Chaguzi ndogo zinavyoiweka ccm uchi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Chaguzi ndogo zinavyoiweka ccm uchi

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by MASEBUNA, Mar 11, 2012.

 1. M

  MASEBUNA JF-Expert Member

  #1
  Mar 11, 2012
  Joined: Oct 9, 2011
  Messages: 243
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  KAMA kuna kitu kinachokitesa Chama Cha
  Mapinduzi (CCM) kwa sasa basi kitu hicho ni
  chaguzi ndogo za majimbo. Chaguzi hizo
  zinaivua CCM nguo na kuiweka uchi. Lakini kwa vile chaguzi hizo kwa namna moja
  au nyingine zimeushikilia uhai wa chama
  hicho ndipo kinapojikuta hakina ujanja
  isipokuwa kukubali kuchagua moja kati ya
  mawili. Mosi, kuficha uchi na kukubali kufa kwa
  kuogopa fedheha au kujiweka uchi ili kila
  mmoja ayaone maradhi yanayokisumbua
  chama hicho katika jitihada za kuulinda uhai
  wake. Imesemwa mpaka na makada wakubwa wa
  chama hicho, na inajionyesha wazi kwa kila
  mmoja kwamba makosa yaliyofanyika ndani
  ya CCM yamekiondolea chama hicho mvuto
  kwa wananchi. Kwa kuukubali ukweli huo
  mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, akatangaza mkakati aliodhani ungeweza
  kuurudisha mvuto wa chama kwa wananchi. Akasema ni lazima chama kijivue magamba.
  Mpaka hapo mwenyekiti alikuwa amekiri
  kwamba chama chake kilikuwa nayo matatizo
  makubwa, ambayo yeye aliamua kuyaita
  magamba kwa lugha ya kisanii. Bila shaka Mwenyekiti Kikwete alikuwa na
  imani kwamba kauli hiyo ya kuikiri dosari
  ndani ya chama chake na kuahidi
  kuishughulikia ilitosha kuwarudishia imani
  wananchi kwamba chama hicho sasa ni safi
  hata kabla ya kuuona utekelezaji wa ahadi hiyo. Kwamba wananchi wangekubali
  kumnunua mbuzi kwenye gunia. Ila baadhi yetu tuliichukulia kauli ya JK ya
  kujivua gamba, kama dawa ya kutuliza
  maumivu tu kwa mgonjwa anayesumbuliwa
  na saratani bila kukigusa kiini cha tatizo
  ambacho ni saratani yenyewe. Matatizo yanayotajwa kwenye Chama Cha
  Mapinduzi ambayo yameshamiri na kuanza
  kukitenga chama hicho na wananchi, kama
  vile rushwa, ufisadi wa aina mbalimbali,
  mmomonyoko wa maadili, myeyuko wa
  uzalendo kwa nchi nakadhalina, ni matatizo yaliyokwishageuka saratani. Kwahiyo si rahisi kuyaondoa matatizo hayo
  kwa ahadi tu ya kujivua gamba. Maana
  kawaida ya saratani ni lazima iondoke na
  baadhi ya viungo kama imewahiwa
  kugundulika na kuonyesha dalili za kuponyeka
  na kuunusuru uhai. Wasiwasi nilio nao ni kwamba kitu hicho
  hakijapata ujasiri wa kukimudu ndani ya CCM
  ya sasa. Kwa sasa ni vigumu kutenganisha rushwa na
  CCM. Pamoja na kanuni ya chama hicho
  isemayo rushwa ni adui wa haki, sitatoa wala
  kupokea rushwa, ni mwana CCM gani
  anayeweza kusimama na kujigamba kwamba
  hajawahi kutoa rushwa katika kuhakikisha usalama wa nafasi yake ndani ya chama? Kama hali iko hivyo unawezaje kuifuta rushwa
  ndani ya CCM ukabaki na CCM iliyo hai? Hiyo
  tayari ni saratani ndani ya chama hicho. Chama ambacho kimeikumbatia rushwa na
  kuifanya ndiyo nyenzo kuu ya mafanikio ya
  kila kitu kinawezaje kuwahakikishia wananchi
  ustawi wao huku haki ya kila mmoja ikiwa
  imezingatiwa? Vilevile inaonekana jinsi chama hicho,
  ambacho mwanzoni kilikuwa cha wakulima na
  wafanyakazi tena kikiwategemea haohao
  kujiendesha, kilivyojigeuza mithili ya jini na
  kuwakumbatia mabwanyenye ambao kwa
  sasa ndio nguzo kuu za chama hicho. Sasa unawezaje kuzitishia nguzo hizo halafu
  udai unakitakia mema chama hicho na mtu
  akuelewe? Hiyo ndiyo inayoonyesha kwamba
  kauli ya kujivua gamba ilitolewa kimzaha bila
  kuupima uzito wa ukweli uliokuwa umebebwa
  ndani yake. Kauli kama hiyo ya kujivua gamba ingeweza
  isihojiwe na wananchi kwa kudhani kwamba
  ingeweza kutekelezeka kama dhamira
  ilivyosikika bila kuonekana na ikizingatiwa
  kwamba aliyetoa kauli hiyo ndiye kinara wa
  chama. Lakini bahati mbaya sasa kauli hiyo imeanza
  kuchokonolewa na hizi chaguzi ndogo na
  hivyo kuonekana kwamba kumbe haikuwa na
  uzito wowote. Uchokonozi huo ulianzia Igunga ambako
  mhimili mmoja wa CCM, Rostam Aziz, baada
  ya kusakamwa sana ndani ya chama chake
  hicho akidaiwa kwamba yeye ni gamba
  lililohitajika kuvuliwa, akaamua kujivua
  mwenyewe bila kusubiri kuvuliwa. Wenzake ndani ya chama wakadhani ni
  masihara kwa vile kauli hiyo ililengwa
  kuyatuliza maumivu bila kutibu ugonjwa,
  lakini walikuwa wamechelewa maana mhimili
  huo ulishauvua hata ubunge uliopatikana kwa
  tiketi ya CCM. Hapo ndipo CCM ikalazimika kubaki uchi kwa
  mara ya kwanza, ikayaweka hadharani
  maradhi yanayoisumbua ikiwa imeutilia
  maanani wimbo ulioimbwa na kada maarufu
  wa chama hicho, John Komba, usemao
  kwamba “mwenye kuficha maradhi kwa aibu au kwa kuogopa fedheha ni lazima kilio
  kitamfichua”. Badala ya CCM kufanya sherehe kushangilia
  kwamba gamba moja limeondoka vikaanza
  kufanyika vikao vya kutafuta namna ya
  kumwangukia Rostam ili akubali kuibeba CCM
  ili iweze kulirudisha jimbo hilo kwenye
  himaya yake. Hebu tujiulize, mpaka hapo tunaonaje? Rostam alikuwa gamba kwa chama au mhimili
  wa chama? Badala yake msemaji wa chama
  ambaye muda wote alikuwa amebeba bango la
  magamba ndiye akaonekana mchafu kwa
  chama na kupigwa marufuku asikanyage
  Igunga kukichafua chama katika harakati za kulirudisha jimbo hilo kwenye himaya kikiwa
  mabegani mwa mhimili wake. Kama nilivyosema awali, chaguzi ndogo
  zinaitesa sana CCM kwa kukilazimisha kubaki
  uchi na kuyaanika maradhi yake. Kwa sasa
  kuna uchaguzi mdogo katika jimbo la Arumeru
  Mashariki kufuatia kifo cha mbunge wa jimbo
  hilo, Jeremiah Sumari (CCM). Tumeona mnyukano ulivyokuwa ndani ya
  chama hicho katika kumpata mgombea wake.
  Hapo kuna mambo kadhaa ya kuyaangalia kwa
  makini ili kuona namna uchaguzi mdogo
  unavyoisulubu CCM. Mpambano mkubwa wa kumpata mgombea
  wa CCM ulikuwa kati ya CCM ikiongozwa na
  mwenyekiti, upande mmoja, na Sioi Sumari
  anayesemekana kusimamiwa na kambi ya
  Lowassa kwa upande mwingine. Ikumbukwe
  Lowassa ni mmoja wa makada wa CCM wanaodaiwa kuwa ni magamba. Kwa hiyo kilichofanyika ni Lowassa kutaka
  kuwaonyesha CCM uwezo wake kwa
  kumpitisha mgombea anayemtaka yeye huku
  chama nacho kikiwa kimejipanga kuizuia
  nguvu ya Lowassa. Lakini mwisho wa yote kambi ya Lowassa
  ikaibuka kidedea kuashiria kuwa yeye bado ni
  mhimili ndani ya CCM na wanaomuita gamba
  wakome. Akaibwaga kambi ya CCM
  ikiongozwa na mwenyekiti! Pamoja na ushahidi wa wazi wa kwamba
  ulichezwa mchezo mchafu wa rushwa katika
  kumpitisha Sioi Sumari kwenye kura za maoni,
  bado vikao vya juu vya CCM vimeshindwa
  kuyabatilisha matokeo hayo, kama ilivyokuwa
  ikifanyika miaka ya nyuma. Vimeamua kuyabariki matokeo ya kura za
  maoni licha ya uchafu ulioambatana nayo.
  Hofu ya CCM ni kwamba uamuzi wowote
  ambao ungekwenda kinyume na matokeo
  hayo machafu ungeweza kukionyesha chama
  njia ya kwendea kuzimu. Hayo ni mateso mengine yanayokikabili chama hicho katika
  hizi chaguzi ndogo. Fikiria, kama chama kinaletewa ushahidi wa
  waziwazi kwamba mmoja wa makada wake
  amekiuka maadili ya chama kwa lengo la
  kujinufaisha yeye binafsi huku akiwa
  amekipaka chama matope, lakini chama
  kikashindwa kumchukulia hatua yoyote kwa kuhofia nguvu iliyo nyuma ya mtu husika. Huo utakosaje kuwa uthibitisho kuwa chama
  hakiko tena kwenye misingi ya maadili yake
  bali kimesimama juu ya nguvu za watu fulani
  waliojigeuza mihimili ya chama hicho hata
  kama watu hao ni wachafu kiasi gani? Jambo jingine linaloshangaza ndani ya CCM,
  kama ambavyo tumekuwa tukionyesha mara
  kwa mara, ni la chama hicho kujiendesha
  kifamilia na kikoo mithili ya ufalme badala ya
  kujiendesha kitaasisi. Mbunge aliyekufa wa Arumeru Mashariki ni
  Jeremiah Sumari. Kabla hata maiti yake
  haijaoza kaburini chama kinamteua mtoto
  wake kuirithi nafasi ya baba yake! Nani
  kasema kwamba ukoo wa Sumari ndio pekee
  unaopaswa kutoa mbunge wa Arumeru Mashariki? Mimi naamini kwamba Sumari kaacha mali
  nyingi alizowarithisha wanae, lakini ubunge si
