Chanzo cha Mungu ni kipi kulingana na maandiko ya kale ya Misri

Undava King

JF-Expert Member
Aug 11, 2017
3,205
5,333
Katika kitabu kilichoandikwa na Sir Ernest Alfred Wallis Budge "Legends of the Gods" tunapata simulizi nzuri ya miungu ya kimisri ambayo inatupatia mwangaza kidogo katika hili la chanzo cha Mungu kulingana na kwamba hadithi hizi zimekuwapo miaka maelfu kabla ya ujio wa maandiko ya dini za kileo.

Kitabu hiki kinazungumzia vyema chanzo na mwanzo wa dhana ya uwepo wa Mungu na kinatoa ufafanuzi mzuri ambao unakosekana katika maandiko matakatifu ya dini ambayo hayajaweza kuelezea kinaga ubaga juu ya kipi kilifanyika kuwa umungu kabla ya Mungu kufanya uumbaji wake.

Simulizi hii haiwezi kukamilika ikiwa hatutoweza kumzungumzia Neb-er tcher (the lord to the uttermost limit) yenye maana ya "Bwana asiye na ukomo" Neno "ukomo" uashiria muda na nafasi (time & space), na ndiye Mungu wa milele wa ulimwengu.

Ni jinsi gani aliweza kutokea huyu Neb-er tcher haijazungumzwa katika kitabu cha wahenga hawa, isipokuwa katika maandiko ya kikoptiki, anaongelewa kwa sifa zote za Kimungu waleo.

Neb-er tcher alikuwa na nguvu zisizoshindwa wala kuwa na kikomo ambazo zilitanda mahali pote katika nafasi yenye utupu. Pindi alipopata shauku ya kuumba dunia, hapo ndipo alipouvaa uhusika kama Mungu Khepera, ambaye ni mwanzo na mwisho;Muumba. Akitambulika kama Mungu muumba na wamisri.

Wakati Neb-er tcher akibadilika kuwa Khepera dunia ilikuwa bado haijaumbwa. Kwa hali iliyoonekana ni kuwa kwa wakati huo kulikuwa na maji mengi sana ambayo yalitanda juu ya uso wa ulimwengu au dunia nzima ya wakati huo iliyoitwa NU, na uwezekano ni kuwa ndani ya bahari hii ndipo mabadiliko yalikochukulia nafasi.

Ndani ya bahari hii kuu kulikuwamo na chembe chembe za uhai wa viumbe wote ambao nao baadae walikuja kuvaa uhusika wa viumbe mbingu na ardhi. Lakini kwa nyakati hizi waliishi katika hali ya utepetevu na kutojiweza.

Kutoka ndani ya bahari hii kubwa ndipo Khepera alikojiinua, hivyo akafahulu kupita hali ya utepetevu na ajizi (state of passiveness and inertness) mpaka katika kutenda.

Pindi Khepera alipokuwa katika hatua za kujiinua kutoka katika lindi kubwa la maji alikumbana na hali ya sintofahamu baada ya kujikuta katika sehemu ya utupu wa space pasipo hata na mahali pa kukanyaga/kujitegemezea.

Katika toleo la pili la mafunjo (papyrus) ya kimisri inaelezea kuwa Khepera alijipatia uwezo wa kuendelea kuwepo katika hali ya kujitegemeza pasipo mahali pa kutia unyayo au kushikilia chochote kupitia kulitamka jina lake mwenyewe. Tukirudi katika toleo la kwanza la maandiko ya mafunjo linatudokeza kuwa Khepera alitumia maneno ili kujitwalia mahali pake anapoweza kukanyaga.

Kwa maana nyingine ni kuwa wakati Khepera akiwa bado ni sehemu ya kiumbe Neb-er tcher, alitamka NENO "Khepera" na punde Khepera akatokea. Vivyo hivyo alipohitaji mahali pa kujitegemeza katika nafasi tupu (space) alitamka tu majina ya vitu na vikawa.

Toleo hilo hilo la kwanza linazungumzia pia juu ya Moyo, wakati toleo la pili likizungumzia uwepo wa Roho ya Nafsi (heart-soul) namna ilivyo mwezesha muumba katika kufikia ubunifu wa kutenda. Kwa namna hii aliweza kutambua kupitia moyo wake kipi akitaraji kukiumba na namna gani akipe jina na punde kiwe kama alivyotarajia kiwe.

Mfumo huu wa kifikra uelezewa na wamisri kama "Laying the foundation in the heart" yaani kujiwekea msingi wa kiroho moyoni. Ili kufanikisha yote haya Khepera pia alipata msaada toka kwa Mungu mke Maat, ambaye uchukuliwa kama Mungu wa sheria, Agizo na ukweli.

Na katika nyakati za zamani Maat alichukuliwa kuwa kama sehemu ya kike ya Mungu Thoth "the heart of the god Ra" yaani moyo wa Mungu Ra. Kwa mujibu wa wahenga inaonekana kama Maat alichukua uhusika zaidi wa kuwa Mungu wa Hekima "wisdom" kama ilivyoelezewa katika kitabu cha Mithali, "for it was by Maat that he "laid the foundation" ikimaanisha kuwa 'ni kwa kupitia Maat, "aliweza kusimika misingi.

Sasa kutokana na tukio lile la kusimama, ikatokea kitu ambacho wamisri walikipachika uhusika wa triad au trinity "UTATU" Khepera alipata kuunganika na kivuli chake na matokeo yake ni kupata kizazi ambacho kilitokana na mwili wake na kuunda miungu Shu na Tefnut.

Kulingana na maandiko ya kwenye mapiramidi tukio hili lilitokea katika eneo lijulikanalo kama ON (Heliopolis) tumezoea kupaita mbinguni. Na kwa namna ya kale ya hadithi za kihenga zinaelezea kwa kuhusisha uzalishaji wa Shu na Tefnut na kitendo cha kujichua.

Kiuhalisia miungu hii inavaa uhusika wa hewa na ukavu pamoja na vimiminika, kutokana na kuumbwa kwao ndipo vifaa (material) vya ujenzi wa anga na matabaka yake vikapatikana.

Shu na Tefnut walibarikiana, na vizazi vyao ni Keb;Mungu wa dunia, na Nut; Mungu mwana mke wa anga.

Mpaka hapo tunakuwa na miungu mitano jumla yaani:

Khepera- mwenye kanuni nzima ya ubunifu (the creative principle)

Shu- Tabaka la angahewa (the atmosphere)

Tefnut- Maji ya anga/mvua (the waters above the heavens)

Nut- Mungu mwanamke wa anga (the sky-goddess)

Keb- Mungu wa dunia (the earth-god)

Katika kipindi hiki jua lilikotokea na kuangaza kwa mara ya kwanza kutoka katika vilindi vya maji ya NU, nakuangazia dunia na ikatokea mchana.

Katika zama za kale mwanga wa jua ulichukuliwa kama muundo wa Shu. Miungu Keb na Nut waliunganishwa katika mwanga na kubarikiana na ujio wa mwanga ndiyo uliokuwa ukiwatenganisha; mfano inapotokea ikawa ni mchana, Nut; Mungu mke wa anga, alibakia katika eneo lake juu ya dunia, akipata support toka kwa Shu, lakini pindi jua linapozama uachilia anga na taratibu uteremka mpaka pale linapotua juu ya mwili wa Keb; Mungu wa dunia.

Sasa kubariki huku kukapelekea Keb na Nut kupata miungu wengine watano baada ya kuzaliwa; Osiris, Horus, Set, Isis na Nephthys.

Osiris na Isis walioana hata kabla ya kuzaliwa kitendo kilichopelekea kuzaliwa kwa mwanao wa kiume aliyeitwa Horus; Set na Nephthys nao vivyo hivyo wakamzaa Anpu (Anubis), japo huyu Anu ajaongelewa kiundani na wahenga katika simulizi zao.

Katika miungu wote hawa ni Osiris pekee ndiye aliyetajwa katika maandiko ya wahenga kwa kupewa umuhimu ambapo katika simulizi ya Khepera akiongea kama Neb-er tcher, anasema kuwa jina lake ni Ausares, yeye ambaye ni kiini cha jambo la kitambo kirefu ambalo yeye mwenyewe ameundwa/kutokana nalo. Hivyo Osiris alikuwa wa dutu ile ile kama Mungu mkuu aliyeumba ulimwengu.

Kulingana na maandiko haya ya wamisri yanatanabaisha kuwa kuzaliwa kwake duniani Osiris ilikuwa ni re-incarnation ya babu mkuu.

Kipande hiki cha maelezo ya wahenga kinatusaidia kupata majawabu juu ya mtizamo uliojengwa juu ya Osiris kwa miaka mingi kuhusiana na kuchukuliwa kama roho kuu ya mababu (the great ancentral spirit) ambaye kipindi alipokuwa duniani alileta faida kubwa kwa binadamu na alipokuwa mbinguni alikuwa ni mwokozi wa nafsi.

Wahenga wanalizungumzia jua kama jicho la Khepera au Neb-er tcher, ambalo upatwa na misukosuko mingi inayopelekea kufifisha mwanga wake na hivyo kabla ya anguko lake na kuzima kabisa, Mwezi uliyoundwa na Khepera utumike kama jicho la pili uangaza badala ya jua na kuupa furaha jicho hilo la kwanza.

Hivyo jua alilipatia kipaumbele maalumu kwa kulipachika katikati ya kipaji chake cha uso na kulipa mamlaka ya kutawala juu ya uso wa dunia na kuwezesha uhai huku mwezi wenyewe ukiusishwa na nguvu ya uzazi na mavuno.

Kulingana na simulizi za wahenga, Mwanaume na Mwanamke hawatokani na dunia, bali moja kwa moja kwenye mwili wa Mungu Khepera au Neb-er tcher, ambaye aliwaweka pamoja watu wake na kuwanyunyizia machozi yake, papo hapo wakawa viumbe hai, kutokana na machozi yaliyodondoka kutoka katika macho yake.

Hakuna mahali katika simulizi ambapo viumbe wengine (ukiachilia binadamu) wamepewa umuhimu katika uumbaji wao, isipokuwa aliumba kila kitu kwa namna yake, ikiwemo na viumbe wakubwa, wakiume kwa wakike,na viumbe vyote vilizaliana na kuongezeka kwa namna zao na kwa sababu hiyo dunia ikajazwa na uzazi wao mpaka waleo.

NB: Hii ni kwa kujibu wa maandiko kutoka katika papyrus of Nes-Menu.
 
Katika kitabu kilichoandikwa na Sir Ernest Alfred Wallis Budge "Legends of the Gods" tunapata simulizi nzuri ya miungu ya kimisri ambayo inatupatia mwangaza kidogo katika hili la chanzo cha Mungu kulingana na kwamba hadithi hizi zimekuwapo miaka maelfu kabla ya ujio wa maandiko ya dini za kileo...

Wakati Neb-er tcher akibadilika kuwa Khepera dunia ilikuwa bado haijaumbwa.
Hapa unasema dunia ilikuwa bado haijaumbwa.
Kwa hali iliyoonekana ni kuwa kwa wakati huo kulikuwa na maji mengi sana ambayo yalitanda juu ya uso wa ulimwengu au dunia nzima ya wakati huo iliyoitwa NU,
Kama Dunia ilikuwa bado haijaumbwa, Hayo Maji yalitoka wapi?
na uwezekano ni kuwa ndani ya bahari hii ndipo mabadiliko yalikochukulia nafasi.
Bahari hiyo iliumbwa na nani?

Au ilitoka wapi?
Ndani ya bahari hii kuu kulikuwamo na chembe chembe za uhai wa viumbe wote ambao nao baadae walikuja kuvaa uhusika wa viumbe mbingu na ardhi. Lakini kwa nyakati hizi waliishi katika hali ya utepetevu na kutojiweza.

