CCM yafika mwisho wa barabara | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

CCM yafika mwisho wa barabara

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Dingswayo, Oct 18, 2010.

 1. Dingswayo

  Dingswayo JF-Expert Member

  #1
  Oct 18, 2010
  Joined: May 26, 2009
  Messages: 4,011
  Likes Received: 86
  Trophy Points: 145
  Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 13 October 2010

  CCM yafika mwisho wa barabara | Gazeti la MwanaHalisi


  KIONGOZI yeyote aliyekaa madarakani muda mrefu akianza kutapatapa, ujue mwisho wa utawala wake umewadia.

  Katika siku za mwisho za kuelekea uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi nchini Zambia mwaka 1991, Rais Kenneth Kaunda alifanya hila.


  Alilazimisha vyombo vyote vya habari vielekeze nguvu kwenye mafanikio ya utawala wake, na hata tafiti za asasi zilipikwa kuonyesha rais huyo wa kwanza wa Zambia huru, alikuwa ametenda makubwa na anapendwa sana na wananchi.


  Kwa kuwa Kaunda alikuwa anataka kusikia sifa nzuri, hata maofisa usalama waliacha kumpelekea taarifa za watu kuuchoka utawala wake. Alihakikishiwa ushindi wa kishindo.


  Kumbe hata wale waliokuwa wanajaa kwenye mikutano yake, wanachama wa chama chake, UNIP walikuwa wamemchoka ‘baba wa watu.'

  Kaunda alipigwa dafrau bila kujijua. Akaingia Frederick Chiluba.

  Huko India, pamoja na ukongwe wa chama cha National Congress na kazi ya kupigania uhuru, Congress kiliondolewa madarakani na chama cha Bharatiya Janata Party (BJP) katika uchaguzi mkuu mwaka 1989.


  Congress kililazimika kuungana na kikundi kilichokuwa kimejitenga; kikajijenga na kujiimarisha na kurudi tena madarakani mwaka 2004.


  Rais Eduard Shevardnadze alitawala kwa raha Jamhuri ya Georgia alipochaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1995, lakini katika uchaguzi wa mwaka 2000 alikabiliwa na shutuma nyingi hasa kwa kushindwa kupambana dhidi ya ufisadi.


  Pamoja na uzoefu wake kuwa waziri wa mambo ya nje wa uliokuwa umoja wa Soviet, mwisho wake ulikuwa mwaka 2003.


  Ilikuwa baada ya uchaguzi wa wabunge kushutumiwa na waangalizi wa kimataifa na Marekani na Umoja wa Mataifa kuafiki kwamba haukuwa huru na wa haki, wananchi wa Georgia walimweka kando Shevardnadze.


  Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete anafuata nyayo za Shevardnadze na Kaunda; hatua kwa hatua. Vyombo vingi vya habari vinatangaza habari zake kwa urefu na kuonyesha umati unaohudhuria mikutano yake.


  Vyombo vingine vya habari vimetenga kipindi maalum kwa ajili ya kueleza mafanikio yake; kwa hiyo ni yeye tu anayesikika.


  Upande wa pili kuna asasi zinazofanya tafiti za kura za maoni juu ya wagombea. Nazo baadhi zinatoa majibu ama kumpendezesha Kikwete au kutomchukiza.


  Tafiti hizo zinazoonyesha mgombea huyo wa CCM ni chaguo la wengi. Halafu jumbe fupi za simu (sms) zinasambazwa kukashfu mpinzani mkuu katika uchaguzi huo.


  Anavyojikaanga


  Katikati ya mzigo mkubwa wa gharama za elimu na afya, Kikwete pamoja na wagombea ubunge kupitia chama chake, wanahaha kuziba macho, masikio na akili za wafuasi wao kwamba haiwezekani kutoa bure elimu na afya.

  Lakini ushahidi kutoka nchi jirani, utawaumbua CCM, Kikwete na wabunge na kuwaonyesha uongo hauna maana.

  Wabishi hawa wanajua maazimio manane ya Umoja wa Mataifa (UN) chini ya Mpango wa Maendeleo ya Milenia (MDG). Mwaka 2000 wakuu wa nchi 192 walitia saini utekelezaji malengo hayo ifikapo mwaka 2015.


  Mpango huo ulifuatiwa na mkutano wa Dakar, Senegal mwaka huohuo ambako viongozi na wakuu wa nchi 164 walikutana kujadili kipengele cha elimu; namna ya kufikia mamilioni ya watoto wanaokosa elimu duniani.


