Taarifa kutoka Ngara:
Source Radio Kwizera 26.09.2011
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kinawashukuru sana wananchi wote wa wilaya ya Ngara waliojitokeza kwa wingi wao katika mapokezi ya mwenyekiti wa Mkoa wa chama hicho mheshimiwa Wilfred Lwakatale hivi karibuni. Pia kimewataka wananchi wa Ngara ambao tayari wameonesha shauku kubwa ya kujiunga na CHADEMA kuongeza kasi ya kufungua matawi kila kijiji ili kujiandaa kuleta mabadiliko ya kweli na uhuru wa kweli katika wilaya yao.
Hayo yalisemwa na ndugu John Malanilo, mjumbe wa kamati tendaji ya wilaya ya Ngara (CHADEMA) wakati kamati tendaji ya wilaya ya Ngara ilipokwenda kufungua tawi la CHADEMA kijiji cha Nyakafandi kata ya Mganza. Pamoja na hayo aliwashukuru pia wanachama wa chama hicho, wapenzi na wanaharakati katika kuchangia gharama za kuendesha chama wilayani Ngara.
Aliongeza kuwa CHADEMA kimejizatiti kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na wanachama na uongozi kwa vile wananchi wana shauku kubwa kuona chama kinawafikia. Akifafanua, alisema kuwa shauku ya wananchi kujiunga na CHADEMA inatokana na kuwa wananchi wameona kuwa Chama Cha Mapinduzi hakiwezi tena kuwaletea wananchi maendeleo na kwa Hiyo CHADEMA ndiye mkombozi wao.
Ndugu Malanilo alisema kuwa tayari maandalizi ya kufungua matawi ishirini kabla ya mwisho wa mwezi wa tisa yamekamilika na amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi wakati matawi yatakapokuwa yanafunguliwa.
Source Radio Kwizera 08.09.2011
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimezidi kuchota wanachama kutoka chama cha mapinduzi, CCM na vyama vingine vya siasa baada ya kupokea wanachama wapya 83 katika kijiji cha Kihinga kilichopo kata ya Bugarama, wilayani Ngara. Tukio hili limetokea mwishoni mwa wiki wakati mwenyekiti wa baraza la vijana wilaya ya Ngara Mheshimiwa Nestori mashishanga alipokuwa anafungua tawi kijijini hapo.
Wananchi zaidi ya mia mbili walijikusanya kushuhudia kupandishwa kwa bendera ya CHADEMA kijijini hapo ambayo ni ya kwanza tangu kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini Tanzania. Akiongea na wananchi hao, alisema kwa mara nyingine wananchi wamethibitisha kupenda CHADEMA na kufanya maamuzi magumu ya kukihama chama cha mapinduzi na kujiunga na CHADEMA. Katika tukio hilo, mwenyekiti wa baraza la vijana alipokea pia kadi 39 kutoka kwa wanachama wa CCM ambao walijiunga na CHADEMA. Katika tukio hilo pia uongozi wa wilaya uliunda uongozi wa tawi la kihinga wa CHADEMA ambapo mwenyekiti alichaguliwa kuwa Elias Deus, katibu Jerome wabandi, Katibu mwenezi Jeremia Gabriel na mwekahazina ni Dioniz Bujana.
Naye mwenyekiti wa baraza la wazee wilaya ya Ngara, mheshimiwa Sebastian Mbonye aliwaambia wanachama wapya kuwa kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992, kila mtanzania mwenye umri wa kuanzia miaka 18 au zaidi ana uhuru wa kujiunga na chama chochote cha siasa na hakuna kiongozi yeyote wa chama au serikali mwenye mamlaka kuhoji maamuzi hayo ya kujiunga na CHADEMA. Akiwasifia wanachama kutoka CCM ambao pia wameshusha bendera za CCM na kupandisha za CHADEMA alisema kuwa hiyo ni sehemu ya ukomavu wa kisiasa lakini wasiwe na wasi wasi kwa sababu hiyo ni sehemu ya matakwa ya sheria na hakuna wa kuwabugudhi.
************ Mwisho***************
CHADEMA Vema
Hakuna kulala mpaka kieleweke
Nitazidi kuwaletea kadiri habari zinavyotufikia