  kati ya mali hizo. Ubunge ni mali ya wana
  jimbo wala haikuwa mali yake. Kwa hiyo wana Arumeru Mashariki ndio
  wanaotakiwa kuelewa mali hiyo wampatie
  nani bila kuangalia anatoka ukoo gani. Ila niwatahadharishe wana Arumeru Mashariki
  kwamba kutoa nafasi hiyo kwa zaidi ya mtu
  mmoja ndani ya familia moja ni kutengeneza
  aina fulani ya ufalme ambapo wananchi
  wengine watakuwa wamejitenga kabisa na
  nafasi hiyo ya uwakilishi wa wananchi. Tukirudi kwenye utata wa maamuzi ya CCM
  tunapata tetesi kwamba mwenyekiti mstaafu,
  Benjamin Mkapa, ndiye kapewa jukumu la
  kuhakikisha chama hicho kinaibuka mshindi
  katika uchaguzi huo mdogo. Lakini ni CCM hiyohiyo ambayo katika
  mkutano wake wa Halmashauri Kuu
  uliofanyika majuzi kule Dodoma, imefikia
  uamuzi wa kuibadili katiba yake ili kuwaondoa
  viongozi wastaafu katika NEC na badala yake
  kuwaundia chombo kingine ambacho bilashaka kitakuwa hakileti vikwazo katika maamuzi
  ambayo wazee hao wasingeyaafiki. Wastaafu wameenguliwa kwenye maamuzi na
  kufanywa washauri. Lakini walio katika
  maamuzi wakisha boronga wazee walio katika
  ushauri waitwe haraka kuokoa jahazi! Pamoja na hiyo ikumbukwe kwamba mng’ao
  wa CCM ulianza kufifia wakati wa uenyekiti wa
  Mkapa. Mkapa ni kiongozi aliyepigiwa debe na
  Baba wa Taifa, Julius Nyerere huku
  akiwashangaa waliokuwa wakiitamani Ikulu
  kiasi cha kutoa hata fedha ili wafanikiwe kuingia. Mwalimu Nyerere aliuliza Ikulu kuna biashara
  gani? Kwamba mtu anayetoa pesa kuingia
  Ikulu atazirudishaje? Ndipo Mwalimu
  alipoonya kwamba Ikulu ni sehemu takatifu, si
  mahali pa kufanyia biashara. Lakini haukupita muda mrefu tangu Mwalimu
  alipotutoka tukapata habari kwamba Rais
  Mkapa kasajili kampuni ya biashara kama
  mjasiriamali aliyekuwa akiishi Ikulu! Mkapa
  akaigeuza Ikulu yetu sehemu ya biashara
  akiwa ameisaliti imani aliyokuwa nayo Baba wa Taifa kwake. Baada ya hapo nguvu ya ushawishi iliyokuwa
  nayo CCM kama ile aliyoitumia Mwalimu
  kuwashawishi wananchi ili wamkubali Mkapa,
  ikaporomoka kwa kishindo na kukiacha chama
  hicho kikitegemea mabavu na shinikizo kwa
  msaada wa vyombo vya dola kufanikisha matakwa yake. Ni katika kipindi hicho cha Mkapa, Tanzania
  kwa mara ya kwanza katika historia ya
  ulimwengu, ikazalisha wakimbizi kufuatia
  mauaji yaliyofanywa na vyombo vya dola
  Unguja na Pemba katika CCM kutafuta ushindi
  kwa mabavu. Kwahiyo ikiwa Mkapa atajitokeza kuifanyia
  kampeni CCM Arumeru Mashariki itabidi
  wananchi wamuulize maswali hayo. Hata
  kama hakutatolewa fursa ya kumuuliza moja
  kwa moja, nina imani hakuna atakayeweza
  kuyazuia maswali hayo yasiulizwe kimoyomoyo. Mkapa aulizwe ni kitu gani kilichosababisha
  uadilifu ndani ya chama chake kumomonyoka
  kiasi cha kumfanya yeye akiwa kiongozi
  mkuu wa chama na kiongozi wa nchi kuamua
  kuigeuza Ikulu yetu, ambayo aliambiwa na
  Mwalimu wake kuwa ni sehemu takatifu, pango la ulanguzi? Aulizwe ulikokwenda ushawishi wa CCM
  ambao nafasi yake imechukuliwa na shinikizo
  la kutumia mabavu kwa vitisho. Maana ni katika kipindi cha Mkapa tulipoanza
  kushuhudia kampeni kama hizo za uchaguzi
  zikiendeshwa kwa mtindo wa kivita kwa
  kutumia vyombo vya dola badala ya
  kuwashindanisha makada wa vyama kumwaga
  sera kwa wananchi. Mkapa pia aulizwe CCM kina uhalali gani wa
  kuendelea kuaminiwa na Watanzania katika
  ujumla wao iwapo wanachama wake
  hawaaminiani tena wala kukiamini chama
  chao? Suala la wana CCM kutishiana maisha kiasi cha
  makada wake wa ngazi za juu kutoleana
  shutuma za kulishana sumu na mambo
  mengine machafu na ya hatari linawezaje
  kukifanya chama hicho kiendelee kuonekana
  ni tegemeo la Watanzania? Aulizwe kwamba CCM imegeuka chama cha
  kifalme? Vinginevyo aeleze inakuwaje chama
  kinajishughulisha na namna mtu atakavyorithi
  nafasi ya baba yake, kitu kinachohamisha
  shughuli za chama, kama taasisi ya ki-nchi, na
  kukifanya chama kionekane kinashughulikia mirathi ambayo inapaswa kuwa shughuli ya
  kifamilia.
   
