Chadema yawashukia Membe, Simba

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
Chadema yawashukia Membe, Simba Monday, 14 March 2011

chademamnyika.jpg
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika






















Chadema kinaandaa hatua za kisheria za kumchukulia Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba kwa kauli zake ambazo amekuwa akizirudia rudia kwamba chama hicho kimekuwa kikifadhiliwa na balozi tano za nchi za Ulaya ili kufanya maandamano ya kuvunja amani nchini.

Pia chama hicho kimemtaka Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikino wa Kimataifa, Bernard Membe kuzitaja balozi hizo zinazofadhili chama hicho na kiasi cha fedha kinachotolewa.

Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mnyika katika mkutano wake na wanahabari.

Mnyika alisema Simba amekuwa akinukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba maandamano ya Chadema ambayo yalikuwa yakifanyika katika Kanda ya Ziwa yamekuwa yakifadhiliwa na Balozi za nchi za Ulaya.

“ Lakini jana (juzi) Waziri Membe aliulizwa kuhusu kuwapo kwa tuhuma za Balozi za Ulaya zinazowakilisha nchi zao hapa nchini kikifadhili chama kimoja cha siasa bila kukitaja, akajibu kuwa anafahamu suala hilo na vyombo vya usalama vinachunguza,”alisema Mnyika.

“Kwa kuwa Waziri mwenzake Simba alishakitaja chama chetu kuwa ndicho kinachofadhiliwa na nchi za Ulaya ili kufanya maandamano ya kuvunja amani, tunaomba sasa azitaje nchi hizo na fedha zinazotolewa,”alisema Mnyika na kuongeza.

“Hakuna sababu kwa Waziri Membe kukaa kimya kuhusu tuhuma zinazofahamika ambazo Waziri mwenzake amekwishaweka hadharani, aueleze umma ili Balozi hiyo ziweze kueleza kuhusu tuhuma hizo,” alisema.

Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema chama hicho hakipewi ufadhili wowote kutoka nje ya nchi kwa lengo la kufanya maandamano ya kuvunja amani.

“Maandamano yale na mikutano ni ya wananchi, wamehamasika baada ya Serikali yao kushindwa kuwatekelezea mahitaji yao muhimu,” alisema.

Aidha, alisema wananchi wanaohudhulia maandamano hayo hawalipwi, wanahamasika baada Serikali yao kushindwa kutekeleza ahadi zake.

Aliongeza kuwa Serikali baada ya kujikita katika kutatua kero za wananchi, wanajikita kwenye propaganda ambazo zitapaswa kufanywa na CCM.

“Mwanzo walieneza propaganda kwamba chama chetu ni cha kikabila wananchi wakapuuza, baadaye wakasema kina udini wakapuuza, sasa wanasema kinapata ufadhili kutoka katika balozi,”alisema.

“ Kutokana na kauli za Waziri Simba, sasa wanasheria wa chama Tundu Lisu na Mabere Marando wanaandaa taratibu za kisheria za kumchukulia,” alisema.

Alisema wanasheria hao wakishaandaa hatua za kuchukua, waandishi wa habari watafahamishwa.

Wakati huo huo, Mnyika amesema kwa mujibu wa ratiba ya chama hicho, baada ya kumaliza mikutano katika Kanda ya Ziwa, kitaelekea katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

“ Ingawa bado haijafahamika ni lini ratiba hiyo itaanza, itajulikana baada ya viongozi wakuu wa kitaifa watakaporejea nchini kutoka Liberia wanakohudhuria mkutano wa vyama vya siasa,” alisema
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom