CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa kitachukua hatamu za uongozi wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa madiwani, ubunge na urais wa mwaka 2015.
Kauli hiyo imetolewa jana na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, katika mkutano maalumu wa viongozi wa Kanda ya Dar es Salaam wa chama hicho, ambapo Dk. Willibrod Slaa alikuwa mgeni rasmi.
Dk. Slaa alisema kwa sasa chama hicho kimeanza kuandaa mikakati mizito yenye mbinu za kisasa na za uhakika ili kiweze kushinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ambayo hata hivyo, hakuweza kuitaja.
Hata hivyo, aligusia kuwa hivi sasa chama hicho kimefanya marekebisho ya ratiba ya uchaguzi wake wa ndani, ili kuweza kujipanga vizuri kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Nimetoa waraka wa kufanya marekebisho ya ratiba ya uchaguzi ndani ya chama. Badala ya kufanyika kila baada ya miaka mitano ambayo huwa karibu na mwaka wa Uchaguzi Mkuu tumerudisha nyuma, hivyo chaguzi ndani ya chama zitaanza mwakani katika ngazi mbalimbali na kukamilika mwaka 2013.
Tunaamini tukifanya uchaguzi mapema tutaweza kumaliza makovu ya uchaguzi huo, hivyo kuingia katika Uchaguzi Mkuu tukiwa kitu kimoja, alisema Dk. Slaa.
Alisema sasa CHADEMA kimepokewa vema na kukubalika kuwa chama cha Watanzania wengi, hivyo ni muhimu viongozi kuanza kufikiri tofauti, ili waendane na matakwa ya wananchi.
CHADEMA ni tumaini jipya, hivyo haiwezi kuwa na mbinu zilezile zilizotumika mwaka 2010, hivyo viongozi hamtakiwi kuacha fikra kwa ngazi moja. Fikra za mbinu mbalimbali zinatakiwa zitoke kuanzia ngazi ya kata, wilaya, mkoa na hata taifa, kwani tunahitaji mabadiliko ya kifikra, alisema.
Aiwataka viongozi hao kusambaza waraka huo kwa wanachama na kufanya kazi ya kuwaelimisha. Aliongeza kuwa kiongozi atakayeshindwa kufanya hivyo atakuwa ameshindwa kwenda na kasi ya chama hicho.
Muda wa kubebana sasa umekwisha, atakayeshindwa kutekeleza haya itafika mahala tutachapana, ni lazima waraka huo ufike chini kwa wananchi. Nitapita eneo kwa eneo kuhakikisha kama hilo limefanyika na kwa watakaoshindwa kufanya hivyo nitatumia katiba kuwaondoa na kuwaweka viongozi wa muda. Hatuwezi kuendelea na viongozi wa aina hii, alisema Dk. Slaa huku akishangiliwa na viongozi hao.
Dk. Slaa aliwataka viongozi hao kukutana naye Januari 5, mwakani ambapo watatoa taarifa ya utekelezaji wa waraka huo pamoja na ushahidi.
Chama si kitu cha mchezo. Watu tunahangaika nchi nzima na tumeweka rehani maisha yetu, wengine mnakaa tu, nawaambieni sasa tutachukua maamuzi magumu, alisema.
Alisema chama hicho kitaweza kufanikiwa zaidi iwapo watainua sauti za wanyonge, hivyo viongozi wabadilike katika utendaji kazi.
Dk. Slaa alisema CHADEMA kinatarajia kutumia njia ya database kuwasiliana na wanachama wake kama walivyofanya viongozi wa chama hicho mkoani Arusha.
Kwa kutumia mfumo huo, ukituma ujumbe mfupi wa maandishi (sms) moja inaweza kufika kwa wanachama zaidi ya 5,000, hivyo ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kuanzia sasa viongozi kusanyeni namba za wanachama wetu ili tuingize kwenye utaratibu wa aina hiyo,alisema.
Katika hatua nyingine, Dk. Slaa alionesha kukerwa kwake na mgogoro unaotaka kuibuka katika Jimbo la Segerea, huku ikijulikana kuwa aliyekuwa mgombea wao, Fred Mpendazoe, amefungua kesi ya kupinga matokeo ambayo inaendelea vizuri mahakamani.
Segerea nianze na ninyi, nimewapa maelekezo hamjayafanyia kazi. Chama kimetumia sh milioni 12 katika kesi ya kupinga matokeo ya jimbo hilo na inaendelea vizuri, sasa viongozi mmeanza migogoro.
Mmeanza kueleza mabaya ya Mpendazoe. Mpendazoe si mtu wa kawaida. Nawapa wiki mbili mgogoro huo uwe umeisha, kwani ni mgogoro wa kipuuzi, alisema.
Aliwashauri viongozi hao kuanzisha matawi na kusimika mabalozi wa nyumba tano, kwani huo ni mtaji wa kisiasa na kuongeza kuwa ni lazima chama kifanye kazi kisayansi.
Akizungumzia mchakato wa Katiba mpya, Dk. Slaa alisema ni lazima mchakato huo urudi kwa wananchi ili waweze kutoa maoni yao na kuongeza kuwa CCM inahofia suala hilo kwa kuwa hawakubaliki kwa wananchi.
Tukiruhusu Rais Kikwete aunde tume hakuna cha maana kitakachofanyika. Mimi nina uzoefu, nilikuwa mbunge na najua uovu wote na pia nilikuwapo kwenye Tume ya Jaji Kisanga. Wakati ule tume inakusanya maoni, CCM ilituma mawaziri wake waende kwa wananchi na kuwafundisha jinsi ya kujibu hata kabla tume haijaenda, hivyo tume ile iliyoundwa ilikuwa ni geresha tu, alisema.
Alisema rais akishaunda tume wananchi hawana mamlaka, ndiyo maana wanaipinga na kwamba ikiwapo hata maoni yatakayotolewa na wananchi hayatafanyiwa kazi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Ubungo John Mnyika, alisema kinachofanyika sasa ni kuwaelimisha viongozi wao kuhusu sheria ya mabadiliko ya Katiba na baada ya hatua hiyo watakwenda kwa wanachama wa kawaida.
Alimshauri Rais Kikwete asiunde tume ya kukusanya maoni kuhusu Katiba mpya, kwani akifanya hivyo atasababisha mgogoro.
Pamoja na rais kusaini muswada huo tunamshauri sheria hiyo isianze kutumika mpaka yatakapofanyika marekebisho ya msingi. Akiunda tume, hatutashiriki, bali sisi tutakwenda kwa wananchi na kuwaeleza kuhusu jambo hilo, njia tutakazotumia tutazieleza baadaye iwapo jambo hilo litatokea, alisema.
|
|