Kutoka ndani ya bahari hii kubwa ndipo Khepera alikojiinua,
Bahari hiyo ilitoka wapi?
hivyo akafahulu kupita hali ya utepetevu na ajizi (state of passiveness and inertness) mpaka katika kutenda.

Pindi Khepera alipokuwa katika hatua za kujiinua kutoka katika lindi kubwa la maji alikumbana na hali ya sintofahamu baada ya kujikuta katika sehemu ya utupu wa space pasipo hata na mahali pa kukanyaga/kujitegemezea...
Hizi zote ni Hadithi za kusadikika sawa na Hekaya za Abunuwasi au riwaya za Alfu Lela ulela.
 
Kumbe hizi story za Mungu zilianza zamani Kabla ya wayahudi
Yap, hadithi hizi ni za kale zaidi kabla ya maandiko ya biblia na quran, na inaaminika kuwa maandiko tunayosoma hivi sasa yakiwa na character tofauti na wale original wa kwenye papyrus, yalitooa sehemu kubwa ya maandiko hayo kutoka katika vyanzo vya hadithi za kale za miungu ya kimisri.
 
Hapa unasema dunia ilikuwa bado haijaumbwa.

Kama Dunia ilikuwa bado haijaumbwa, Hayo Maji yalitoka wapi...
Usiwe mwepesi wa kukimbilia hitimisho bali ruhusu akili yako kuwa na subira na jaribu kudadisi, hapa sijawasilisha andiko hili ku-clear kuwa kinachoelezewa katika masimulizi haya ni kweli 100%,

bali hii ni katika kusakafia KNOWLEDGE GAP katika biblia na quran ambazo hazituelezi kabla ya Muumba au Neno kutamka na vikatokea vilivyotokea yeye alikuwa wapi..nadhani mpaka hapo utakuwa umeelewa uzi unazungumzia nini.

Nilijibu sasa swali lako linalouliza je hiyo Nu (bahari kuu) iliundwa na nani, kwa mujibu wa maandiko hapo juu; maji hayakuumbwa na Mungu Khepera bali akiwa bado kama roho (Neb-er tcher) naye kama tulivyokuwa sisi (ndani ya maji yale kulikuwa na chembechembe za uhai wa viumbe wote) humo ndani ya maji tulikuwa kwenye hali ya koma/kupooza mpaka pale yeye roho yake ilipoweza kujinasua katika ile koma na kupanda juu ya maji ndipo yakatokea yote hayo aliyoyafanya kutokana na ufahamu wake huo mpya akiwa ndani ya ile roho kuu ya Neb-er tcher.

Hii inatupa taswira kuwa inawezekana nguvu ya kiroho isiyo na mipaka yaani Neb-er tcher ndiye Mungu mwenyewe ambaye aliumba hiyo bahari na uhai ndani yake kwa ajili ya kujituliza humo, mpaka pale nguvu hiyo ilipoamua kutoka katika utulivu wake na kuinua nafsi moja ili ipate kuvaa form/umbile jingine la umwili (Mungu Khepera) ndipo itaji la kuunda nchi kavu likaja na ndiyo ukawa mwanzo wa ulimwengu wote kuumbwa na viumbe hai vyote kusisimuliwa kutoka katika hali yake ya utulivu kwenda kwenye vibration (uhai) .
 
Everything ni uongo uongooo tu
Bado tunajitafuta tumetokea wapi lakin kamwe hatutapata majibu cos hata sis huwepo wetu hapa ni uongo uongoo
Heri kujitafuta kuliko kujikatia tamaa au kuruhusu akili zako zigote katika shauri la haiwezekani, wakati umri ni kijana na shule ulipelekwa na wazazi masikini na jamii ikakulea ili mwisho uisaidie pengine hadi taifa bado linakudai mkopo wao ulionufaika nao.

