Wasifu mzito na historia za kutukuka za baadhi ya wateule wanaounda
timu ‘mpya' ya viongozi watendaji wa CCM kwa kiwango kikubwa ndicho
kitu kikubwa pekee kinachosababisha mtu yeyote makini ajikute akipata
shida kuyabeza yale yaliyofanywa na chama hicho tawala mwishoni mwa
wiki kule Dodoma.................absalom kibanda critical thinking
Msuko mpya wa safu ya wakuu wa idara za CCM uliotangazwa na Rais
Jakaya Kikwete ukiwajumuisha wanasiasa wasiojua mizaha wawapo kazini
kama alivyo Philip Mangula, au makada wa muda mrefu wa chama hicho wa
kariba ya Muhammad Seif Khatib na Zakia Meghji una kila sababu ya
kutafutiwa dawa mahususi na makamanda wa kambi ya upinzani ambao kwa
muda mrefu wamekuwa wakipambana kuing'oa CCM madarakani.
Ni mtu asiyejali au mpuuzi asiyezijua vyema siasa za Tanzania
anayeweza akasimama na kuudharau uteuzi uliofanywa na Rais Kikwete
ambaye baada ya kushindwa mara kadhaa hatimaye amefanikiwa
kumshawishi, mmoja wa wanasiasa makini na wakongwe, mtumishi wa umma
wa muda mrefu, mwanadiplomasia na Kanali Mstaafu wa Jeshi,
Abdulrahaman Kinana kuwa Katibu Mkuu wa CCM.