CCM wakubali makosa kwanza...

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,473
39,986
Tangia sakala la "orodha ya ufisadi" lianze, serikali ya CCM imekuwa ikitoa majibu ya kukanganyana na mengine hayaingii akili hata kidogo. Majibu mengine yamejaa kiburi na dharau na mengine inabidi mtu ajiulize "walikuwa wanafikiria nini". Kwa maoni yangu kabla ya viongozi wa serikali na wa CCM kuanza kutoa majibu kuhusu tuhuma kwa viongozi 11, la kwanza ambalo wangelifanya ni kukubali tatizo kwanza, hiki kiburi wanachokionesha kuwa wao hawawezi kukosea na wengine wanadai kuwa wamekuwa waadilifu kwa miaka zaidi ya 30 ni kutufanya sisi Watanzania "hamnazo". Nimeona nijitolee kuwaonesha njia CCM ili jambo hili liishe kwa amani. Tadhali sikiliza hoja yangu kuhusu kwanini CCM wakubali makosa kwanza.
 
Mwanakijiji, unajua wakikubali makosa wanatakuwa wamejitia aibu zaidi. Lakini sasa hivi aibu yao naweza kusema ni obvious, hakuna atakayepinga. Swala ni kuwa ni vipi watapambana nayo. Lakini cha ajabu ni kuwa wameacha kulivaa tatizo na kulishughulikia wanataka kumvaa Slaa na wapinzani wote kwa ujumla. No doubt kuwa ndani ya CCM kuna wachace ambao wanakerwa na hali hii, hata hiyo list of shame sio kama imetoka kwa Slaa peke yake kama watu wanavyoweza kudhani, inawezekana kabisa walioko CCM wanaoitakia Mazuri Tanzania ndio wameitoa.
 
Mkjj, kuna kitu kinacho ni vuruga na wakati mwingine kuniudhi sana akilini kila nikikifikiria kiundani...Inakuwaje watu/viongozi hawa walio wengi hawakubali makosa yao?! Najua kuna nakala nyingine ulisha andika kuhusu 'viongozi wasiokosea na taifa lisilo hoji' kama sijakosea; kila leo hii basi nikiona madhambi mbali mbali yaliyopo lakini watu hawa wajibiki au kuwajibishwa inanishangaza na kuniudhi kweli kweli.

Kifupi ni kuwa, maadili ya kazi hayapo au yanafutika kabisa pale mtu anapokataa kuwa kafanya makosa, hali kuwepo kwake pale kumesababisha utendaji kushuka, uzalishaji kushuka na mengine mengi ambayo unaweza kujumuisha na kuyaita uzembe au ufisadi. Hamna mtu ambaye ni malaika, no one is infallible, if you fail to deliver or do a blunder then be prepared to accept the punishment accordingly. Lakini kwenye maadili yetu na kwa viongozi wetu walio wengi naona hili halikubaliki na halipo. Inasikitisha kwa kweli.

SteveD.
 
Hiii inaashiria jambo moja.

SISIEMU hawajajipanga kama wao wapendavyo Watanzania wote wajue.
SISIEMU wamechanganyikiwa na kujichanganya kama kundi la Nyumbu na Pundamilia wanao kimbia ovvyo ovyo kwa hofu ya kufanywa msosi na kundi la Simba.

Kila mtu ndani ya SISIEMU anakurupuka na kusema chochote kimjiacho akilini au anachoshauriwa na wapambe waliochanganyikiwa.

SISIEMU hawana umoja kiasi cha kuwa na sauti moja na kauri moja juu ya jambo.Wanatoa majibu ya mfa maji majibu yasiyo na mpangilio na yasiyojibu hoja ya msingi.

SISEMU kwa kawaida ni wazuri sana katika Propaganda za kisiasa. Ukali wa hoja ya Dr Slaa na namna ilivyosukwa kwa umaridadi, umakini na ushahidi wa kutosha nje na ndani unaleta kiwhewhe kwa SISIEMU kupenyeza meno na makucha yao kwa nia ya kuisambaratisha hoja.

Hoja ya Slaa ni funda iliyofungwa madhubutu ikafungika kwa SISIEMU kuifumgua bila kuonyesha aibu yao na kujianika uoza wao kwa Watanzania wote.

SISEMU wanaendelea kutoa majibu yakuokoteza ili muda ukatike na wananchi wasahau na kuona ni hadithi ndogo isiyo na mpango na isiyo na uhusiano na taabu na karaha zao.

SISEMU wangefurahi sana endapo wangefunguliwa mashitaka, kwani kwao ungekuwa ni mwanya mzuri wa kuipiga dan dana kesi na kuinyamazisha kam maji ya mtungi kama wafanyavyo juu kesi ya kada wao mnyonga Roho Brother Ditto.

Pamoja na kula kiapo cha kutosema ukweli Asilani na kusema uongo Daima chini ya alama za umasikini wa kutupwa Jembe la mkono na Nyundo ya Sido, Wamesahau kitu kimoja kidogo sana.

Uongo sikuzote haufanani.
 
Tatizo ni kwamba wakishapata hizi kazi wanafikiri wameridhishwa kwa hiyo hakuna wa kuwaondoa wala kufukuzana. Tabia hii ikitoweka tutapiga maendeleo, hawaelewi kwamba cheo ni dhamana na kama umeshindwa mwachie mwingine naya afanye.
 
CCM...Hivi ni kweli CCM ni wafisadi..Au hata wewe Unae soma hii thread Ulisha wahi Kua Fisadi?
 
CCM...Hivi ni kweli CCM ni wafisadi..Au hata wewe Unae soma hii thread Ulisha wahi Kua Fisadi?

Duhh, haya sasa makubwa.

Kama mtu amewahi ama bado ni fisadi bora atubu mapema na kurudisha kilicho chetu, kwani si mmesikia kuwa list nyingine inakuja , waweza kuumbuka........
 
CCM...Hivi ni kweli CCM ni wafisadi..Au hata wewe Unae soma hii thread Ulisha wahi Kua Fisadi?

jee wewe ni fisadi au uliwahi kuwa fisadi au una mpango wa kuwa fisadi?

maswali kama haya majibu yake baadhi ya wakati huwa maudhi kwa muulizaji
 
Ufisadi ni unaanza na Utashi, unaishia na kupindisha sheria na taratibu ili kulinda matokeo ya ufisadi.

Siyo kweli kwamba utashi wa watu wote unawasukuma kuhujumu taifa, vilevile si uongo kwamba baada ya kuhujumu watu wanatumia vyeo na mamalaka waliyo nayo kujikinga na nguvu ya mkondo wa sheria.

Imani kwamba watu wote ni waovu asili na chimbuko lake ni SISIEMU.

Kwa kutawanya uongo kwamba mtanzania yeyote ni duni wa fikra na siku zote ataishi maisha bora kwa udokozi ujambazi na ufisadi, SISEMU wanaeneza sumu ya kuenzi uovu wao ili waonekane Malaika watukufu mbele ya wananchi.

SISIEMU wana pandikiza kwa hila wazo kwamba utawala wowote nje ya SISIEMU utakuwa hatari kwa Amani na Utulivu wa nchi.

Amani na utulivu maana yake nini?!?
 
Umwinyi, usultan na unyambaa ndio unaoimaliza serikali ya CCM. Ni ajabu watu wenye akili timamu kukataa kwamba kuna matatizo ya kiutawala au kiutendaji ndani ya serikali.

Sasa kama hakuna rushwa Takukuru ya nini na ya nani?
Kama kuna utawala bora Wizara ya kushughulikia utawala bora ni ya nini?

Wameomba wasaidiwe kuwatambua wafisadi na wala Rushwa. Majina wamepewa na maelezo ya kutosha, wanataka nini tena? Tukae kimya na kupiga makofi?

Uongozi na ahadi za kinafiki zinaipeleka Tanzania kuzimu. Ni vyema viongozi wetu wakajua kwamba Tanzania ya leo sio ya jana. Watu wamebadilika na kilio chetu kikubwa ni maendeleo kwa kila mtanzania.

Hatuko tayari kuwa wakimbizi kwa sababu ya maamuzi ya wachache. Wakubali kwamba muda wa uongozi wa ndio mzee umekwisha.

Tutahoji na tutahoji bila kujali uswahiba wala cheo cha mtu.
Hakuna sababu yeyote ya tanzania kuwa masikini, isipokuwa uongozi mbovu ndio uliotufikisha hapa tulipo. Wameshindwa kubadilika na kutoa watendaji wote wabovu na tunalazimika kuchukua madaraka na kuwapa wanaoweza.

CCM ijue kwamba tatizo la wananchi kwa sasa ni maisha bora, ambayo wao wanatuletea maigizo wakubali kuachia ngazi kwani kazi imewashinda.
 
hivi najiuliza wapinzania wakiingia madarakani hawatokuwa mafisadi ? yaani watakuwa wanafanya tu kila kitu right ? nadhani wajibu yao yatakuwa ndio kwamba watatumikia taifa kwa moyo mmoja bila ufisadi, lakini je ni kweli ?
 
hivi najiuliza wapinzania wakiingia madarakani hawatokuwa mafisadi ? yaani watakuwa wanafanya tu kila kitu right ? nadhani wajibu yao yatakuwa ndio kwamba watatumikia taifa kwa moyo mmoja bila ufisadi, lakini je ni kweli ?

bila ya shaka si kweli. Hakuna mwanadamu mwenye madaraka ambaye hana mwelekeo wa kutumia vibaya madaraka hayo. Kubwa ambalo tutalitaka kwa watakaoibadili CCM ni kutengeneza miundo ya kuhakikisha kuwa ufisadi wa kipuuzi kama huu tunaoushuhudia hautokei. Mojawapo ni kupitisha sheria ya mgongango wa Kimaslahi, kukataza Rais na Waziri Mkuu kutumia ofisi zao kufanya biashara zao, na kuhakikisha mikataba yote inayoingiwa na serikali yetu inaweza kupitiwa na kuvunjwa na Bunge. Unaonaeje kuhusu angalau mambo hayo matatu?
 
ok....that sounds good on the outside, lakini on the real note: mtalewa madaraka kama waliopo sasa hivi ! kwa hiyo unaweza ukaniambia maneno matamu hapa hadi milele lakini that wont satisfy me unless muanze na muendelee kushirikiana na the so called mafisadi mpambane nao wakiwa madarakani ili kutuonyesha kwamba kweli kazi mnaiweza lakini anything less, lets roll the dice !
 
Kinacho-iua Tanzania na serikali ya sasa iliyopo madarakani ni kulewa madaraka. Uhakika wa kiongozi kwamba hakuna wa kuhoji wala kumwajibisha. Hii ndio hali iliyozaa uzembe na ufisadi wa hali yajuu.

Nchi zilizoendelea nazo zina mapungufu yake ya uongozi lakini kila mmoja anawajibika kwa uozo wake.

Kinachotakiwa kutokea Tanzania ni uwajibikaji wa viongozi wa serikali na umma katika maslahi ya Taifa. lazima viongozi waheshimu madaraka yao ktk kuhudumia jamii na wajue wapo kwa maslahi ya watu.

Hivi sasa hawafanyi kazi kwa ajili yetu bali wao wenyewe. Haijalishi nani atakuwepo madarakani ila tunataka katiba itakayoheshimu raia wake na kutunza mali za nchi.

Swala la kwamba wapinzani wakiingia ikulu mambo yatakuwa mstari sio kweli. Lakini hakuna maendeleo bila ushindani na hakuna mshindi kama hakuna wa kumshinda. Upinzani unaleta changamoto ya kujua kwamba nisipofanya vizuri nitatemwa. Kwahiyo tutajua mengi tutahoji mengi na watakwenda wengi jela bila kujali itikadi na maendeleo yatakuja.

Wazee walio jaa CCM ambao hawataki mabadiliko ndio wanaoiua nchi. Dunia imekuwa ndogo kama kiganja, watanzania wengi wameshaonja maisha bora na demokrasia ya kweli kwenye nchi za watu sasa wanataka hali hiyo iwepo nyumbani. Viongozi wetu kwa makusudi hawataki kwa sababu ya kufichiana uozo.
 
Mzee Mwanakijiji,
Nadhani itabidi tukubaliane kuwa serikali siyo ya CCM ni ya watanzania wote ila inaongozwa na CCM. Kwa nini nimesema hivyo? Watanzania walio wengi huwa wana uoga wa kuiondoa CCM madarakani kwa sababu mawazoni mwao wanajua ukiondoa CCM unaondoa serikali na mtu anajiuliza ni kivipi CHADEMA au CUF itaunda serikali mpya? Chama kikiingia madarakani kazi yake kubwa ni kuongoza serikali. Unaposema CCM wakubali makosa ni makosa gani hayo unayoongelea? Sera au usimamizi wa sera? Hivi tunao uhakika wowote kama Balali ni mwanachama wa CCM? Lakini tunajua anaongoza idara ya serikali na siyo idara ya CCM. Ni kitu cha kuuzunisha tumefika mahali mtanzania anaona BOT ni mali ya CCM, BOT ni mali yetu wote lazima tupiganie iendeshwa kwa manufaa yetu wote.
 
BAADA ya wapinzani kushusha tuhuma nzito dhidi ya viongozi kadhaa wa serikali, viongozi wa CCM wamezinduka kama watu waliokuwa katika usingizi wa mang’amung’amu.

Katika kuzinduka kwao, kila mmoja anasema limtokalo mdomoni mpaka wanafikia mahali wanahitilafiana na kuacha swali, ni nani anayesema kweli?

Nionavyo, tatizo la CCM ni kutokubali kukosolewa, yaani kukubaliana na hali halisi ya nchi ilivyo hivi sasa.

Linapokuja suala la kuwa na katiba mpya, CCM huwa kama mtu aliyetoneshwa kidonda kisichopona (donda ndugu). Badala ya kujibu hoja, wao hujibu mashambulizi katika kile kionekanacho kama ‘jino kwa jino’.

Madai ya wapinzani kuhusu ufisadi wa baadhi ya viongozi wa serikali, CCM inataka ushahidi upelekwe mahakamani.

Wapinzani walitaka kuutoa bungeni wakafanyiwa mizengwe. Wanapokuja kwa wananchi kueleza yaliyojiri ndani ya jumba lile la kutunga sheria, CCM inasema eti walishindwa kutoa ushahidi, mara walishindwa kwenye uchaguzi na sasa wanawalaghai wananchi.

Nani anayelaghai kati ya mwenye kutaka kutoa ushahidi na yule anayekataa kuusikiliza ushahidi huo?

Kama kumbukumbu zangu ziko sahihi, Rais Jakaya Kikwete aliwahi kusema kuwa inashangaza kusikia suala linaloihusu polisi moja kwa moja watu kutaka iundwe tume ya uchunguzi.

Kama Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amegundua upotevu/ubadhirifu wa fedha kwa kununua vitu visivyoonekana au kutorejesha fedha za masurufu bila maelezo, kwa nini polisi hawaitwi ili watimize wajibu wao?

Kila mwaka, ripoti ya Mkaguzi Mkuu huonyesha mamilioni ya fedha yaliyopotea, ama kwa uzembe, ubadhirifu au wizi wa kutumia kalamu.

Mpaka sasa si mamilioni tena, bali mabilioni kadhaa ambayo yangeweza kutumika kwa maendeleo ya nchi. Hakuna yeyote aliyefikishwa mahakamani kwa kosa la ufisadi wa fedha za umma.

Hali hiyo inawafanya wajanja wachache waendelee kujichotea fedha kila mwaka na itaendelea hivyo mpaka itakapokuja serikali yenye watendaji makini wasio wa ‘ponda mali kufa kwaja’ kwa maana ya ‘chukua chako mapema.’

Kwa woga walio nao CCM ndiyo maana hata majimbo ya uchaguzi wameyataifisha kwa kuyaita ‘yao’ kana kwamba wapinzani si raia wa nchi hii, na kwa hiyo hawastahili kugombea wala kuchaguliwa! Kauli za lazima ‘tukomboe majimbo yetu’ ni ushahidi kuwa CCM inataka kutawala milele.

Kwa nini? Kwa sababu inaogopa kama itashindwa na wapinzani kushika madaraka, wakubwa wataulizwa juu ya mali walizojilimbikizia na ubadhirifu mwingi waliofanya wakati wa utawala wao.

Labda niwakumbushe wana CCM jambo moja muhimu. Kule Taiwan, kuna chama kiitwacho Kuomintang (KMT), yaani chama cha umma kilichotawala kwa miaka 50 mfululizo - 1950 - 2000.

Chama hicho kilitwaa madaraka kwa katiba iliyoundwa mwaka 1947 na kufanyiwa marekebisho mara nne 1992, 1994, 1997 na 1999. KTM ilianzishwa na Dk. Sun Yatsen mwaka 1894 na iliadhimisha karne moja (miaka 100) Novemba 24, 1994.

Lakini pamoja na uzoefu wa miaka yote hiyo katika siasa na kuwa madarakani kwa miaka 50 mfululizo, ilifikia mwisho wake mwaka 2000 kwa kushindwa na Chama cha DPP (Democratic Progressive Party) kilichokuwa na umri wa miaka 14 tu tangu kilipoundwa.

Nataka kuwaambia CCM kuwa kila chenye mwanzo hakikosi kuwa na mwisho na ngoma ivumayo sana haikeshi.

Kama chama kilichoundwa miaka 100 iliyopita na kuwa na uzoefu wa utawala kwa miaka 50 kimeangushwa na chama kichanga, basi siku za CCM kuangushwa kwa kura, tena za kishindo, ziko kwenye kizingiti cha mlango.

Hata kwa mtu aliyekimbia umande, yaani ambaye hakuuona mlango wa darasa, hawezi kudanganywa katika kuhesabu fedha zake. Anaijua fedha kuanzia senti moja mpaka noti ya shilingi elfu kumi.

Vivyo hivyo, ingawa si Watanzania wote, ni wachumi, lakini wanajua uchumi wa nchi umeporomoka na unaendelea kuporomoka, tena kwa kasi.

Kama uuzaji wa bidhaa na mazao mbalimbali nje ya nchi umeshuka kwa asilimia 39.8 hadi kufikia dola milioni 5.7 za Marekani katika kipindi cha mwezi Julai mwaka huu, ni vipi serikali inajigamba kuwa uchumi ‘unapaa?’

Aidha, iwapo uuzaji wa pamba katika kipindi hicho ulipungua kutoka tani 115,952 hadi tani 26,443 (tofauti ya tani 89,509) na korosho kupungua kutoka tani 84,200 mpaka tani 57,400 (tofauti ya tani 26,800) ni vigumu kuamini kuwa uchumi wetu unakua.

Maana uchumi waweza kukua iwapo tunauza mazao na bidhaa nyingi nje na tunanunua bidhaa chache kutoka huko. Hata taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inathibitisha kupanda kwa mfumuko wa bei kutoka asilimia 5.9 mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu na kufikia asilimia 9.0 mwisho wa mwezi Julai.

Sasa uchumi huo unakua kinyumenyume au kwa miujiza ya Mungu?

Turejee kwenye mada ya wapinzani dhidi ya ubadhirifu wa mali ya umma kwa upande mmoja na CCM dhidi ya wapinzani kwa upande wa pili.