Ikiwa wengine waliweza kutafiti na kuandika mapokeo hayo na yakakubalika na jamii japo bado yameacha maswali mengi, kwanini wewe usijaribu kufanya tafiti kuweza kuyajibu hayo maswali hili kukamilisha walichokianzisha wao badala ya kuwakosoa au kujiridhisha kuwa kila kinachoongelewa tusichokuwa na uthibitisho nacho au ambacho ufahamu wetu bado haujafikia katika level ya kuweza kuki-digest na kukielewa ni nonsense?
 
SEHEMU YA PILI

SIMULIZI ZA UUMBAJI ZA BABELI

Kama ilivyoandikwa na baadhi wa waandishi wa mambo ya kale katika vitabu vyao, ningependa nimtumie zaidi mwandishi Budge E.W katika kitabu chake cha "The Babylonian legends of the creation" ambaye ameweza kuelezea kinaga ubaga kuhusiana na mapokeo haya.

Mtizamo na imani ya Wababeli na Waashuri (Assyrians) kuhusu uumbaji ilivumbuliwa kwa mara ya kwanza na Layard A.H etal na kuhifadhiwa huko kunako makumbusho ya uingereza.

Mabaki hayo ni miongoni mwa mabaki ya ikulu yaliyotokea katika maktaba yake huko Ashur-ban-pal (waashuru) B.C 668-626) mahali pajulikanapo kama Kuyunjik (Nineveh)

Bila shaka wengi wetu tumewahi kukutana na maandiko mbalimbali yaliyoandika habari nyingi kuhusiana na viumbe marduk, enlil, enki, anunnaki n.k lakini chanzo cha masimulizi haya na uwepo wake ukawa ni kitu kigeni kwetu.

Naam nikuondoe shaka kuwa kupitia hapa utapata kufafanuliwa kwa ufupi mpangilio wa matukio hayo na tablets zake ili iwe rahisi kuelewa nini kilitokea katika zama hizo za wahenga wa kibabeli.

Cha kwanza kabisa tunapaswa kuzingatia hili kabla ya kuendelea, kuwa historia ya Babeli kwa kiasi kikubwa inazungumzia zaidi, kutukuzwa kwa MARDUK;mtoto wa Ea (Enki), kama shujaa aliyemshinda au conqueror wa joka Tiamat na siyo historia ya uumbaji wa mbingu, dunia na wanadamu.

Uumbaji uliozungumziwa hapa ni ule wa Marduk katika Sixth tablet na Seventy tablet ambao umejikita zaidi katika kuelezea wasifu wa kutisha wa Marduk.

Historia inaonesha kuwa Marduk alipandishwa juu ya miungu wengine kisifa wa babiloni kwa ajili ya maslahi mapana ya kisiasa ila shujaa wa kwanza wa miungu hiyo alitambulika kama ENLIL (BEL), Mungu mkuu wa Nipa (Nippur) utambulika pia kama Nafar au Nufar katika maandiko ya kiarabu, na ya kwamba katika nyakati zile babiloni ilipoinuka katika utawala wa awamu (dynasty) ya kwanza yapata miaka 2300B.C, nafasi yake mhenga huyu ikapata kupitwa (kutwaliwa) na Marduk wa Babeli.

Katika jumbe za uumbaji wa kibabeli uhusisha miungu watatu; Enlil au Marduk au Ashur. Wahenga wa Gilgamish (Second tablet) ni miungu ya kike ya Aruru aliyeumba Enkidu (Eabani)kutokana na kufinyanga udongo wa mfinyanzi kwa mate yake.

Na katika kile kiitwacho "bilingual" toleo la uumbaji wa kihenga tunapata maelezo kuwa Mungu huyu Mwanamke alimsaidia Marduk sawia katika uumbaji wa uhai wa binadamu.

"The Bilingual" toleo la uumbaji la wahenga, Nanukuu "...All the lands were sea 11. "At the time that the mid sea was (shaped like) a trough, 12. "At that time Eridu made, and E-sagil was built, 13. "The E-sagil where the midst of the Deep the god lugat-dul-azaga dwelleth, 14. "Babylon was made, E-sagil was completed, 15. The gods of the ANUNNAKI he created at one time,16. "They proclaimed supreme the holy city, the dwelling of their heart's happiness.

