikafika kutamkwa na kuandikwa “Christmass”.
Yaani hapa tunacheza na maendeleo ya lugha ya Kiingereza katika matamshi na
maandishi tu. Hadi hapo nadhani nimeeleweka.

Lakini suala la CHRISTMAS na X-MAS linarudi kwenye lugha ya Agano Jipya ndiyo Kigiriki au Kiyunani. Jina hilo “Crist” au “Christ” limetoholewa kutoka jina “CHRISTOS” ndiyo Kristo (tukifupisha kwa kudondosha “s” ya mwishoni). Walatini (watu wa Dola ya Rumi) wakatamka “CHRISTUS” ndiyo Kristu (tukifupisha kwa kudondosha “s” ya mwishoni). “Christos” maana yake ni Mpakwa, Masiya au Masiha. Masiya au Masiha yenyewe inatoholewa kutoka jina la Kiebrania “Meshiah” kama nilivyoonesha hapo juu.
Waingereza hutohoa “Meshiah” na kuandika na kutamka “Messiah”.
Kumbe katika Kigiriki au Kiyunani, “CHRISTOS” huandikwa kwa herufi ndogo "Χριστός” na kwa herufi kubwa “XPICTOC” au “ΧPIΣTOΣ” au kwa sanaa “XPISTOS”. Katika Kigiriki
hiyo “X” siyo “eksi” bali ni “ch” na hiyo “P” siyo “pi” bali “r”. Hivi kwa Kigiriki “XPI” husomwa “Chri.”
Halafu, kutokana na herufi “X” na “P” kusimama mwanzoni mwa jina “XPISTOS” au
"XPICTOC", Wakristo wa mwanzo walizitumia herufi hizo mbili kufupisha jina
“CHRISTOS” hivyo wakawa wanaandika wakibebanisha “X” na “P” na kuzaa alama moja maarufu sana mnayozoea kuiona kwenye nguo za misa au vitambaa vya altareni na kwenye vitabu. Ni alama ya “P” iliyokatwa mguuni kwa mstari -- au X.
(Poleni, hapa nashindwa kuichora. Herufi za Kigiriki zinagoma).

Kwa maelezo haya basi, “X-MAS” si neno tofauti na “CHRISTMAS”. Ni neno lile lile
isipokuwa badala ya kuandika CHRIST kirefu watu wanafupisha kwa X tu. Ndipo
inapotokea X-MAS mahali pa CHRISTMAS. Hivyo hiyo “X” ya mwanzoni haimaanishi
“mkasi” wenye maana ya “kukata” au “hakuna” bali “X” yenye kufupisha jina “CHRISTOS” na “MAS” huko mwishoni kumaanisha “SIKUKUU” au “SHEREHE”.
Kwa hiyo, asiwadanganyeni mtu wala asiwababaisheni mtu kwamba “X-MAS” maana yake “HAKUNA KUSANYIKO LA KRISTO” eti kwa vile “MAS” ni neno la Kigiriki
linalomaanisha “MKUSANYIKO”. Hakuna neno la Kigiriki MAS linalomaanisha
MKUSANYIKO. Iweni na amani, vijana. Hata mtu akilazimisha maneno ya Kigiriki
maneno yote yanayokaribiana na MAS japo kwa maandishi na matamshi hakuna neno lenye maana ya mkusanyiko. Tazama maneno yaliyopo ni “μασάομαι” lenye maana ya kuuma, kung’ata, “μαστιγόω”lenye maana ya mchapo wa kiboko au kuadhibu,
“μαστίζω”lenye maana ya kuchapa, “μάστιξ” lenye maana ya pigo la mjeledi na maradhi na “μαστός” lenye maana ya kifua. Kama msomavyo hapa katika maneno haya hakuna neno linalomaanisha “MKUSANYIKO”.
Basi, vijana kuweni na amani. X-MAS si neno tofauti na CHRISTMAS. Ni neno lile lile
isipokuwa badala ya kuandika CHRIST kwa urefu watu wanafupisha kwa X tu.
Nawatakieni maandalizi mema ya Krismasi au Noeli.
Kwisha kumaliza somo hili la lugha ya Kiingereza na Kigiriki naomba kuwaongezea mambo kidogo.

Majina: sikukuu hii huitwa pia Kuzaliwa (Nativity) au Yule. Ni sikukuu ya utamaduni wa Kikristo. Maana yake ni kukumbuka na kuadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Na kwa vile ni shauri la Mungu kutupatia sisi wakosefu zawadi ya Mkombozi, katika kuadhimisha sikukuu hii zawadi hutawala. Ni sikukuu inayosherehekewa kwa mikusanyiko, upambaji wenye ishara nyingi kama vile miti ya Krismasi na dhifa za keki, kula na kunywa pamoja.

Tarehe ya kuadhimisha katika Kanisa la Magharibi na baadhi ya Makanisa ya Mashariki pamoja na walimwengu wengine ni tarehe 25 Desemba. Lakini katika baadhi ya Makanisa ya Mashariki huadhimishwa tarehe 7 Januari. Na katika makanisa ya Kiarmeni huadhimishwa tarehe 6 Januari.

KILA LA HERI KWENU NYOTE!
Mzee wetu Pd. Titus Amigu
 
Back
Top Bottom