Chadema imedandia behewa la cuf!

Nichangie kuweka kumbukumbu sawa:

Mtoa hoja amedai kuwa CHADEMA ilianzisha M4C mwaka 2011, na kwamba CUF ilianza Vision for Change mwaka 2008 na hatimaye kuanza kuingiza katika ilani yake 2010. Ukweli ni kuwa CHADEMA katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 ilitumia kauli mbiu "Mabadiliko ya Kweli, Uhuru wa Kweli" (Real Change, Real Freedom) na wakati huo kuna maneno tulikuwa tukiyarudiarudia sana kwenye kampeni, mabadiliko ya kweli hayawezi kuletwa na mafisadi walewale, wa chama kile kile, chenye uoza ule ule wakiendeleza yale yale kwa ari, nguvu na kasi mpya. Ilani yetu ya wakati huo iliyokuwa na vipaumbele vichache tulikuwa tukiinadi kuwa ni dira ya mabadiliko ya taifa letu. Mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, nilibahatika kuwa mwezeshaji wa tathmini ya chama baada ya uchaguzi na maandalizi ya Mpango Mkakati wa Chama 2006-2010 ambayo msingi wake mkuu ulikuwa ni kufanya mabadiliko ndani ya chama kama msingi wa kushinda uchaguzi na kuleta mabadiliko makubwa katika taifa.

Kufuatia kupitisha Mpango Mkakati huo tarehe 13 Agosti 2006 tulifanya mkutano mkuu wa chama na kuzindua TUMAINI JIPYA, siku hiyo tulizindua katiba mpya ya chama, bendera mpya ya chama, mabaraza ya chama na mpango mkakati wa chama. Hatua hiyo ilitanguliwa na mchakato wa kukusanya maoni toka kwa wanachama na ngazi za chini za chama na nilibahatika kuwa katibu wa kamati iliyofanya marekebisho hayo ambayo kwa upande wa masuala ya falsafa na itikadi ilikuwa chini ya Profesa Baregu. Kupitia kazi hizo nilizozifanya wakati huo nikiwa pia Mkurugenzi wa Taifa wa Vijana nilipata wasaa wa kuifahamu kwa kina historia ya chama na pia kufanya rejea ya historia ya mageuzi nchini.

Mkakati wa M4C haukuanza mwaka 2011 kama ambavyo CUF inajaribu kupotosha, mwaka 2006 mara baada ya kupitisha mkakati huo wa chama tulianza shughuli mbalimbali za utekelezaji wa mkakati huo, kati ya shughuli hizo wakati huo nikiwa Mkurugenzi wa Vijana wa CHADEMA tulianzisha Y4C (Youth for Change) ikiwa ni kundi la vijana wenye dira na dhima ya kuona mabadiliko katika taifa, tulifanya matukio kadhaa mwaka 2006, 2007 kipindi ambacho CUF haikuwa imezindua Vision for Change. Mwaka 2007, mara baada ya kutoa orodha ya mafisadi (List of Shame) Septemba 15 MwembeYanga tulikaa kutafakari tutaendelezaje vuguvugu la mabadiliko nchini, ni wakati huo likaja wazo la kuwa na Movement for Change (M4C), miezi michache baadaye chama kilifungua akaunti katika benki mbalimbali kwa ajili ya harambee ya kukusanya michango ya umma kwa ajili ya mabadiliko; Akaunti hizo ziliitwa M4C. Mwaka 2008 tukaingia katika uchaguzi wa marudio katika Jimbo la Tarime ya kushinda, baada ya ushindi huo M4C iliendelea kama mkakati wa kukusanya rasilimali za umma kwa ajili ya mabadiliko hata hivyo kwa vuguvugu lililokuwepo wakati huo baada ya ushindi tukaamua kuzindua Operesheni 'Sangara'. Miezi michache baadaye CUF nayo ikazindua Operesheni Zinduka CCM ikaanza Operesheni Nyavu. Mwaka 2009 CUF ilifanya kongamano Diamond Jubilee kuhusu Dira ya Mabadiliko, na ni ukweli katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ilani yake iliita dira ya mabadiliko (Vision for Change) hata hivyo katika uzinduzi huo CUF haikutumia kifupi V4C.

Miezi michache baada ya CHADEMA kuzindua M4C kwa upande wa Arusha, ndipo CUF akatangaza tena Vision for Change safari hii ikitumia pia kifupi cha V4C. Wakati huo CHADEMA ilianza pia shughuli ya "Vua Gamba, Vaa Gwanda", CCM nayo ikaja ".....Vaa Uzalendo". Ni wazi kwamba M4C ni tofauti na V4C, ni wazi pia kwamba M4C ilitangulia V4C; kama ambavyo Operesheni Sangara ilitangulia Operesheni Zinduka. Baada ya uchaguzi wa 2010, watanzania wanaweza kupima vizuri zaidi matokeo ya Operesheni Sangara ukilinganisha na Zinduka, na baada ya uchaguzi wa 2015 watanzania watapima M4C vs V4C vs "Vaa Uzalendo ya CCM". Na kwa kweli, CHADEMA inachotazama zaidi ni kufanya mabadiliko kwa kuiondoa CCM madarakani na kuweka uongozi bora, sera sahihi, mikakati makini na oganizesheni thabiti kwa maendeleo endelevu ya Tanzania. Nikipata wasaa mwingine nitajibu upotoshaji uliojitokeza kuhusu bendera ya CHADEMA, people's power na madai ya katiba mpya kwa kuwa nimepata bahati katika kipindi cha kati ya 2004-2010 kushiriki kwa karibu kwenye michakato muhimu ndani ya CHADEMA na ya kamati za ushirikiano iliyohusisha CUF na vyama vingine. Yote kwa yote, suala la msingi si nani ameanzisha nini, muhimu ni nini kinafanyika kuwezesha mabadiliko ya kweli nchini kwa maslahi ya umma.

JJ

Thats why I respect CDM.Ni kwa ajili ya vichwa kama hivi.
 
Back
Top Bottom