TandaleOne
JF-Expert Member
- Sep 4, 2010
- 1,644
- 709
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu
za rambirambi, akiomboleza kifo cha Miongoni mwa waasisi wa TANU na wazee wa CCM
mkoani Mwanza Mzee Masalu Ngofilo kilichotokea juzi, Jumatano, Aprili 13, 2016 mkoani
Mwanza.
Katika salamu zake za rambirambi kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Ndugu
Anthony Diallo, Dk. Kikwete amesema “Nimeshtushwa mno na taarifa za kifo cha Mzee
Ngofilo. Kwa hakika, ni msiba ulionihuzunisha sana.”
Mzee Ngofilo aliyezaliwa Februari 12, 1935, amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za
uongozi ndani ya CCM na katika michezo nchini ambapo ndani ya CCM amewahi kuwa
Mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Mwanza, Diwani kwa kipindi cha miaka 20, Mjumbe
wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa na Mwenyekiti wa CCM wa iliyokuwa wilaya ya Mwanza na
amefariki dunia kwa maradhi ya shinikizo la Damu na Kisukari.
Dk. Kikwete amemweleza Ndugu Diallo: “Tumempoteza Mzee hodari na mmoja wa waasisi
wa TANU ambaye mchango wake katika kuijenga TANU na baadae CCM katika shughuli za
uongozi wa nchi yetu na wananchi wake upo dhahiri.”
Ameongeza Dk. Kikwete: “Nakutumia wewe Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza salamu
zangu za rambirambi na kupitia kwako kwa wana-CCM wote kwa kuondokewa na Mzee
wetu.”
Aidha, nakuomba unifikishie pole zangu nyingi kwa familia ya Mzee Ngofilo pamoja na ndugu
na marafiki wa familia hiyo. Naelewa machungu ya familia kwa kuondokewa na mhimili wao.
Wajulishe Wananchi wa Mwanza na ijulishe familia ya Marehemu Ngofilo kuwa niko nao
katika maombolezo ya msiba huu mkubwa kwa sababu msiba wao ni msiba wangu.
Napenda pia wajue kuwa naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke pema
peponi roho ya Marehemu Masalu Ngofilo. Amen.
Imetolewa na;
Ndugu Christopher Ole Sendeka
MSEMAJI WA CCM
MJUMBE WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA,
15/04/2016