 2. Losambo

  Losambo JF-Expert Member

  #2
  Mar 11, 2012
  Joined: Nov 8, 2011
  Messages: 2,623
  Likes Received: 8
  Trophy Points: 0
  Ilipofika CCM ni point of no return, inakwenda kuzama na makundi yake na siku yakizama makundi hayo yatabaki kulaumiana tu maana hawajui mchezo wanaoufanya hatma yake ni nini.
   
 3. jogi

  jogi JF-Expert Member

  #3
  Mar 11, 2012
  Joined: Sep 25, 2010
  Messages: 19,335
  Likes Received: 12,800
  Trophy Points: 280
  Masebuna umechambua vizuri sana! wakisoma robo yao watapata shinikizo la damu, chapisho linaweza kutengeneza by election kadhaa!!!
   
 4. M

  Mr.Busta JF-Expert Member

  #4
  Mar 11, 2012
  Joined: Mar 24, 2011
  Messages: 672
  Likes Received: 3
  Trophy Points: 35
  uchambuzi mzuri sana! Big up!
   
 5. Head teacher

  Head teacher JF-Expert Member

  #5
  Mar 11, 2012
  Joined: Mar 10, 2012
  Messages: 1,811
  Likes Received: 7
  Trophy Points: 0
  Ina maana SIOI ndi msimamizi wa mirathi ya baba, wamechemk, rithi mali si madaraka
   
Loading...