17. "Marduk laid a rush mat upon the face of the waters, 18. "He mixed up earth and moulded upon the rush mat, 19. "To enable gods to dwelling the place where they fine would be.

20. He fashioned Man. 21. "The goddess Aruru with him created the seed of Mankind.

22. "He created the river idiglat (Tigris) and the river purattu (Euphrates) and he set them in their places..."

Tugeukie sasa katika tafsiri nyingine iliyoandikwa na mgiriki BEROSUS, Mtawa wa BEL-MARDUK huko Babiloni, miaka 250 B.C "Kuna kipindi katika historia ambapo hakukuwepo na chochote kile isipokuwa giza na lindi la maji, ambamo ndani yake iliishi viumbe vyasiri (hideous), ambao walitokana na kanuni ya two-fold.

Pale wakatokea binadamu ambao walikuwa wameambatanishwa na mabawa mawili, wengine manne, pamoja na sura mbili. Walikuwa na mwili mmoja lakini vichwa viwili; kimoja cha Mwanamke na kingine cha Mwanaume. Vivyo hivyo katika viungo vyao vingine vingi. Maumbile mengine ya binadamu yalionekana kuwa na maumbile ya nusu-mtu-nusu-mnyama kama vile farasi, mbwa, ng'ombe n.k mfano wake ni umbo la nyota ya hippo-centaurs.

TUKIO LA KUCHINJWA KWA MALKIA WA KUZIMU (ABYSS)

Mtu aliyeongoza juu yao, alikuwa Mwanamke aitwaye OMUROCA; ambaye katika lugha ya kichaldeans uitwa THALATH. Kigiriki ni THALASSA, Bahari. Lakini kwa tafsiri nyingine sawia umaanisha pia mwezi.

Wakati vitu vyote vikiwa katika hali hiyo, Belus alikuja na akamkata Mwanamke pasu katika vipande viwili (asunder); na nusu yake (Mwanamke) ikaunda dunia na nusu yake iliyobakia ikaunda mbingu na wakati huo huo nguvu hiyo ikaharibu ile hali ya unyama ndani yake.

NB: Haya yote yanayozungumziwa ukichunguza kwa lugha ya ishara ni kielelezo cha maumbile ya kimazingira.

UUMBAJI WA MTU

"Kwa ajili ya ulimwengu mzima kuwa na unyevu-unyevu na wanyama kukua ndani yake, ilimbidi miungu (deity) aliye juu yake kujikata kichwa chake mwenyewe. Ambapo miungu wengine walichanganya damu hiyo wakati ikifuka nje pamoja na udongo na kutokana na hapo ndipo binadamu akaumbwa. Kwa sababu hii wao (binadamu) ni wenye akili timamu na wanashiriki ujuzi wa kiungu.

BELUS ANAUMBA ULIMWENGU

Huyu Belus, ambaye uakisi sifa ya sayari ya Jupita, aligawa usiku, akagawa mbingu na dunia na akapunguza order ya ulimwengu. Lakini wanyama ambao hawakumudu tokeo la uwepo wa mwanga walifariki.

Kutokana na tukio hili Belus akabaini uwepo wa nafasi kubwa sana iliyobakia bila viumbe au chochote, sasa kupitia hapo ndipo alipotoa amri kwa miungu kukata kichwa chake na kichanganywe na damu pamoja na udongo na kutokea pale waumbwe binadamu wengine na wanyama, ambao wataweza kuishi kwa hewa.

Belus pia alihusika na kuunda nyota, jua na mwezi pamoja na sayari zingine tano za nyakati hizo. "Hii ni kwa mujibu wa Mwanahistoria Alexander, na hiki ndicho BEROSUS alichotupatia katika kitabu chake cha kwanza."

