Chadema kuaandamana Jiji la Mbeya

fangfangjt

JF-Expert Member
Apr 25, 2008
571
139
Chadema kuaandamana Jiji la Mbeya

Geofrey Nyang’oro na Ellias Msuya

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kitaendelea na ratiba zake za maandamano na hivi sasa yataanzia jijini Mbeya kwa ajili ya kuwashukuru wananchi kwa kuwapa kura na kushinikiza viongozi wa serikali na CCM kuwajibika kwa wananchi. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe alisema maandamano ni haki na wajibu wa chama cha siasa.

“Maandamano ni haki na wajibu wa Chama siasa na kwa msingi huo Kamati kuu imeiagiza sekretarieti ya kamati kuu ya Chadema kuendelea na maandalizi ya ziara ya kuwashukuru wananchi na maandamano katika Mikoa ya Kanda ya Nyanda za juu Kusini na safari hii, maandamano yatafanyika katika Jiji la Mbeya,” alisema Mbowe.

Kauli ya Chadema inakuja huku maandamano yaliyofanyika katika Kanda ya Ziwa yakishutumiwa na rais pamoja na viongozi mbalimbali kuwa yanahatarisha amani ya Taifa na yana lengo la kuiondoa serikali iliyoko madarakani. Akijibu hoji hizo Mbowe alisema kamwe Chadema haijiwahi na wala haijapanga kuiondoa serikali iliyoko madarakani kinyume na taratibu na kusisitiza wanaotoa kauli hizo wanahofia nafasi zao.

“Kamati kuu ilipokea na kujadili kwa umakini tathmini ya maandamano yaliyofanyika Kanda ya Ziwa pamoja na matamko yaliyotolewa na viongozi wa serikali na CCM wakiwamo Rais Jakaya Kikwete, mawaziri Bernad Membe, Stephene Wassira na Sophia Simba pamoja na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati na kugundua mambo mawili ,”alisema Mbowe.

Alisema kamati kuu ilisikitishwa na kauli za viongozi hao wa serikali na CCM na kwamba kauli hizo zinaashiria viongozi hao hawajui maana na kazi ya vyama vya upinzani. Alisema maandamano katika Kanda ya Ziwa yalifanyika kwa amani na utulivu yalifuata sheria na yaliazimia mambo makuu manne ambayo ni kuishinikiza serikali ya CCM kuachana na mpango wake wa kuilipa kampuni ya Dowans Sh 94 bilioni kufuatia hukumu iliyotolewa na Mahakama ya kimataifa ya Biashara ya ICC na kuishinikiza serikali kumaliza mgawo wa umeme.

Alitaja maazimio mengine kuwa ni serikali kuwawapunguzia wananchi adha ya ugumu wa maisha kwa kupunguza mfumko wa bei, kuhakikisha uchaguzi wa Meya wa Arusha unarudiwa na kutaka Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi anajiuzulu.

“Malengo ya mandamano hayo yalianishwa, kauli ya Rais Kikwete kwamba mandamano yalilenga kuiondoa serikali iliyoko madarakani kwa njia zisizo za kidemokrasia ni uongo na uzishi, wasiwasi na hofu aliyonayo ni kushindwa kwake kutekeleza yale aliyowaahidi wananchi,”alisema Mbowe. Kuhusu maandamano yatakayofanyika kuanzia Mei 4 mwaka huu katika nyanda za juu kusini Mbowe alisema yamelenga kuwashukuru wananchi kwa kura nyingi walizotoa kwa chama hicho, kuendelea kuishinikiza serikali kuchukua hatua za kupunguza adha ya gharama za maisha kwa wananchi.

“Ziara na maandamano ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yatatumika kushinikiza serikali kupunguza bei ya bidhaa muhimu za unga, mchele , umeme, maharage, mafuta na sukari kwa kuwa bidhaa hizi zinatumika kwa wananchi wa kawaida,”alisema Mbowe. Kuhusu mgawo wa umeme kamati kuu ya Chadema imemtaka Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kujiuzulu wadhifa wake kwa kuwa ameshindwa kuitumikia nafasi hiyo ili hatua zaidi ziweze kuchukuliwa.

Alisema sekta ya nishati na madini ukiwamo umeme imegubikwa na ufisadi mkubwa unaowahusisha viongozi wa juu wa serikali tangu mwaka 1991 Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lilipobinafishwa kwa IPTL na kwamba inaendelea kuitafuna nchi hadi leo. Pamoja na kumtaka Waziri huyo kujiuzulu wadhifa wake, Mbowe ambaye ni kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni aliitaka serikali kuacha mpango wowote wa kuingia mkataba na kampuni ya Dowans kwa kuwa kufanya hivyo ni kulifedhehesha taifa.

Kuhusu sekta hiyo ya umeme Mbowe alitoa tahadhari kwa serikali kutoanunua mitambo hiyo na pia kutaka iachene na mpango wa kukodi mitambo ya umeme unaotumia mafuta kutoka Marekani wenye thamani ya Dola za Marekani Sh 260 milioni.
 
Back
Top Bottom