  Mikakati ya wakuu wa nchi ilikuwa kuona uwezekano wa kufuta ada na badala yake kutoa elimu bure kwa watoto chini ya usaidizi mkubwa wa UN.


  Afrika na hasa Kusini mwa Jangwa la Sahara, ndiko ilibainika kati ya watoto 10, wanne watakuwa hawajaandikishwa shuleni.


  Ni kutokana na maazimio hayo ya kimataifa, mwaka 2001 serikali, iliyodai haiwezi kutoa elimu bure, ilianzisha Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (Mmem) wenye lengo la kuandikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule.


  Ni hapo shule nyingi zilijengwa, ada ikafutwa ili kuwapa wazazi unafuu wa kusomesha watoto wao.


  Mwaka 2007 serikali ikafuta mitihani ya mchujo darasa la nne na kidato cha pili kwa shule za sekondari.


  Nchini Uganda serikali, chini ya Rais Yoweri Museveni ilianzisha mpango wa elimu ya msingi kwa wote (UPE).


  Miaka 10 baadaye, yaani mwaka 2007 ikaanzisha mpango wa elimu ya sekondari kwa wote (USE) unaolenga kuhakikisha watoto wote waliofaulu wanapata nafasi ya kusoma sekondari.


  Mipango hiyo ililenga zaidi kuendeleza familia maskini. Serikali ilizitaka shule 1,000 za sekondari za serikali kupokea wanafunzi wa sekondari bure.


  Huko Rwanda, siyo tu kwamba serikali ilikuwa inatoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari hadi kidato cha tatu, bali pia posho kwa vyuo vikuu. Bali ina mpango wa kufanya marekebisho katika elimu ya vyuo vikuu.


  Nchini Malawi, elimu ya bure kwa shule za msingi nchini ilianza kutolewa mwaka 1994, Lesotho, Burundi na nchi nyingine jirani zimefuta ada kwa shule za msingi.


  Kwa nchi jirani, Kenya, serikali ya muungano wa vyama ya NARC iliyoingia madarakani Desemba 2002 ilianza kutekeleza mpango wa elimu bure mwaka 2003.


  Mwaka 2008, seriali ya umoja wa kitaifa chini ya Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu, Raila Odinga, ilianzisha mpango wa elimu bure kwa sekondari. Lengo lilikuwa kuongeza idadi ya wafunzi wa sekondari hadi milioni 1.4.


  Serikali, chini ya mpango huo inalipa ada za wanafunzi lakini wazazi wanalipa gharama za bweni kwa watoto wao.


  Wakati nchi zote jirani zinaangalia uwezekano wa kutoa elimu bure hadi vyuo vikuu, viongozi wa CCM ambao serikali yao inasimamia utekelezaji wa Malengo ya Milenia na Mikakati ya Dakar, wanakataa eti haiwezekani.


  Hatima


  CCM inaweza kuwafanya watu wote wajinga kwa wakati mmoja; inaweza kuwafanya baadhi yao wajinga wakati wote, lakini haiwezi kuwafanya watu wote wajinga wakati wote.  Nguvu kubwa ya CCM ni wanachama wake na wananchi wengine vijijini waliogubikwa na woga, ujinga na umaskini – wale ambao walitishwa tangu awali kuwa vyama vingi vitaleta vita.


  Siku watakapong'amua, kwamba sera za elimu na afya bure zinazonadiwa na Dk. Willibrod Salaa wa CHADEMA na Prof. Ibrahim Lipumba wa CUF zinawezekana, CCM itakuwa imefika mwisho wa barabara. Je, itakuwa mwaka huu?
   
 2. awesome

  awesome Member

  #2
  Oct 18, 2010
  Joined: Oct 11, 2010
  Messages: 37
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Ni kweli imefika kikomo.
   
 3. MANI

  MANI Platinum Member

  #3
  Oct 18, 2010
  Joined: Feb 22, 2010
  Messages: 6,409
  Likes Received: 1,862
  Trophy Points: 280
  "CCM inaweza kuwafanya watu wote wajinga kwa wakati mmoja; inaweza kuwafanya baadhi yao wajinga wakati wote, lakini haiwezi kuwafanya watu wote wajinga wakati wote."

  Hapo ndio wanapaswa kupaelewa ingawaje ni wagumu kuamini hivyo.
   
Loading...