THE SEVENTH TABLET OF CREATION

Hapo mwanzo hakukuwepo na chochote isipokuwa APSU; ambayo tunaweza kuielezea kama kitu kisicho na ukomo, maji mengi yasiyoweza kuelezeka; ni kwa jinsi gani yaliweza kutokea hilo hakijulikani. Kutoka katika maji haya tunapata mjumuisho wa viumbe, yaani mapepo (demons) na miungu.

Mapepo walikuwa na maumbile yaliyojificha (hideous) ni kama BEROSUS alivyosema; kuwa walikuwa na maumbile ya nusu mnyama, nusu mijusi (reptilia) na nusu binadamu.

Lakini miungu wao walikuwa na maumbile mazima yaliyokamilika bila kuchanganyika, na katika lugha ya alama au ishara kitendo hiki umaanisha matabaka matatu ya Dunia; yaani Mbingu au Anga, Angahewa (atmosphere) na Kuzimu (underworld).

Muunganiko wa Angahewa na Kuzimu vikapelekea kuunda dunia inayotazamana na anga au mbingu.

Andiko linatanabaisha kuwa miungu wawili waliotengenezwa kabla, walikuwa LAKHMU na LAKHAMU. Na baadaye wakafatiwa na miungu ANSHAR na KINSHAR "host of heaven" na baadaye "host of earth."

Baada ya kipindi kirefu katika muda usiyoweza kuelezewa ndipo wakaja kuwepo miungu ya Kibabeli (Babylonian Pantheon) mfano, ANU, EA (Enki), ambaye aliitwa NUDIMMUD, na wengineo.

Punde tu miungu ilipojitokeza katika ulimwengu "Order" ikaanza kuwepo. Pale ''APSU'', kiwakilishi cha maji mengi yasiyoelezeka, alipoona uwepo wa "Order" ilimbidi kushauriana na mshirika wake Mwanamke TIAMAT.

Ili waweze kupata namna ya kuuvuruga au kuharibu "Way" (al-ka-at) au "Order" ya miungu. Bahati nzuri Wababiloni na Wasiriya (Waashuru) wameweza kumzungumzia kinaga ubaga huyu Mungu TIAMAT kwenye maandiko yao.

Tiamat ni Mungu Mwanamke aliyekuwa ni monsta mwenye hasira na wakuogopesha mara nyingi aliweza kubadilika na kuwa katika umbile la nyoka mkubwa na wakati mwingine mnyama.

Pia Tiamat alikuwa ndiye "Mama wa kila kitu" na mmiliki wa DUP SHIMATI au "TABLET OF DESTINIES."
 
Muumba ndiye CHANZO HALISI hana mwanzo wala mwisho, hana dini wala dhehebu na ni mmoja tu na hagawanyiki.

Yesu aliwaambia wayahudi kwa uchache kwamba mnaabudu msichokijua katika Yohana 4:20 lakini hakufafanua kwa wakati ule adi now wengi walikuwa wanaabudu wasichokijua.
 
Muumba ndiye CHANZO HALISI hana mwanzo wala mwisho, hana dini wala dhehebu na ni mmoja tu na hagawanyiki.

Yesu aliwaambia wayahudi kwa uchache kwamba mnaabudu msichokijua katika Yohana 4:20 lakini hakufafanua kwa wakati ule adi now wengi walikuwa wanaabudu wasichokijua.

Sasa wewe umejulia wapi ukweli huo na ukajiridhisha kuhusiana na huyo CHANZO HALISI ikiwa hata Yesu mwenyewe unakiri kuwa hakuwahi kuwafafanulia Wayahudi juu ya yule wamwabuduye?
 
Sasa wewe umejulia wapi ukweli huo na ukajiridhisha kuhusiana na huyo CHANZO HALISI ikiwa hata Yesu mwenyewe unakiri kuwa hakuwahi kuwafafanulia Wayahudi juu ya yule wamwabuduye?

Kwakuwa CHANZO HALISI mwenyewe amekuja kutufafanulia kama alivyosema katika Mika 1:2-6
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom