Tangu miaka ya 80 nilipojiunga na CCM,kauli mbiu yetu ilikuwa 'CCM yajenga nchi'. Kauli hii tuliambiana,tuliimbiana,tuliandikiana na kukumbushana.Tena kimatendo. Lakini sasa ni tofauti.CCM haijengi tena nchi. Kujenga nchi, kwa uelewa wangu, ni kusikiliza wananchi,kuwahudumia na kuwafanya wawe wamoja.Kufanya mambo ya kimaendeleo pamoja.
Kujenga nchi ni kuheshimu maoni ya wengine,changamoto mpya na kuzikabili kiutatuzi ili mambo ya nchi yaende mbele. CCM sasa haijengi nchi.Haisikilizi wananchi wake. Haiwaheshimu wananchi wake na kuwafanya wamoja. Inawatawanya makusudi ili kuendelea kubaki madarakani. Mbinu hii ni chakavu na itashindwa hima. CCM ile ilikuwa ikijirudi haraka na kusonga mbele.Hii ni tofauti. Haiambiwi;haisikii.
Hebu tutupe macho kwenye uandikaji wa Katiba mpya. CCM,yenye asilimia 99 ya Wajumbe wa Tume ya Katiba,imefikia kuibishia Tume na watanzania kwa ujumla. Inataka mawazo yake tu yaheshimiwe.Kwamba,kuwe na Serikali mbili na Mawaziri wawe Wabunge. Imeandaa nyaraka yake na kuwalazimisha Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya waiseme nyaraka kama ilivyo.Huku ni kuvuruga nchi.
Leo,CCM imekiuka hadi Sheria za kimataifa.Imemtumia Balozi wa China nchini kukinadi chama. Kidiplomasia,hata Waziri Bernad Camilius Membe anaweza kushuhudia, Balozi huiwakilisha nchi yake katika nchi nyingine.Balozi ni wa kitaifa na wala si wa kichama. Kumtumia kwa namna yoyote Balozi yeyote katika mikutano ya kichama,ni ukiukwaji wa sheria husika na ni kuwagawa wananchi katika minajiri ya kichama. Ni kuvuruga nchi.
Kwa leo naishia hapa. Nikihitajika kwa mjadala zaidi nitakuwa 'around'.Ijulikane kuwa sasa CCM haijengi nchi;inavuruga nchi. Ni dalili mbaya kisiasa.
Mzee Tupatupa wa Lumumba,Dar es Salaam.