CCM inataka wapinzani wapeleke ushahidi polisi. Ule uliotolewa hadharani kwa wananchi au wa ziada? Kama ni wa ziada mbona ndiyo itaumbuka zaidi?

Tukubaliane na CCM kuwa wapinzani wapeleke ushahidi polisi. Kama mkuu wa wilaya anaweza kuamuru mtu kuwekwa ndani na polisi ikatii bila kutafuta uhalali wa kukamatwa na kutiwa ndani, itakuwaje kwa wapinzani wanaoonekana mbele ya macho ya CCM kuwa mahasimu wao? Watatendewa haki?

Majaji, mkuu wa Takukuru, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Mkuu wa Upelelezi nchini, Msajili wa vyama vya siasa na Mkuu wa Usalama wa Taifa wote wameteuliwa na Rais.

Bunge limetawaliwa na CCM na hoja yoyote ya wapinzani hushindwa kutokana na uchache wao, kwani wenzao hukutana kama ‘kamati ya chama’ na kupanga jinsi ya kuwavunja nguvu.

Kinachotetewa ni masilahi ya chama na si ya wananchi. Kwa hali hii ni nani wa kumfunga paka kengele mkiani?

Idi Amin Dada (Mungu amrehemu) alipotoa vitisho na hata kuivamia Tanzania kule Kagera katika kile kilichokuja kujulikana kama Vita ya Kagera, aliwauliza askari wake kuwa ndege ya kivita ingechukua dakika ngapi kutoka Entebbe mpaka Dar es Salaam na kurudi baada ya kuangusha mabomu.

Vitisho vyake vilitupa muda wa kujiandaa kwa vita na tulipokuwa tayari, tulitangaza nia ya kupigana naye, sababu na uwezo na ndivyo ilivyokuwa. Aliikimbia nchi yake akisahau kofia na bastola yake chumbani!

Waziri mmoja wa serikali ya awamu ya pili, alitangaza kuwa siku inayofuata atakwenda kukagua ghala moja la chakula la kampuni maarufu nchini, baada ya kuambiwa kuwa kampuni hiyo inauza vyakula vilivyopitwa na wakati.

Kilichofanyika ni tajiri wa kampuni ile kukodi vibarua waliofanya kazi usiku kucha kuhamisha vyakula vibovu na kuvipeleka walikojua. Waziri alipokwenda kesho yake, akakuta ghala jeupe.

Hii ina maana gani? Ni kama kumwambia mwenye ghala: “Wewe, ficha vyakula vyako vibovu ili nikija kesho na waandishi wa magazeti tusikute kitu.” Na kwa Idi Amin vilevile ni kama alituasa tujiandae kwa vita.

Tahadhari hizi hazina tofauti na TAKUKURU inapowatahadharisha viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na viongozi wenye majumba makubwa ya thamani ya kuogofya kuwa, itawafuata baada ya kazi waliyo nayo kukamilika.

Kwa hiyo, inawapa nafasi wanaotuhumiwa na kushukiwa wajiandae au kuchukua hadhari kabla ya hatari. Atakamatwa nani kwa mpango huo?

Hebu fikiri mtuhumiwa wa ubadhirifu wa fedha za umma, anatetewa kwa nguvu zote na serikali akiachwa aendelee na shughuli zake za kiofisi akiwa na uwezo wa kuharibu ushahidi wote unaohusu tuhuma dhidi yake.

Kwa nchi zinazojua maana ya demokrasia, watu kama hao hujiuzulu au hulazimishwa kujiuzulu ili uchunguzi ufanyike vizuri. Si hivyo kwa Tanzania yetu!

Kama kweli CCM inataka kujikosha, ikubali madai ya wapinzani yachunguzwe na tume huru ili ukweli uwekwe hadharani na sheria ifuate mkondo wake.

Tofauti na hili, itakuwa porojo zisizokuwa na maana zaidi ya kuwasononesha wananchi walio wengi.

marobarnabas@yahoo.com
0756 855 314
0784 334 096
 
Back
Top Bottom